Hakuna njaa lakini tuchukue tahadhari ya ukame

Muktasari:

  • Hoja zinazotolewa na wanasiasa hasa kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe zimejikita zaidi kwenye kupanda kwa bei za vyakula katika maeneo mbalimbali nchini.
  • Hata hivyo, hoja hiyo haiwezi kuchukuliwa moja kwa moja kwamba kuna njaa nchini.

Kumekuwa na mjadala mpana kuhusu suala la upungufu wa chakula hapa nchini; wakati wanasiasa wakisema kuna njaa, Serikali imekanusha suala hilo na kusisitiza kwamba chakula kipo cha kutosha, wananchi waendelee kufanya kazi.

Hoja zinazotolewa na wanasiasa hasa kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe zimejikita zaidi kwenye kupanda kwa bei za vyakula katika maeneo mbalimbali nchini.

Hata hivyo, hoja hiyo haiwezi kuchukuliwa moja kwa moja kwamba kuna njaa nchini.

Ninakubaliana na msimamo wa Serikali kwamba Tanzania hakuna njaa kwa sasa kwa sababu chakula bado kinapatikana katika sehemu mbalimbali licha ya kupanda kwa bei ya baadhi ya vyakula kama vile mahindi.

Kama mwaka jana ulikuwa na mvua nzuri na mavuno mazuri, ni wazi kwamba chakula hicho ndicho kinachotumika sasa. Kwa msingi huo, tunaweza kuzungumzia habari za njaa baada ya mavuno ya msimu huu.

Hata hivyo, ni vyema wakulima na Serikali wakachukua tahadhari juu ya tishio la ukame lililopo sasa ili kuepukana na baa la njaa ambalo linaweza kujitokeza siku zijazo kwa kupanda mazao stahimilivu au yale ya muda mfupi.

Kupanda kwa bei za vyakula kunaweza kuwa kiashiria cha kupungua kwa chakula lakini haina maana kwamba kuna njaa. Dhana ya ‘njaa’ ina maana kwamba chakula hakuna kabisa hata kama una fedha ya kununua. Bado nchi yetu haijafikia hatua hiyo.

Kupanda kwa bei za vyakula kunaweza kuwa na sura mbili, aidha kupungua kwa chakula nchini au kuimarika kwa bei ya mazao ya wakulima kama ambavyo wamekuwa wakililia miaka mingi bila mafanikio.

Ni muhimu kwa wanasiasa kuwa wa kweli na kueleza kama kuna viashiria vya njaa waviite ‘viashiria’ na siyo njaa kama inavyoelezwa. Pia, mifano ya halmashauri au wilaya kadhaa isiwe hoja ya kuhitimisha kwamba Tanzania kuna njaa.

Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Dk Charles Tizeba alitoa takwimu kwamba mwaka jana Tanzania ilikuwa na ziada ya chakula tani milioni tatu na kati ya Oktoba na Novemba 2016, tani milioni 1.5 ziliuzwa nchi jirani zilizokuwa na uhaba wa chakula.

Dk Tizeba alikiri kwamba kuna halmashauri 43 nchini ambazo zilikuwa na upungufu wa chakula, lakini katika maeneo mengi ya nchi, chakula kilipatikana cha kutosha.

Alisema tofauti iliyopo sasa ni kupanda kwa bei kutoka wastani wa Sh65,000 kwa gunia mwaka jana mpaka wastani wa Sh85,000 kwa gunia mwaka huu.

Kuhusu suala la ukame, waziri huyo mwenye dhamana alisema Serikali inafanya jitihada za kuwahamasisha wakulima kwenye maeneo yanayokabiliwa na ukame kulima mazao yanayostahimili ukame.

Ukame wa sasa unaweza kusababisha mavuno yasiwe mazuri mwaka huu. Ni wakati wa kuhamasisha wakulima kugeukia kilimo cha umwagiliaji au kulima mazao yanayostahimili ukame ili kuepukana na upungufu wa chakula ambao unaweza kujitokeza siku za usoni.

Septemba mwaka jana, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA), Dk Agnes Kijazi alisema mvua zitachelewa kuanza na zikianza zitakuwa chini ya wastani. Aliwashauri wakulima kuzingatia ushauri wa maofisa kilimo na kuhifadhi akiba ya chakula waliyonayo.

Ni jambo muhimu kwa Taifa kuwa na mkakati maalumu wa kilimo cha umwagiliaji na kukipa nguvu ili wakulima waachane na kilimo cha kutegemea mvua. Jambo hili likifanikiwa litaimarisha uhakika wa chakula wakati wote.

Peter Elias anapatikana kwa simu namba 0763891422 au baruapepe: [email protected]