Monday, March 20, 2017

Harambee ya uchangiaji wanafunzi kufanyika Dar

 

By Tausi Ally, Mwananchi

Dar es Salaam. Taasisi za Serikali na zisizo za kiserikali, viongozi wa dini na wadau wa elimu wametakiwa kujitokeza kuchangia vifaa vya shule Machi 25, katika Viwanja vya Leaders Club ili kuwasaidia wanafunzi wanaosoma na kuishi katika mazingira magumu vijijini.

Blessing Mlanga ambaye ni mwanzilishi wa taasisi ya Furaha, amesema lengo la harambee na ukusanyaji wa vifaa vya shule ni kusaidia kuwavalisha sare wanafunzi 1,000 wa shule za msingi Wilaya ya Kibondo mkoani Kigoma.

Amesema uchangiaji huo utaanza saa tatu asubuhi hadi saa 11 jioni na kwamba, iwapo mzazi au mlezi atakuwa na sare za shule zilizotumika ambazo zina ubora, mabegi ya shule, soksi, viatu vyeusi na hata vitabu avipeleke ili viweze kuwasaidia watoto wanaoishi kwenye mazingira magumu.

Mkazi wa jijini Dar es Salaam, Masunga Ntarambe amwsema utaratibu wa kusaidia katika suala la elimu hapa nchini haupo, lakini katika nchi ya Kenya umekuwapo miaka mingi.

-->