Hatuhitaji misaada bali biashara ya haki

Muktasari:

  • Halihitaji kwenda mbali kulibaini hilo. Fedha zilizotolewa katika bajeti ya Serikali ya mwaka 2016/17 iliyomalizika Juni, imeashiria kuwapo kwa tatizo hilo la kiuchumi.

Tanzania ni nchi tajiri kwa rasilimali, lakini lofa wa fedha wazungu wanasema resource rich, cash poor. Hii inathibitishwa na utafiti mbalimbali uliofanywa miaka ya karibuni.

Halihitaji kwenda mbali kulibaini hilo. Fedha zilizotolewa katika bajeti ya Serikali ya mwaka 2016/17 iliyomalizika Juni, imeashiria kuwapo kwa tatizo hilo la kiuchumi.

Theluthi mbili ya Watanzania wanaoishi chini ya mstari wa umasikini au Dola moja ya Marekani kwa siku ni uthibitisho wa kuwapo kwa tatizo hilo, licha ya utajiri mkubwa wa rasilimali na maliasili zilizopo nchini.

Tatizo hilo; tajiri wa mali, lofa wa fedha, watafiti wamelipachika jina linalobeba sifaya “laana ya rasilimali (resource curse) haliikumbi Tanzania pekee. Karibu nchi zote zinazo endelea ambazo zimebahatika kuwa na utajiri wa rasilimali, zinalo.

Tatizo hilo ni kubwa zaidi kwa nchi za Afrika kutokana na sababu mbalimbali, zikiwamo kukosa uzalendo na kukithiri kwa rushwa na ufisadi pamoja na mifumo dhaifu ya utawala wa kidemokrasia inayotetea usiri hata katika masuala yanayohitaji uwazi na uwajibikaji.

Kwa mfano, mtafiti na mchumi mashuhuri duniani, Joseph Stiglitz aliyewahi kupata tuzo ya Nobel mwaka 2001, amezitahadharisha Tanzania, Uganda, Ghana na Msumbiji kuwa makini na katika mikataba ya uvunaji wa rasilimali zao na wawekezaji kutoka magharibi.

Profesa huyo wa uchumi wa Chuo Kikuu cha Columbia, Marekani kwa kutanguliza uzalendo na kutetea na kulinda masilahi ya nchi na watu wake. Kwamba uvunaji huo wa rasilimali hautozinufaisha nchi zao bali mataifa tajiri yenye ‘makengeza ya kikoloni’ ya kuvuna na kuondoka na mali siyo kuendeleza mataifa husika.

Stiglitz anatambua kwamba nchi nyingi kati ya hizo ‘zimeshajifunga’ katika mikataba mibovu isiyo na masilahi kwa nchi zao iliyopewa kinga (sanctity of contracts).

Pamoja na hilo, bado nchi hizo zina uwezo na uhalali wa kudai na kulazimisha mapitio ya mikataba yote ya uvunaji wa madini na rasilimali nyinginezo ili kulinda masilahi yake.

Inapothibitika kuwapo kwa udanganyifu au wizi kinyume na mikataba iliyopo pamoja na kasoro zote, nchi inayoibiwa inayo haki ya kusitisha mikataba hiyo na kuipitia upya.

Ushauri wa Stiglitz ni kwamba, linapo tokea tatizo kama hilo, suluhu iliyopo ni moja tu; kupitiwa upya kwa mikataba hiyo. Kama hilo litakuwa gumu au pakatokea kigugumizi cha aina yoyote, dawa iliyobaki ni kutoza kodi kubwa (windfall profit tax) kwa mapato yoyote yatakayopatikana.

Marekani imewahi kupata fursa hiyo. Imefanyika hivyo pia katika nchi za Bolivia na Venezuela, Israel na Australia. Kila nchi duniani, inalinda rasilimali na maliasili zake zisiporwe kwa udanganyifu na mataifa mengine au kampuni za kimataifa.

Hakuna mkataba unaokubalika duniani kama unahalalisha uporaji na wizi wa maliasili na rasilimali za nchi nyingine. Kwa miongo minne au mitano iliyopita, Botswana imenufaika kutokana na rasilimali zake baada ya kufanya mapitio ya mikataba yote ya uvunaji wa rasilimali na kufikia makubaliano yenye masilahi kwa pande zote mbili.

Wanaodai Tanzania haina uwezo wala teknolojia kuchimba madini au kuyachenjua ili kuyaongezea thamani ni wapotoshaji.

Miaka hamsini iliyopita, Korea Kusini ilikuwa inazalisha zaidi mpunga na kuuza nje ya nchi kuliko ilivyokuwa viwandani. Wangekubali kutii imani potofu ya kuzalisha zaidi mpunga badala ya kuelekeza nguvu zao katika ubunifu, utafiti na viwanda, hivi sasa ingekuwa bado nchi masikini inayotegemea kilimo.

Kwasababu walithubutu, leo ni miongoni mwa nchi zilizoendelea kiviwanda duniani. Mtafiti mwingine maarufu duniani, Jason Hickel, pia amezitahadharisha nchi masikini juu ya uvunaji wa rasilimali zake huku zikiendelea kuwa ombaomba.

Utafiti wa kulinganisha fedha zinazopokelewa na nchi zinazoendelea kutoka nchi zilizoendelea kwa mfumo wa misaada, uwekezaji, biashara za kimataifa na mapato mengine, ni chache zikilinganishwa na zinazotoka kupitia biashara za kimataifa, uvunaji wa rasilimali na maliasili, uwekezaji.

Kwa mwaka 2012 pekee, nchi zinazoendelea zilipoteza Dola trilioni mbili za Marekani zaidi kuliko ilizopata kutoka nchi zilizoendelea.

Nchi masikini inahitaji zaidi kufanya biashara ya haki na si misaada ambayo haina nia njema. Jitihada zilizoanzishwa na Rais John Magufuli ni mwelekeo sahihi katika kulinda masilahi ya Watanzania na vizazi vijavyo.

Mikataba iliyopo isiporekebishwa, Tanzania itaendelea kuwa masikini; bajeti yake ikitegemea wahisani na mikopo kutoka nje huku wananchi wake wakiwa hohehahe.

Kufanikisha mabadiliko haya, ushirikiano wa wataalamu wote, uchumi, sheria na biashara unahitajika.

Mwandishi ni mchambuzi wa masuala ya uchumi. Anapatikana kwa 0683 555124