Haya yafanyike kukomesha wizi wa watoto majumbani

Ngollo John

Muktasari:

Mathalan, mkoani Mwanza, kwa muda wa miezi miwili watuhumiwa wawili wamekamatwa wakiwa wameiba watoto wa waajiri wao. Tukio la kwanza lilitokea Julai 3 ambapo mwanamke mkazi wa kijiji cha Mbugani, Tarafa ya Buchosa wilayani Sengerema, Paulina Mashiku (27) alikamatwa na anashikiliwa na polisi kwa tuhuma za wizi wa mtoto wa kiume mwenye umri wa wiki tatu.

Hivi karibuni kumeibuka matukio ya wafanyakazi wa ndani kuiba watoto wa waajiri wao na kutokomea kusikojulikana. Hata hivyo, polisi kwa kushirikiana na raia wema wamekuwa wakifanikiwa kuwakamata baadhi ya watuhumiwa na kuwafikisha mbele ya vyombo vya sheria.

Mathalan, mkoani Mwanza, kwa muda wa miezi miwili watuhumiwa wawili wamekamatwa wakiwa wameiba watoto wa waajiri wao. Tukio la kwanza lilitokea Julai 3 ambapo mwanamke mkazi wa kijiji cha Mbugani, Tarafa ya Buchosa wilayani Sengerema, Paulina Mashiku (27) alikamatwa na anashikiliwa na polisi kwa tuhuma za wizi wa mtoto wa kiume mwenye umri wa wiki tatu.

Aliyekuwa kamanda wa polisi mkoani Mwanza, Ahmed Msangi alisema mtuhumiwa baada ya kuhojiwa alidai kufanya kitendo hicho kutokana na kukaa muda mrefu bila kupata mtoto.

Tukio jingine lilitokea Agosti 5 katika Kijiji cha Kisesa Jiwe la Mkaa ambapo Neema Selemia alikamatwa na polisi eneo la Nyegezi akidaiwa kuiba mtoto mwenye umri wa miezi minane wa mwajiri wake.

Akihojiwa polisi mtuhumiwa huyo alidai kupitiwa na shetani na ndipo alipofanya kitendo hicho.

Mbali na tukio hilo, mkoani Shinyanga pia mfanyakazi wa ndani alipatikana wilayani Kahama akiwa ameiba mtoto wa miezi saba wa mwajiri wake.

Matukio hayo na mengine mengi ambayo hayaripotiwi polisi yamekuwa yakitokea katika maeneo mbalimbali nchini ambapo mbali na hao wanaoiba na kutokomea, pia wapo wanaowaua watoto na waajiri wao.

Mfanyakazi wa ndani huko Kisumu nchini Kenya anadaiwa kumuua mwajiri wake Elizabeth Achieng pamoja na kichanga chake chenye miezi mitatu.

Inadaiwa mfanyakazi huyo alianza kwa kumpiga mtoto mpaka akamuua kisha akamfuata mama ambaye alimchoma kisu mara kadhaa kisha kumchoma na kitu kinachodhaniwa ni pasi ya umeme au tindikali.

Hayo ni baadhi tu ya matukio ambayo yamewahi kutokea ndani ya muda mfupi na taarifa zake kuripotiwa kwenye mamlaka husika kwa ajili ya ufuatiliaji pamoja na hatua za kisheria.

Vitendo kama hivi vinatakiwa kukemewa ili kukomesha matukio ya wizi na ukatili unaofanywa na watu hao ambao wamekuwa wasaidizi wa karibu hasa waajiri wanapowaamini na kuwaachia majukumu yote ya nyumbani pale wao wawapo kazini.

Huenda vitendo hivi vinafanyika kutokana na baadhi ya waajiri kukiuka Sheria ya Mtoto namba 21 ya mwaka 2009; Sheria ya Ajira na Uhusiano Kazini ya mwaka 2004 kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2017; Waraka wa Mishahara wa mwaka 2013 pamoja na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977.

Inadaiwa na watetezi wa haki za mtoto kuwa matukio ya namna hiyo yanachangiwa na baadhi ya waajiri kushindwa kuwalipa wafanyakazi hao mishahara yao kwa mujibu wa sheria.

Wanadai kuwa wengi wamekuwa wakiwanunulia nguo na zawadi ndogondogo huku wengine wakiwapiga, kuwanyima chakula na kuwatukana hali inayochochea kuwepo kwa chuki na hatimaye utekelezaji wa matukio hayo.

Nilipomuuliza mratibu wa kupinga ukatili wa kijinsia kutoka shirika lisilo la kiserikali la Plan International, Gadily Kayanda juu ya kuongezeka kwa matukio hayo alisema wapo wafanyakazi wanaotumwa na watu ambao hawajabahatika kupata watoto na wengine wanafanya hivyo kwa chuki binafsi ili kuwakomoa waajiri kutokana na kushindwa kutimiza sheria na kanuni za ajira.

Kwa mujibu wa Kayanda, mnyororo wa ukatili huanzia kwa baba au mama wa familia anapoamua kumgandamiza mfanyakazi wa ndani na kuwatetea watoto wake. Hali hiyo hubadilika pale wazazi hao wasipokuwepo ambapo wafanyakazi huwageukia watoto wa waajiri wao.

Jambo hilo pia lilizungumziwa na mkuu wa dawati la jinsia na watoto mkoani Mwanza, Bethnsimbo Shija aliyeeleza kuwa matukio hayo yanachangiwa na waajiri wenyewe.

Mkuu huyo wa dawati hilo lililopo chini ya Jeshi la Polisi alisema vitendo hivyo vinaweza kuzuilika endapo tu kila mmoja kati ya pande hizo atatambua wajibu wake.

Alisema takwimu zilizowasilishwa polisi mwaka jana zinaonyesha matukio 41,000 yaliripotiwa kati ya hayo 13,000 yalihusisha watoto.

Kuna kila sababu ya jamii kushikamana kutokomeza vitendo hivyo ambavyo kwa namna moja au nyingine vinasababisha jamii iwe na woga wa kuajiri wafanyakazi wa ndani.

Waajiri pia wanatakiwa kuhakikisha wanawalipa wafanyakazi wao mishahara iliyopangwa kwa mujibu wa sheria ili kutokomeza vitendo hivyo ambapo inaarifiwa kuwa wengi wa wanaofanya kazi za ndani hawana mikataba maalumu ya kimaandishi na wanalipwa chini Sh40,000 tofauti na kiwango kilichopendekezwa kwenye sheria ya ajira.

Tunaweza kuwa na jamii bora na tulivu endapo tutahakikisha tunatimiza wajibu wetu.