Hedhi mzigo mzito kwa wanafunzi wengi wa kike

Mwalimu Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Bahi, Srella Suleiman akizungumza na wanafunzi wa kike wanaoishi hoteli.​

Muktasari:

DONDOO

  • 2012 serikali ilipitisha mpango mkakati wa miaka mitano kuboresha maji na usafi katika shule za msingi na sekondari ikiwa ni hatua ya kuimarisha utoaji wa taaluma, mahudhurio na afya za watoto shuleni.
  • 2016 serikali pia ilitoa mwongozo wa kitaifa kuhakikisha kiwango cha chini cha upatikanaji wa maji na vifaa vya usafi mashuleni. Hata hivyo baadhi ya watendaji serikalini wanasema utekelezaji wa mipango hiyo umekuwa ukitegemea fedha za nje na hakuna bajeti ya ndani inayotengwa.

Saa 5.30 asubuhi, niko ofisini kwa Mwalimu Grace Mbega. Huyu ni mwalimu wa afya wa Shule ya Msingi Chifuduka, wilayani Bahi katika Mkoa wa Dodoma.

Mara anaingia mwanafunzi wa kike. Baada ya kutuamkia anasema: “Mwalimu naomba kile kitu, naumwa.” Mwalimu Grace akacheka na kumuuliza kwani hujui kutengeneza za kienyeji?

Yule mwanafunzi alisema anajua isipokuwa amesahau na hata kama angekumbuka namna ya kutengeneza, asingeichukua kwani hakujua kama angekuwa katika hali hiyo kwa siku hiyo.

Baadaye nilikuja kubaini kwamba binti huyo mdogo alikuwa akiomba taulo ya kike (pedi) baada ya kuingia ghafla katika mzunguko wake wa hedhi akiwa tayari amefika shuleni.

Mwalimu Grace alifungua droo yake, akachukua kitambaa kigumu, mkasi, pamba na uzi. Huku akimuelekeza, alianza  kutengeneza taulo ya kike ya asili kwa kukata kitambaa kwa mtindo wa duara. “Ukishakata kitambaa chako, unaanza kukifuma vizuri pembeni,” alisema Grace huku akifuma kitambaa hicho na wakati huo akimuelekeza mwanafunzi huyo aliyekuwa amesimama pembeni yake.

Alitengeneza vishikio viwili alichukua pamba na gozi, kisha akapachika pamba iliyowekwa kwenye gozi vizuri. Baada ya hapo alimuelekeza namna ya kuitumia na kumkabidhi.

Msichana huyo aliondoka ofisini kwa mwalimu wake huku akifurahi. “Nilishawafundisha, nikaa nao kiurafiki, wale walio kwenye umri wa kupevuka na waliopevuka wanaelewa namna ya kutengeneza,” anasema mwalimu huyo.

Hata hivyo, Mwalimu Grace anasema huwa anawasaidia taulo za dharura tu, na kwamba, mabinti wengi hutumia zaidi vitambaa kwa sababu hawamudu gharama za kununua pedi. “Hata hizi za asili tunazotengeneza hapa shuleni zinagharama japo ni kidogo,” anasema.

Hedhi ni kati ya vikwazo vinavyowafanya wanafunzi wengi wa kike kukatisha masomo yao hasa wale wanaosoma maeneo ya vijijini.

Taasisi ya Uangalizi wa Haki za Binadamu ya Human Rights Watch (HRW) katika ripoti yake ya mwaka huu kuhusu hali ya utoaji wa elimu ya sekondari nchini, inasema mazingira ya shule nyingi si rafiki kwa mwanafunzi wa kike hasa akiwa katika hedhi.

Ripoti hiyo inasema usimamizi mzuri wa usafi wa hedhi unahitaji maji ya kutosha, mazingira safi na faragha ili kuruhusu wasichana kubadili au kutupa kwa ustaarabu taulo au pedi wakiwa shuleni.

Utafiti uliofanywa na Shirila la Maendeleo la Uholanzi la SNV katika wilaya nane nchini, unabainisha asilimia 98 ya shule za wilaya hizo hazina miundombinu rafiki kwa wasichana wanapokuwa kwenye hedhi.

Mwalimu wa afya wa shule ya Sekondari ya Magaga, Wende Mbuna anasema kwenye shule hiyo wanafunzi wengi wa kike huwa hawagusi shule wakati wanapokuwa hedhi.

“Pedi za ziada zipo lakini anapewa moja tu, akija kuomba akati inapomtokea dharura. Umaskini ni tatizo kubwa hivyo, vifaa duni vya kujisitiri huwafanya waamua kukaa nyumbani,”anasema Mbuna.

Ilibainika kuwa wanafunzi wengi hawamudu gharama za taulo za kike ambazo ni kati ya Sh2,500 hadi 3,500 kwa paketi moja.

“Natumia vitambaa na huwa nahofia kama nikibaki darasani naweza kuchafuka kwa kupata madoa kwenye sketi yangu ya shule halafu nichekwe, ndio maana naona bora nibaki nyumbani,” anasema mmoja wa wanafunzi katika shule ya Sekondari Chonama.

Msichana huyo (jina linahifadhiwa) huwa anatumia kati ya siku nne hadi tano kila mwezi kwa hedhi na anasema katika siku hizo huwa haendi shule.

Anasema hajawahi kubahatika kutumia taulo ya kike (pedi) ya dukani tangu alipopevuka miaka miwili iliyopita.

Msichana mwingine wa  darasa la saba katika shule ya msingi Chifuduka anasema pia hajawahi kutumia taulo za dukani na kwamba mama yake amekuwa akisema hawezi kumnunulia kwasababu hana fedha.

“Natamani sana kutumia za dukani kwa sababu nitakuwa na uhakika wa kutochafuka nikiwa darasani. Hizi za vitambaa inabidi ubadilishe kila mara, na kwa kubadilishia hakuna labda chooni nako kuna harufu kali,”anasema.

Anasema kukuwa hakuna mitihani darasani kwao, kipindi cha hedhi huwa haendi shule. “Huwa nakaa kimya simwambiagi mama wala baba. Huwa nasema kichwa kinauma basi nabaki nyumbani,”anasema msichana mwingine.

Mganga mfawidhi wa Hospitali Teule wa Hospitali ya Kigoma Ujiji, Dk Kilawa Shindo alisema zipo athari nyingi za watoto wa kike au wanawake kutumia vitambaa wakati wa hedhi.

Dk Kilawa anasema mwanamke anayetumia vifaa hivyo ni rahisi kupata maambukizi  kwenye kizazi ‘Pelvic Inflamatory Desease)  na  kwenye njia ya mkojo  endapo kitambaa hicho kitakuwa na vimelea vya wadudu kama bacteria na fungus.

“Pia mavitambaa ni rahisi kuloa hali inayoweka eneo la ukwe kuwa na unyevu na kuhatarisha mwanamke kupata fungus kisha kuwashwa sehemu zake za siri,” anasema.

Anasema kuwa inashauriwa ikiwa mwanamke atatumia vitambaa badala ya pedi ni sharti kifuliwe kwa maji safi, kikauke na kupigwa pasi ili kuua vimelea vyote vinavyoweza kuzalisha wadudu.

Kuhusu maumivu makali ya tumbo, Dk Kilawa anasema kitaalamu inaitwa Dysmenorrhea, hali hii inatokana na misuli ya ukuta wa uzazi kujiminya wakati wa kuuvunja ukuta uliokuwa umeandaliwa kupokea kijusi endapo mwanamke angekutana na mwanaume.

Afisa Afya wa tarafa ya Bahi Sokoni, Mudila Mundeli anasema yapo yapo magonjwa yanayoweza kuwapata watoto wa kike kutokana na matumizi ya vifaa vya hedhi vizivyo salama.

“Magonjwa yanawakumba sana kwa sababu maji na vifaa wanavyotumia wengi sio salama hii ni hatari pia,” anasema.

Anasema hata wakitoa elimu kwa watoto na wazazi wao, ugumu unabaki kwenye hali ya uchumi kwa kuwa wengi hawamudu gharama.

“Ndio maana tunasisitiza kila shule iwe na kitengo cha afya kwa sababu hiki kinasaidia walau wanafunzi hasa wa kike kupata elimu inayowahusu,”anasema.

Ni suala la kawaida

March 8 mwaka jana Tanzania iliungana na nchi nyingine duniani kuadhimisha siku ya hedhi ili kuelimisha jamii kwamba jambo hilo ni la kawaida katika mfumo wa maisha ya jinsia ya kike, na hutokea kila baada ya siku 28.

Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Chifuduka, Daniel Mchomvu anasema hedhi sio siri tena shuleni kwake. “Hata hiyo mtoto mdogo muulize kuhusu hedhi anajua. Tumeamua kuwafundisha ukweli wajitambue tangu wadogo. Wasione ajabu,” anasema na kuongeza:

“Tulimteua mwalimu wa kike, kazi yake kubwa ni kukaa na mabinti hapa shuleni ili  waliopevuka awasaidie elimu ya afya na wanapokuwa hedhi waone ni kawaida, wasiache masomo”.

Kwa upande wake Mwalimu Grace anasema katika jitihada za kutoa elimu kwa jamii, waliitisha kikao cha wazazi ili wajadili suala la hedhi kwa watoto wao na namna wanavyoweza kuwasaidia, wahudhurie masomo.

“Baba au mama yeyote anaweza kuzungumza na mwanae wa kike, hedhi sio siri tena,”anasema.

Mzazi, Jeremia Matonya anasema hajawahi kujua siku za hedhi za binti yake. Hata hivyo anakiri kuwa kila mwezi kuna siku binti yake huwa huwa haendi shule.

“Naanzaje kumuuliza eti upo mwezini? Hiyo ni kazi ya mama yake. Akilala ndani najua anauma,”anasema Matonya akiona ajabu kwa namna anavyoelimishwa kwamba, hedhi ni kitu cha kawaida.

Anasema hajawahi kutoa fedha yoyote kwa ajili ya kumnunulia taulo binti yake, japo ni mwaka wa pili tangu apevuke.

Mwalimu Grace analazimika kutumia muda mrefu, kuwalekeza namna ya kuwajali mabinti zao japo ukweli unabaki palepale, gharama za kumudu.

Ofisa elimu wa Sekondari Wialaya ya Bahi, Hassan Mohamed anasema walimu wakiume na wakike kwenye wilaya hiyo wameshafundishwa namna ya kuwasaidia wasichana wanapokuwa hedhi.

Mtandao wa maji na mfumo wa majitaka nchini (TAWASANET) katika mapendekezo yake yaliyotokana na utafiti wake kuhusu miudombinu katika shule kwa ajili ya manbinti wakati wa hedhi, unapendekeza kutungwa kwa sera zitakazolazimisha ujenzi wa shule kuzingatia mahitaji hayo.

Kadhalika Tawasanet wanapendekeza kuwapo kwa mfumo rasmi wa masuala ya hedhi kuzungumzwa kwa uwazi katika utoaji wa elimu, ili kuvinja ukimya ambao umekuwa sababu ya ‘mateso’ kwa wanafunzi wa kike.

Ofisa elimu wa Sekondari Wilaya ya Bahi, Hassan Mohamed anasema walimu wakiume na wakike kwenye wilaya hiyo wameshafundishwa namna ya kuwasaidia wasichana wanapokuwa hedhi ikiwa ni hatua ya kwanza ya utekelezaji.

Hata hivyo, wakati wa maashimisho ya Tamasha la Jinsia, halmashauri za Wilaya ya Kishapu na Kisarawe zilipata tuzo baada ya kuweza kutenga bajeti na kuanza kutoa bure pedi kwa wasichana wote waliopevuka shuleni.