Heshima ya soka Afrika iliyozoeleka ipo Russia

Muktasari:

  • Timu zinazoliwakilisha Bara la Afrika katika Fainali za Kombe la Dunia 2018 ni Misri, Morocco, Nigeria, Senegal na Tunisia. Kati ya timu hizi mojawapo inatakiwa kutwaa ubingwa wa dunia 2018!.

Timu 32 zitakazoshiriki Fainali za Kombe la Dunia 2018 nchini Russia zimeshafahamika huku Afrika yaani Shirikisho la Soka Afrika (CAF) likiwakilishwa na timu tano, Shirikisho la Soka Asia (AFC) timu 5, Shirikisho la Vyama vya Soka vya Kaskazini, katikati ya Marekani na Visiwa vya Caribbean (CONCACAF) timu tatu, Shirikisho la Soka la Amerika ya Kusini (CONMEBOL) timu 5 na Shirikisho la soka la Ulaya (UEFA) timu 14.

Timu zinazoliwakilisha Bara la Afrika katika Fainali za Kombe la Dunia 2018 ni Misri, Morocco, Nigeria, Senegal na Tunisia. Kati ya timu hizi mojawapo inatakiwa kutwaa ubingwa wa dunia 2018!.

Ndiyo, timu hizi zimeshikilia mapambano ya Afrika katika kutafuta haki ya kuongezewa nafasi ya kupeleka timu zaidi katika Fainali za Kombe la Dunia, pia kulipatia heshima inayostahili Bara la Afrika katika mchezo wa soka.

Bila timu hizi kufanya vizuri katika Fainali za Kombe la Dunia 2018, tutaendelea kukosa heshima tunayostahili katika mchezo wa soka kwani hatujawahi kuingiza timu katika hatua ya nusu fainali ya Fainali za Kombe la Dunia tangu fainali hizo zilipoanzishwa mwaka 1930.

Katika fainali zilizopita za Kombe la Dunia 2014 zilizofanyika nchini Brazil, Afrika tulishindwa kuingiza timu hata katika hatua ya robo fainali wakati katika fainali zilizofanyika Afrika Kusini 2010 tuliingiza timu moja katika hatua ya robo fainali ambayo ni Ghana.

Unaweza kuona kwa uwazi kabisa kwamba Afrika lipo katika kutafuta heshima linayostahili kwani ni aibu kubwa kwa Bara la Afrika lenye nchi 54 na vipaji lukuki vya wachezaji soka, lakini linashindwa kufanya vizuri katika Fainali za Kombe la Dunia.

Nalipenda Bara la Afrika na nawapenda wachezaji soka wa Waafrika, lakini naona kuna mambo muhimu kuhusu soka la Afrika ambayo kwa muda mrefu sasa yamekuwa hayafanyiwi kazi na hivyo kusababisha timu za Afrika kushindwa kutamba katika Fainali za Kombe la Dunia.

Ni wazi wachezaji wa Afrika wamekuwa wakicheza kwa nguvu, huku wakishindwa kutumia akili inayotakiwa kutwaa ubingwa wa dunia au kufanya vizuri na kuhakikisha wanafikisha timu zao katika hatua ya nusu fainali ya Fainali za Kombe la Dunia.

Soka halihitaji nguvu tu, ila akili ya juu, ninadhani hii ndiyo sehemu wachezaji wa Afrika wanatakiwa kuifanyia kazi kwa kiwango cha juu ili kufanya vizuri katika Fainali za Kombe la Dunia.

Najua wachezaji wa Afrika wanaweza kushindana sehemu yoyote duniani, kama wakitambua umuhimu wa matumizi ya akili ya juu uwanjani, nidhamu, shauku, uamuzi na heshima.

Baadhi ya wachezaji wa Afrika wanashindwa kuzichezea timu zao za taifa kwa shauku, heshima na unyenyekevu kama wanavyozitumikia klabu zao za Ulaya kwa wale wanaocheza soka Ulaya.

Pia, timu zetu za Afrika zina makosa mengi katika safu ya ulinzi, ubunifu katika kiungo na ujanja wa kupiga na kuzitumia pasi za mwisho, pia timu zetu zinashindwa kuzuia mbinu za pasi za mwisho, mipira ya kona na hata mipira ya adhabu na kuzifanya zishindwe kuwa bora mbele ya timu za Ulaya na Amerika Kusini.

Kubwa zaidi ni wachezaji wa Afrika kufanya makosa mengi katika mechi.

Sawa soka ni mchezo wa makosa, lakini makosa yayoyofanywa na wachezaji wa timu za Afrika katika Fainali za Kombe la Dunia huwagharimu na hivyo kuaga mapema fainali hizo