Hili la timu ya Zanzibar lisifumbiwe macho

Muktasari:

  • Michuano hiyo imeibua shaka juu ya umri sahihi wa wachezaji wanaoshiriki.

Michuano ya Vijana chini ya miaka 17 ya Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (Cecafa), imeanza na inaendelea kwenye Uwanja wa Muyinga huko Burundi.

Michuano hiyo imeibua shaka juu ya umri sahihi wa wachezaji wanaoshiriki.

Tumesikia yaliyozikuta timu za taifa za Vijana ya Zanzibar na Ethiopia. Hali ikiwa mbaya zaidi kwa Zanzibar ambayo imeondolewa kabisa katika michuano, kutozwa faini na kufungiwa pia.

Hali hii ni ya fedheha kwa nchi, viongozi wa ZFA na makocha waliohusika katika ngazi ya klabu na Taifa.

Ni jambo ambalo lilikuwa halikutarajiwa kwa upande wa Zanzibar kwa sababu wengi tunaamini kuwa huko visiwani mchezo wa mpira wa miguu unapendwa sana na vijana kuanzia umri mdogo. Tuliamini vijana hao ambao huonyesha vipaji na hatimaye kuendelezwa wapo.

Pamoja na madhara ambayo Zanzibar (na Tanzania kwa ujumla) na wadau wanayapata ya kutoamiwa, waliofanya hivyo wajue kwamba kuna madhara makubwa zaidi kwa wachezaji ambao wanarudisha umri wao chini.

Mara kadhaa wachezaji wa aina hiyo hawadumu kiuchezaji kwa muda mrefu kwa sababu miili ya wachezaji huwa inakua kulingana na umri halisia hivyo kushindwa kuhimili mazoezi yenye kuwaletea utimilifu.

Hali hiyo husababisha mchezaji kusika kuandamwa na majeruhi ya mara kwa mara.

Ninashangaa, katika karne ya sasa ya sayansi na teknolojia ambako kuna njia nyingi za kuutambua umri wa mchezaji, bado viongozi wanafanya kosa kama hilo, pengine kwa sababu ya muonekano wa maumbile.

Wengi wanaweza kuwalaumu moja kwa moja ZFA kwa kasoro hiyo, binafsi nawatupia lawama hiyo kwanza makocha wa klabu/timu walikotoka wachezaji hao.

Hii inatokana na ukweli kwamba makocha wengi wanaofundisha klabu na timu za vijana hawawi makini katika kubaini umri sahihi wa wachezaji inavyopaswa. Ni jambo rahisi sana kama kocha husika ni mwadilifu. Ataomba cheti cha kuzaliwa cha mchezaji na kama hana, alipokwenda kuandikishwa shule ya awali au msingi, lazima aliandikisha mwaka wake wa kuzaliwa.

Makocha ambao si waadilifu na wanataka kuonyesha timu zao zimeshinda na ndio wanaokuwa wa kwanza kudanganya umri.

Kundi la pili ambalo linatakiwa kuibeba lawama hii ni benchi zima la ufundi (likijumuisha kocha mkuu na wasaidizi wake – kocha msaidizi na daktari wa timu- na meneja) kwa sababu wao ndio waliotakiwa kuhakikisha kwamba wanahakikiki umri sahihi wa wachezaji wao.

Hakuna njia kwa kundi hili kuikwepa lawama hiyo moja kwa moja kwa sababu ndilo lililopewa dhamana ya kuteua wachezaji na hatimaye kuwachagua wale wenye vigezo.

Hilo sasa limeshatokea na hakuna jinsi, bali ni kuhakikisha kwamba jambo kama hilo halijitokezi tena.

Mfano mzuri wa kujifunza kutokana na makosa ni kukumbuka jinsi timu ya Serengeti Boys ilivyoondolewa licha ya kufuzu kwenda kucheza fainali Gambia kutokana na mchezaji mmoja, Nurdin Bakari kudanganya umri.

Kutoka kipindi hicho, Tanzania haijafanya kosa hilo hadi makala haya yanapoandikwa.

Ushauri wangu kwa makocha wa timu zote za vijana, ni vyema kuzingatia umri kwa sababu kwa kufanya hivyo tutakuwa tumewasaidia wachezaji kucheza kwa muda mrefu na watakuwa na manufaa zaidi kwa klabu na Taifa.

Njia za mkato zina gharama kupata mafanikio na hizi ndizo gharama zake. Vijana wajengwe lakini si kwa kutimia ubabaishaji kama huu ambao hauna maana kabisa kwao na Taifa kwa ujumla.