Mwananchi -

Hili la ving’amuzi Serikali iliangalie upya

Tuesday December 5 2017

By Mwananchi

        Serikali imefanya mambo kadhaa katika sekta ya habari, ikiwamo kuanzisha Sheria ya Huduma za Habari ya mwaka 2016.

Uanzishwaji wa sheria hiyo unalenga kuweka wigo mpana wa upatikanaji wa habari ukizingatia matakwa ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 ambayo inatoa haki ya uhuru wa mawazo kwa Watanzania.

Ni ndani ya Katiba hiyo, ibara ya 18(2) inaeleza kuwa “kila raia anayo haki ya kupewa taarifa wakati wote kuhusu matukio mbalimbali nchini na duniani kote ambayo ni muhimu kwa maisha na shughuli za wananchi, na pia juu ya masuala muhimu kwa jamii.”

Serikali mara zote imesimamia msingi huu wa Katiba na ndiyo maana ikatoa fursa ya kuwapo kwa vyombo vingi vya habari na pia uhuru mkubwa kwa wananchi wake kuhusu suala hilo.

Hata hivyo, uwapo wa taarifa kwamba takribani theluthi moja ya watumiaji wa ving’amuzi nchini hawatumii tena vifaa hivyo kutazama luninga, kikiwa ni kiwango kikubwa kuwahi kurekodiwa ndani ya miaka mitano iliyopita, inatatiza suala la upatikanaji wa habari.

Mwenendo huo, unaotajwa kupaa kwa kasi ndani ya miaka mitatu iliyopita, unahatarisha upatikanaji wa habari kwa wananchi kupitia luninga na hivyo kuwaweka katika mazingira magumu ya kutojua nini kinachoendelea duniani sanjali na kutopata habari zinazoweza kuathiri au kuwa na msaada katika maisha yao. Uchambuzi wa takwimu za robo ya pili ya mwaka 2017 za Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) umebaini kuwa idadi ya ving’amuzi vinavyonunuliwa inaongezeka kila mwaka, lakini ukuaji huo unaathiriwa na kasi ya kupaa kwa ving’amuzi visivyotumika kwa muda mrefu.

Takwimu hizo zinabainisha kuwa hadi kufikia Desemba mwaka 2016 Tanzania ilikuwa na ving’amuzi milioni 1.7. Hata hivyo watumiaji 500,000 walikuwa hawavitumii kwa wakati huo (sawa na asilimia 29.4 ya ving’amuzi vyote vilivyokuwa vimenunuliwa).

Idadi ya watu wenye ving’amuzi lakini hawavitumii ilianza kupanda miaka miwili iliyopita kutoka asilimia sifuri mwaka 2014 hadi asilimia 29.4 mwaka 2016 huku baadhi ya wananchi wakieleza kuwa ukata umesababisha kutotumia vifaa hivyo vya digitali.

Mwaka 2014 ving’amuzi vyote vilivyokuwapo nchini vilikuwa vinafanya kazi.

Ikiwa sababu kubwa ya wananchi kushindwa kumudu gharama za ving’amuzi ni ukata, hata vile ambavyo ‘bando’ lake la chini linapatikana kwa bei ndogo, basi Serikali inapaswa kuliangalia kwa jicho la tatu suala hili ambalo ni la kikatiba.

Ni wazi kwamba watoa huduma ya habari kwa kutumia ving’amuzi wanawajibika kujiendesha kibiashara, lakini pia kwa kuwa ni haki ya wananchi kupata habari, chombo pekee kinachoweza kuwawezesha kupata haki hiyo ni Serikali.

Ni vyema Serikali ikaangalia namna inavyoweza kulishughulikia suala hili, kwa ama kuwapunguzia kodi watoa huduma ili baadhi ya ‘chaneli’ za luninga ziendelee kupatikana bila malipo au itoe ruzuku kwa watoa huduma hao mahsusi kwa ajili ya ‘chaneli’ hizo.

Wakati moja kati ya mambo hayo mawili likifanyiwa kazi, wananchi waachiwe haki yao ya kikatiba ya kupata habari bure kupitia ‘chaneli’ hizo hususan zile za Kitanzania.     

Advertisement