Hoja Tanzania inyimwe misaada si mwafaka

Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu

Muktasari:

  • Lissu mwenye wadhifa wa Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), alitoa tamko hilo wakati akilalamikia kamatakamata ya viongozi wa Chadema, akidai vitendo hivyo ni kukandamizwa kwa demokrasia nchini, huku akitoa mfano wa Afrika Kusini ilivyotengwa wakati wa utawala wa makaburu kwa kuendesha siasa za ubaguzi.

Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu alinukuliwa na vyombo vya habari mapema wiki hii akitoa maneno makali dhidi ya Serikali. Lissu ambaye pia ni mbunge wa Singida Mashariki, alitoa tamko kwa niaba ya chama chake akiitaka jumuiya ya kimataifa kuinyima Tanzania misaada.

Lissu mwenye wadhifa wa Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), alitoa tamko hilo wakati akilalamikia kamatakamata ya viongozi wa Chadema, akidai vitendo hivyo ni kukandamizwa kwa demokrasia nchini, huku akitoa mfano wa Afrika Kusini ilivyotengwa wakati wa utawala wa makaburu kwa kuendesha siasa za ubaguzi.

Mwanasheria huyo alilalamika kuzuiwa vyama vya upinzani kufanya mikutano ya ndani ya siasa huku viongozi wa CCM wakiruhusiwa kufanya mikutano hiyo bila kubughudhiwa na vyombo vya dola.

Juzi, Serikali ilitoa kauli kumjibu Lissu huku ikionya wale wanaotumia uhuru wao vibaya na kusisitiza kuwa itaendelea kuenzi na kuilinda misingi ya demokrasia, uhuru wa watu na kuwapa fursa wananchi kushiriki katika uchumi wa Taifa.

Tunaamini Lissu ambaye ni mwanasheria gwiji na mwanasiasa aliyejijengea heshima na mvuto katika jamii, alikuwa na njia nyingi za kutumia ili kufikisha ujumbe wake kwa Serikali au hata kwa jumuiya ya kimataifa.

Hoja ya kutaka Serikali ya Rais John Magufuli inyimwe misaada tunaona haistahili na tunadhani kwamba mwanasheria huyo gwiji na mwanasiasa nguli, hakupaswa kuitamani njia hiyo. Ni ukweli usiopingika kuwa ikitokea hilo la kunyimwa misaada likadhiri, watakaoumia ni Watanzania hasa maskini, kundi ambalo ndilo kubwa zaidi.

Kwa waliofuatilia hotuba ya Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango akiwasilisha Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha wa 2017/18, watakumbuka kwamba aliwataja washirika wa maendeleo ambao wanatoa fedha nyingi kwa mfumo wa kusaidia bajeti ya Serikali na umuhimu wao katika shughuli za maendeleo.

Ingawa Lissu hakutaja aina ya misaada anayotaka isimame, lakini tunachofahamu kuna misaada mingi ikiwamo ya kiuchumi, kitalaamu, kijeshi, ushauri na misaada ya kibinadamu. Pia, Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) linaisaidia Tanzania chini ya Mpango wa Ushauri wa Kisera (PSI).

Si dhamira yetu kujenga Taifa la kupenda kupokea misaada, lakini kilichotusukuma kupinga hoja ya Lissu ni kwamba iwapo wahisani watasimamisha misaada yao ambayo tayari ipo kwenye mipango ya maendeleo, maana yake ni kwamba watakaoumia ni Watanzania na si wanasiasa pekee.

Watanzania wana matatizo mengi, ikiwamo ukosefu wa ajira, uhaba wa dawa hospitali na ubovu wa miundombinu ambayo yote yameainishwa chini ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa mwaka wa fedha wa 2017/18 kuwa ni vipaumbele vya msingi katika kumkomboa Mtanzania aliye kwenye dimbwi la umaskini.

Miradi mikubwa kama ya ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha Standard Gauge, miradi ya chuma ya Liganga na makaa ya mawe ya Mchuchuma na uanzishwaji wa kanda maalumu za kiuchumi havitawezekana kirahisi kama tutaomba kukatiwa misaada.

Tunaamini Lissu ana njia nyingi za kufikisha ujumbe wake na hata kutafuta mbinu za kukutana na wenye mamlaka ili kuwakosoa kwa mujibu wa sheria pale wanapokuwa wameteleza tukiamini kuwa Serikali ni sikivu.