Hongera HESLB kwa kukubali rufaa

Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Abdul-Razaq

Muktasari:

Kwa mujibu wa HESLB, wanafunzi 1,847 ka ya hao walioshinda rufaa ni wa mwaka wa kwanza ambao mikopo yao ina thamani ya Sh6.84 bilioni.

        Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) imetangaza orodha yenye wanafunzi 2,679 waliopata mikopo ya jumla ya Sh9.6 bilioni baada ya kukamilika uchambuzi wa rufaa walizokata kupinga kunyimwa mikopo.

Kwa mujibu wa HESLB, wanafunzi 1,847 ka ya hao walioshinda rufaa ni wa mwaka wa kwanza ambao mikopo yao ina thamani ya Sh6.84 bilioni.

HELSB imesema wanafunzi 832 ni wale wanaoendelea na masomo, lakini hawakuwa na mikopo katika miaka iliyopita.

Bodi hiyo imesema kuwa wanafunzi wanaoendelea na masomo wamepata mikopo yenye thamani ya Sh2.76 bilioni na kwamba fedha zimeshatumwa vyuoni. Kukamilika kwa rufaa zao kunafanya jumla ya wanafunzi 33,200 wa mwaka wa kwanza kuwa wamepangiwa mikopo ya jumla ya Sh108 bilioni kwa mwaka 2017/18 hadi sasa na bajeti ya jumla kwa wanafunzi wote kwa mwaka 2017/18 ni Sh427.54 bilioni.

Tunapenda kuipongeza bodi ya mikopo, kwanza kwa kuweka mfumo huo wa kupata maoni ya wanafunzi ambao hawakuridhika na jinsi wachambuaji walivyofikia uamuzi wa kutowapa mikopo.

Tunaamini kuwa mfumo huo ni wa wazi na unaofuata haki hivyo wale ambao wameshinda rufaa zao walistahili kupata mikopo na ambao hawajashinda, hawakustahili.

Kitendo cha kuruhusu rufaa ni kizuri kwa kuwa kinaipa bodi nafasi nzuri ya kupitia upya uchambuzi wake wa wanafunzi wanaostahili kupata na wasiostahili, kuangalia udhaifu ulipotokea na kutathmini kama umekuwa wa mara kwa mara ili kuchukua hatua za kurekebisha na pia unajenga imani kwa wanafunzi kuwa wakati mwingine hunyimwa mikopo kimakosa na hivyo wanaweza kukata rufaa.

Pili, uamuzi wa kuweka hatua ya rufaa inamaanisha kuwa wanafunzi wanapata uzoefu wa jinsi ya kuingiza taarifa zao wakati wakiomba mikopo kwa kuwa pengine wengine hunyimwa kutokana na kutoweka vizuri taarifa zao pamoja na vielelezo, hivyo wanapokata rufaa hupata fursa zaidi ya kurekebisha maombi yao.

Kukubali rufaa zaidi ya 2,600 kunamaanisha kuwa wakati bodi inapotangaza orodha ya kwanza ambayo hulalamikiwa kwa kuwa na idadi ndogo, hakumaanishi kuwa ni mwisho au ina upungufu wa fedha, bali baadhi hukosa kutokana na kasoro au udhaifu wa kupitia vizuri maombi.

Wanafunzi hawana budi kuwa makini katika ujazaji taarifa zao wakati wanapoomba mikono ili kupunguza rufaa ambazo pia hutumia rasilimali nyingi za Serikali wakati wa kuzipitia.

Pia tunaishauri bodi iendelee kuweka mifumo mizuri ya ushirikishwaji wanafunzi katika kuhakiki taarifa zao ili kujenga imani zaidi kwa wananchi kwamba hata kidogo kinachopatikana kinatolewa kwa njia ambazo ni za haki na uwazi.

Bodi haina budi pia kutafuta vyanzo zaidi vya fedha kwa ajili ya kuongeza kiwango cha kukopesha wanafunzi kinachotolewa kwa mwaka kwa kuwa wahitaji ni wengi lakini wanufaika ni wachache.

Kutegemea ruzuku pekee ya Serikali kutaifanya bodi iendelee kusaidia wanafunzi wachache na kusababisha wengi ambao hawana uwezo kushindwa kuendelea na masomo na hivyo kushindwa kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa Taifa kwa kutumia ujuzi ambao wangeupata vyuoni.

Kama tulivyoishauri bodi, Serikali pia haina budi kuangalia jinsi ya kuongeza wigo wa vyanzo vya fedha kwa ajili ya wanafunzi wa vyuo vya elimu ya juu. Ruzuku pekee haiwezi kutosheleza mahitaji ya wanafunzi kwa kuwa ni wengi.

Serikali inaweza kujadiliana na taasisi za fedha kuangalia jinsi zinavyoweza kushiriki katika utoaji mikopo.