MAONI: Hongera Serikali, sasa juhudi ziwe katika usimamizi

Muktasari:

  • Mbali ya mkataba huo wa uundwaji wa meli mpya, pia katika utiaji saini huo ulioshuhudiwa na Rais John Magufuli jijini Mwanza na maelfu ya wakazi, meli nyingine mbili za Mv Butiama na Mv Victoria zitakarabatiwa.

Serikali ya Tanzania imeweka historia nyingine baada ya jana kutia saini mkataba utakaowezesha kuundwa meli kubwa kwa ajili ya kusafirisha abiria na mizigo katika Ziwa Victoria.

Mbali ya mkataba huo wa uundwaji wa meli mpya, pia katika utiaji saini huo ulioshuhudiwa na Rais John Magufuli jijini Mwanza na maelfu ya wakazi, meli nyingine mbili za Mv Butiama na Mv Victoria zitakarabatiwa.

Aidha, baadaye kampuni iliyoshinda zabuni ya kujenga meli na kukarabati nyingine mbili itajenga chelezo yaani sehemu ambapo meli hiyo itaundwa na nyingine zitakuwa zinakarabatiwa zikipata hitilafu.

Mradi huu unatarajiwa kuwafuta machozi Watanzania waliopata msiba mkubwa wa kuondokewa na wapendwa wao Mei 21, 1996 baada meli ya Mv Bukoba kuzama katika ziwa hilo na kusababisha vifo vya watu zaidi ya 800 na upotevu wa mizigo na mali nyingine.

Moja ya sababu kubwa ya meli ile iliyokuwa tegemeo kubwa kwa usafiri kati ya Mwanza na Bukoba na ambayo ilizama kilomita 30 hivi kabla ya kutia nanga katika bandari ya Mwanza ni kwamba ilizidisha abiria na mizigo.

Pengine ili kuondokana na adha ile na kuepuka yasijirudie ya Mv Bukoba, Serikali imekuja na mradi mkubwa wa ujenzi wa meli kubwa inayojengwa miaka 22 tangu maafa ya awali, ambayo itakuwa na uwezo wa kubeba abiria 1,200 na mizigo tani 400 pamoja na magari madogo 20.

Hii ni kwa sababu itakuwa na urefu wa mita 90 yaani mita 10 kasoro kuwa na sawa na urefu wa uwanja wa mpira na kimo cha mita 10.9 sawa na jengo la ghorofa tatu. Si hivyo tu, meli hiyo mpya itakuwa na kasi zaidi kwamba itakuwa na uwezo wa kutumia saa sita kati ya Mwanza na Bukoba tofauti na ile ya zamani ambayo ilikuwa inatumia kati ya saa 10 hadi 12.

Tunaipongeza Serikali kwa mradi huo mkubwa wenye lengo la kurahisisha usafiri wa watu na mizigo baadhi ikiwa ni malighafi za viwandani, kukuza uchumi na biashara.

Tunajua huu ni mwendelezo wa juhudi za Serikali katika ujenzi wa miundombinu ya barabara na reli ya kisasa pamoja na kununua vyombo vikubwa vya usafiri maana hivi karibuni ilizindua meli katika Ziwa Nyasa, na kwa ajili ya usafiri wa anga ilinunua ndege mpya. Mbali ya kununua ndege inajenga na kukarabati viwanja vya ndege ili usafiri wa ndani usiwe shida huku wale wa kimataifa wataunganishwa kwa ndege kubwa aina ya Dreamliner.

Pomoja na pongezi, juhudi zinapaswa kuimarishwa katika usimamizi wa miradi hii yote inayojengwa kwa kodi za Watanzania.

Haiwezekani Watanzania wajifunge mikanda kwa kukatwa kodi kugharimia miradi mikubwa kama hiyo halafu wakabidhiwe watu wasiojali thamani na kujitoa kwa Watanzania kufanikisha miradi hiyo.

Tumeshuhudia mara nyingi usimamizi huwa mzuri siku za mwanzo wa kila jambo, lakini kadri siku zinavyokwenda hujengeka tabia ya uzembe, bora liende yaani watendaji kutowajibika ipasavyo.

Mfano, meli ya Mv Bukoba iliyojengwa mwaka 1979 ilikuwa na uwezo wa kubeba tani 850 za mizigo na abiria 430, lakini kadri siku zilivyopita idadi ya watu ilikuwa ikizidishwa. Tunashauri uzembe ule usirudiwe.