Hongereni waandaaji SportPesa

Muktasari:

  • Kutoa ufadhili kwa timu hizi katika ushiriki wa Ligi Kuu za nchi zao ni msaada mkubwa kwa klabu husika ukizingatia kwamba kuendesha klabu ya mpira wa miguu katika ngazi hiyo ni gharama kubwa.

Kampuni ya SportPesa imeleta aina mpya ya uwekezaji katika medani ya mpira katika ukanda huu wa Afrika Mashariki, hususan nchi za Kenya na Tanzania ambapo timu nne kutoka katika kila nchi zinapata udhamini wa kushiriki Ligi Kuu za nchi zao.

Kutoa ufadhili kwa timu hizi katika ushiriki wa Ligi Kuu za nchi zao ni msaada mkubwa kwa klabu husika ukizingatia kwamba kuendesha klabu ya mpira wa miguu katika ngazi hiyo ni gharama kubwa.

Ufadhili wa SportPesa ni ufadhili ambao umekuwa ni wa aina yake kwa sababu zifuatazo:

Kuaandaa mashindano maalumu baina ya timu za nchi husika

Pamoja na kutoa ufadhili wa timu nne za Ligi Kuu kutoka katika kila nchi, wadhamini hawa kuanzia mzimu wa kwanza wa udhamini, tumeshuhudia klabu nne kutoka katika kila nchi zinakuwa na mashindano ya pamoja na mshindi hupewa nafasi ya kucheza na klabu ya kongwe ya Everton ya Uingereza ambapo mwaka jana mshindi Gor Mahia alipata fursa ya kucheza na Everton uwanja wa Taifa uliofanyika Dar-es-salaam mwaka 2017.

Mashindano hayo mwaka huu yamefanyika Kenya na mshindi ni Gor Mahia tena kwa kumfunga Simba ya Tanzania mabao mawili kwa bila na hivyo atakwenda Uingereza kucheza na Everton huko Uingereza.

Hali hii ya mshindi kupata fursa ya kucheza na Everton iwe hapa Afrika Mashariki au huko Uingereza, kunaongeza ari ya wachezaji kwani wanafahamu kwamba kupata nafasi ya kucheza na timu kama hiyo, ni fursa pekee ya kuonekana na vilabu vya madaraja tofauti Uingereza.

Kuwezesha timu kujipima viwango vyao. Mashindano hayo ya timu nane za nchi za Kenya na Tanzania yanasaidia vilabu na wachezaji wenyewe kujipima viwango walivyonavyo kwa kujilinganisha na timu au wachezaji wa timu nyingine. Pamoja na kujipima, wachezaji wanaweza kuitumia fursa hiyo kujifunza kutoka kwa wachezaji wa timu nyingine na hivyo kuboresha viwango vyao.

Wachezaji kuweza kupata timu ndani na nje ya ukanda wa Afrika Mashariki

Mashindano ya aina hii yanaweza kusaidia mchezaji binafsi kupata timu ya kuichezea ndani ya ukanda huu wa Afrika Mashariki au hata nje kutegemea na kiwango ambacho anakionyesha.

Hii ni faida kubwa kwa mchezaji binafsi na hata klabu yake kwa sababu klabu anayotoka pia italipwa. Ninaamini wachezaji waliyajua hayo ili kuhakikisha kwamba wanacheza kwa ufanisi na kuweza kupata timu za kuchezea.

Ninakumbuka Seleman Matola aliwahi kushiriki michuano inayofanana na hii kule Nairobi na akawavutia viongozi wa Super Sport ya Afrika Kusini na hatimaye kusajiliwa.

Wachezaji kupata mechi nyingi za kimashindano kwa mwaka

Pamoja na kwamba michuano hiyo ni ya mtoano ambapo timu ikipoteza mchezo inaondoka, kwa timu ambazo zilifika hatua ya fainali ninaamini zimepata mechi nne za kimataifa hivo wachezaji kuwa na utimamu mkubwa wa kimchezo na kwa mchezaji binafsi.

Ushauri kwa waandaaji wa mashindano haya ni kwamba waangalie namna ambayo wanaweza kuwabadilisha ili kundi la timu nne zicheze kwa mzunguko hivyo kuongeza idadi ya mechi na hivyo kuongeza msisimko.

SportPesa kuangalia uwezekano wa kuongeza timu wanazozidhamini.

Kwa kuangalia matokeo mazuri ya timu ambazo walizidhamini kwenye ligi za nchi husika, nashauri pia kwamba waangalie uwezekano wa kudhamini timu zaidi, mathalani sita kila nchi ili kuzisaidia timu hizo kushiriki vizuri ligi ya nchi zao na kuongeza msisimko wa mashindano yanayojumuisha timuzote zinazo fadhiliwa.