Hospitali za rufaa zijengewe uwezo

Muktasari:

  • Hospitali hiyo imesema wataalamu kwa ajili ya shughuli hiyo wapo na vifaa yaani mashine za kisasa kabisa kwa ajili ya upandikizaji figo nazo zinapatikana kwa ajili ya kuwahudumia wagonjwa kwa ufanisi.

        Mwishoni mwa wiki iliyopita Hospitali ya Benjamin Mkapa iliyopo katika Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) ilitoa habari njema za maendeleo ya teknolojia ya tiba kwamba kuanzia Machi mwaka huu itaanza kupandikiza figo.

Hospitali hiyo imesema wataalamu kwa ajili ya shughuli hiyo wapo na vifaa yaani mashine za kisasa kabisa kwa ajili ya upandikizaji figo nazo zinapatikana kwa ajili ya kuwahudumia wagonjwa kwa ufanisi.

Halafu uongozi umesema, ingawa upandikizaji wa figo katika hospitali hiyo utafanyika kwa mara ya kwanza, wamejipanga kuhakikisha unafanyika kwa mafanikio makubwa na kuandika historia kuwa hospitali ya pili baada ya Muhimbili.

Tunafahamu kwamba Hospitali ya Mkapa haitakuwa ya kwanza kupandikiza figo nchini bali kinachofurahisha katika hili ni kuwa sasa tiba ya magonjwa ambayo madaktari wake ama walikuwa wanapatikana nje ya nchi au Muhimbili tu sasa imeanza kusogezwa mikoani.

Kwa miaka mingi, kumekuwa na hospitali zinazoitwa za rufaa kama vile KCMC ya Moshi, Bugando ya Mwanza na Mbeya Rufaa ya jijini Mbeya lakini bado hazikuwa na uwezo wa kutibu baadhi ya magonjwa hadi wagonjwa wapelekwe Muhimbili.

Mathalani japokuwa mikoani na hospitali za rufaa zina vitendo vya kuhudumia wenye matatizo ya mifupa lakini kitengo cha Tiba ya Mifupa Muhimbili (Moi) ndicho cha uhakika.

Aidha tiba ya ugonjwa kama wa kansa kwa miaka mingi imekuwa ikilazimu wagonjwa kupelekwa Ocean Road pekee; magonjwa yanayohusiana na moyo wagonjwa wamekuwa wakipelekwa India hadi hivi karibuni ilipoanzishwa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) Muhimbili, na hivi karibuni Muhimbili imejengewa uwezo wa kuhudumia wenye matatizo ya usikivu.

Katika tiba ya moyo utaalamu umefikia hatua ya kuwawekea vifaa vya kusaidia mapigo ya moyo kwa watoto wengi ambao bila ya taasisi hiyo ama wangepoteza uhai au wangeigharimu Serikali mamilioni ya shilingi kuwapeleka nje ya nchi. Mafanikio haya hakika yanastahili pongezi maana ni juhudi za kuondokana na utegemezi.

Tunapongeza zaidi kwa sababu mara nyingi, kila Serikali inaposema inaboresha huduma zake huwa ni kuongeza uwezo wa Muhimbili na mara chache zinazoitwa hospitali za rufaa. Lakini sasa Serikali imevunja mwiko huo imepeleka huduma hii muhimu na ghali kwa Hospitali ya Mkapa tena katikati ya nchi. Upandikizaji wa figo ni teknolojia ngeni ndiyo maana katika Hospitali ya Mkapa utafanywa na madaktari wa Tanzania kwa kushirikiana na wenzao kutoka Japan kwa kuwa wameanza siku nyingi.

Ushirikiano huu ni wa kawaida katika siku za mwanzo na kutokana na ukweli kuwa kumsomesha daktari hadi afikie kubobea katika fani yoyote kama hizo za figo na moyo ni gharama na inachukua muda, lakini mkazo uwe kupata wa kwetu kwani hiyo ndiyo njia pekee ambayo itawezesha nchi kupata madaktari wake tena wa kutosha.

Vilevile, Hospitali ya Mkapa imesema kwa kuanzia ina wagonjwa wawili watakaopandikizwa figo na kwamba gharama zao zitalipwa na chuo na hospitali kwa sababu mpaka sasa gharama halisi ya kufanya upandikizaji haijapangwa.

Tunatoa rai, wakati utakapofika, wizara ya afya ipange gharama nafuu ili watu wengi wenye uhitaji waweze kumudu na kuokoa maisha yao.

Wenye uwezo wanaweza kuendelea kutafuta tiba mahali popote duniani lakini Watanzania wengi hawana uwezo mkubwa kifedha hivyo wafikiriwe, na ikiwezekana Serikali ibebe sehemu kubwa ya gharama.