Hospitali za umma zidhibiti madaktari feki

Muktasari:

  • Habari hiyo inaelezea jinsi walinzi wa Hospitali ya Muhimbili walivyomfuatilia kijana mmoja waliyekuwa na wasiwasi naye na baadaye kubaini kuwa alikuwa akijitambulisha kwa wagonjwa kama daktari, ingawa haikusema huwa anafanyaje kazi hospitalini hapo.

Katika ukurasa wa sita wa toleo letu la juzi, kulikuwa na taarifa iliyokuwa na kichwa cha habari kisemacho “daktari feki mwingine anaswa Hospitali ya Taifa Muhimbili”.

Habari hiyo inaelezea jinsi walinzi wa Hospitali ya Muhimbili walivyomfuatilia kijana mmoja waliyekuwa na wasiwasi naye na baadaye kubaini kuwa alikuwa akijitambulisha kwa wagonjwa kama daktari, ingawa haikusema huwa anafanyaje kazi hospitalini hapo.

Picha zinamuonyesha kijana huyo akiwa na pingu mikononi huku shingoni akiwa amevalia kipimo cha mapigo ya moyo ambacho kimekuwa kikitumika kama nembo ya madaktari katika michoro, maigizo na vielelezo vingine. Tukio hilo ni moja ya matukio mengi ya kukamatwa kwa watu wanaojifanya kuwa ni madaktari katika majengo ya hospitali, hasa za Serikali. Watu kama hao wameshawahi kukamatwa hospitali za Morogoro, Geita, Mbeya, Mwanza, Muhimbili na sehemu nyingine. Hayo machache ni baadhi ya matukio mengi ambayo yamejulikana kutokana na kuripotiwa na vyombo vya habari au baada ya mtuhumiwa kunaswa na askari.

Hii inatia wasiwasi kuhusu udhibiti wa watu wanaoingia katika hospitali za umma, hasa kwenye vyumba vya madaktari na sehemu nyingine za kufanyia kazi wauguzi. Pia, inatia wasiwasi kuhusu usalama wa huduma wanazopata wagonjwa.

Katika tukio moja, mtu ambaye hakuwahi si tu kusomea udaktari, bali hata kupata elimu ya sekondari, alifanya kazi ya kutibu wagonjwa kwa muda mrefu bila ya kugundulika, ikiwa ni pamoja na kuchoma wagonjwa sindano.

Haieleweki mtu huyo aliwezaje kumudu kufanya kazi hospitali hiyo ya Taifa kwa muda mrefu bila ya kugundulika wakati kuna idara kama ya utawala, ambayo moja ya majukumu yake ni ulinzi na usalama, pamoja na idara ya rasilimali watu inayohusika na ajira na masilahi ya wafanyakazi. Haieleweki mtu kama huyo anawezaje kujipenyeza hospitalini hadi chumba cha sindano na kufanya kazi kwa muda mrefu bila ya idara hizo mbili kuhisi kuwa kuna mtu ambaye hafahamiki anayefanya kazi za kitabibu.

Maana yake ni kwamba alikuwa anapangwa zamu hata bila ya mpangaji kujua kama huyo ni muajiriwa halali kwa kuwa kama angekuwa hapangwi siku moja angegongana na mtu mwenye zamu eneo hilo.

Ingekuwa mtu huyo kajipenyeza hospitalini kwa siku moja na kutoweka, ingeweza kueleweka lakini ukweli kwamba amefanya kazi kwa muda mrefu bila ya kutambulika ndio unaozua maswali mengi, hasa kuhusu mifumo ya udhibiti wa watu katika taasisi hizo nyeti kwa afya ya binadamu.

Kama wafanyakazi wa hospitali hizo za Serikali wanaweza kudhibiti ndugu wasione wagonjwa wao hadi muda uliopangwa unapofika, inakuwaje wasiwe na uwezo wa kudhibiti mtu kuingia vyumba vya watoa huduma kama madaktari na matabibu wengine.

Ni lazima idara zinazosadia utabibu katika hospitali za umma zitekeleze majukumu yao ipasavyo ili kuwawezesha madaktari na wauguzi wengine kufanya kazi zao vizuri na pia kuwawezesha wagonjwa kupata huduma bora inayotolewa na watu wenye taaluma na wanaotambulika.

Uongozi wa hospitali za umma hauna budi kubuni mbinu bora za kudhibiti maeneo muhimu ili wale wanaoingia vyumba vya madaktari au vya uuguzi, wawe ni wale wanaotambulika ili kuepusha uwezekano wa wananchi kupewa tiba zisizostahili kutoka kwa watu wasiostahili.

Hadi sasa wale waliomudu kuingia sehemu hizo za madaktari na matabibu na kufanikiwa kutoa huduma kwa muda mrefu bila ya kujulikana ni wale ambao walitaka kutumia maeneo hayo kwa ajili ya kujipatia fedha. Lakini watu wenye nia ovu wakifanikiwa kuingia maeneo kama hayo wanaweza kuwa na hatari kubwa zaidi. Ni matumaini yetu kuwa habari ya kijana aliyekamatwa juzi Hospitali ya Taifa Muhimbili, itawakumbusha wahusika wa maeneo hayo kubuni mbinu za udhibiti ili watu kama hao wasiweze kujipenyeza katika hospitali za umma na kutoa huduma kama madaktari.