Huu ndiyo muda wa kugeukia miamala ya fedha kielektroniki

Muktasari:

Lakini kwa wenzetu huko duniani, ni vigumu kuwakuta wakibeba fedha nyingi taslimu kwa lengo la kwenda kufanya ununuzi au kupata huduma fulani inayohitaji malipo.

Katika shughuli za uuzaji na ununuaji hapa nchini, ni kawaida kuwakuta wanunuzi wa bidhaa na huduma zote zinazohitaji malipo, hulipa kwa fedha taslimu au hundi. Ndiyo njia iliyozoeleka zaidi.

Lakini kwa wenzetu huko duniani, ni vigumu kuwakuta wakibeba fedha nyingi taslimu kwa lengo la kwenda kufanya ununuzi au kupata huduma fulani inayohitaji malipo.

Wengi wao hupendelea zaidi kufanya miamala ya fedha kielektroniki kutokana na muundo wake ambao ni rahisi na ni salama zaidi.

Ripoti ya wageni wanaotembelea nchini ya mwaka 2016 iliyotolewa na Wizara ya Maliasili na Utalii Oktoba mwaka jana, inaonyesha matumizi ya fedha taslimu kwa watalii katika malipo yanaongezeka. Yaliongezeka kutoka asilimia 81.2 mwaka 2015 hadi kufikia asilimia 83.9 mwaka 2016. Katika ripoti hiyo watalii wanawalalamikia watoa huduma wengi wa hapa nchini hawataki kuwakubalia kufanya malipo kwa njia ya kielektroniki.

Kwa muskabali huo, kama watalii wataendelea kunung’unikia jambo hilo, kuna hatari ya kuanza kuwapoteza, kwa sababu wengi wao hawajazoea kutembea na fedha nyingi mifukoni, wameshazoea kufanya miamala mingi ya fedha kielektroniki hata kama atanunu peremende.

Lakini wengine hupendelea zaidi kufanya miamala hiyo kwa lengo la kutunza kumbukumbu za matumizi yake ili ahakikishe bajeti yake aliyojipangia haivurugiki.

Jambo la malipo ya kielektroniki sio la nchi zilizoendelea pekee, bali hata kwetu mifumo hiyo ipo kwenye mabenki tunayohifadhi fedha zetu na hata katika mitandao ya simu kupitia huduma zao za kifedha. Ni utashi tu umekosekana.

Ifike wakati sasa kwa Serikali kuanza kuhimiza matumizi ya fedha kielektroniki badala ya kung’ang’ania mfumo uliopitwa na wakati. Kwani kufanya hivyo kutasaidia kupunguza kiwango kikubwa cha matumizi ya fedha taslimu katika shughuli zetu kutokana na huduma za malipo ya kielektroniki zitaendelea kuboreshwa kila siku.

Ripoti ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) ya hivi karibu inaonyesha Watanzania waliojiunga na huduma za miamala ya fedha ya simu wapo zaidi ya milioni 20, lakini pia mwaka 2012 idadi ya Watanzania waliokuwa wakitumia huduma za kibenki walikuwa asilimia 12.

Nashindwa kuelewa kwa nini? Watanzania tunakumbatia mfumo huu wa malipo ambao unapitwa na wakati na kugharimu fedha nyingi huku tukiuacha ule wenye unafuu na wepesi katika ufanisi.

Ni muhimu kufahamu kuwa matumizi ya fedha tasilimu yanaongeza gharama za kuweka na kutoa na kuhifadhi na hauna uwiano halisi wa viwango vya kubadilishia fedha za kigeni.

Watoa huduma za kifedha wajitahidi kuendana na mabadiliko haya mapya ya namna ya kufanya miamala kwa wepesi na usalama zaidi. Waendelee kuanzisha huduma za kufanya malipo kwa njia ya mtandao, kuhifadhi na kuhamisha fedha wengine hata mikopo.

Kila siku tunashuhudia ubunifu mpya katika miamala ya simu na benki kupitia vifaa vya kielektroniki ambavyo watu wengi wanavimiliki sasa.

Baadhi ya sehemu za huduma na maduka ya bidhaa wameanza kuuelewa utaratibu huu ndiyo maana unakuta wameweka chaguo tofauti la namna ya kufanya malipo yako iwe kwa kadi, simu au tasilimu.

Mara nyingi sehemu hizo ni zile ambazo watu kutoka nje ya nchi huzitembelea zaidi. Maeneo hayo ni kama yale ya maduka makubwa, hoteli na migahawa mikubwa ambayo hutumiwa zaidi na wageni, lakini kwa maeneo yanayotumiwa zaidi na Watanzania kama sokoni na maeneo mengine kama hayo bado hayajashtuka.

Lakini kama wataanza kutumia mfumo huo, utawasaidia wanunuzi na hata wao watapata fursa ya kuweka taarifa na mtiririko sahihi zaidi wa mapato na matumizi kwenye huduma zao.

0756939401