Sunday, September 10, 2017

IGP Sirro hakustahili kutoa kauli hii

 

Katika kukabiliana na uhalifu na matukio mengine yanayotishia usalama wa wananchi, ni muhimu kwa wananchi wenyewe kwanza kuwa mstari wa mbele kushirikiana na Jeshi la Polisi.

Hii ni pamoja na kutoa taarifa kwa jeshi hilo kuhusu mienendo yoyote ya watu wanaodhani kuwa si wema na wana lengo baya dhidi ya jamii au watu fulani.

Na hata mwananchi ambaye anadhani kuwa maisha yake yako hatarini kutokana na kuhisi mienendo ya watu fulani dhidi yake, anapaswa kutoa taarifa Jeshi la Polisi ili lichukue hatua za kumuepusha na hatari ya kushambuliwa na watu hao wabaya.

Lakini hilo haliondoi jukumu la Jeshi la Polisi kuchukua hatua za kuepusha wananchi wake na matukio kama hayo pale ambapo halipewi taarifa za kuwepo hatari kama hizo. Jeshi la Polisi limepewa nyenzo zote muhimu za kuchunguza mienendo ya watu wanaowahisi kuwa ni hatari kwa jamii au kwa watu wachache.

Ndio maana Serikali inatumia kodi za wananchi kwa ajili ya kuhakikisha Jeshi la Polisi linasomesha, linaajiri na kuwapa nyenzo zote muhimu askari wa eneo la intelijensia ili waone mapema njama au mipango miovu ya kudhuru jamii au mtu mmoja mmoja iwe kwa kutaarifiwa na wananchi wenyewe au kwa kutumia mbinu za kiintelijinsia kuzibaini njama hizo.

Lakini kauli ya Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Simon Sirro alipokuwa akijibu swali la mwandishi mmoja mjini Dodoma kuhusu chombo hicho kutochukua hatua baada ya Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu kusema kuwa alikuwa anafuatiliwa na watu wenye nia mbaya, inakwenda kinyume na wajibu huo wa Jeshi la Polisi.

Kamanda Sirro alisema kuwa Jeshi la Polisi halikuweza kuchukua hatua baada ya Lissu kusema hayo hadharani kwa kuwa mbunge huyo wa Singida Mashariki hakuripoti kituo chochote cha polisi kuwa alikuwa anafuatiliwa na watu anaohisi ni waovu.

Cha ajabu, Jeshi la Polisi ndilo limekuwa likimsaka Lissu, kumkamata na kumfungulia mashtaka kwa tuhuma za kutoa maneno ya uchochezi kwenye mikutano hiyo hiyo ambayo pia aliitumia kueleza wasiwasi wa usalama wake.

Kama Jeshi la Polisi liliweza kumsikia Lissu akitoa kauli ambazo linahisi za kichochezi,linashindwaje kusikia kauli za mtu huyohuyo kuhusu wasiwasi wa kushambuliwa na watu wasiojulikana?

Kazi kuu za Jeshi la Polisi ni pamoja na kulinda wananchi na mali zao na ili lizifanye kwa ufanisi, Serikali inalipa kila utaalamu unaotakiwa ili libaini njama, vitendo vya uhalifu na kuweza kuzuia na pale linaposhindwa kuzuia, lidhibiti au kuwashughulikia wahusika.

Kama Jeshi la Polisi halikuweza kuchukulia kwa makini kauli ya Lissu ambaye ni mbunge, kuhusu wasiwasi wa usalama wake, vipi kuhusu wananchi wengine ambao hawana umaarufu wala heshima kama ya mbunge?

Suala la usalama wa wananchi ni nyeti kama lilivyo kwa viongozi. Kila mwananchi anastahili kulindwa maisha na mali zake.

Ni kweli kwamba mtu yeyote anayehisi yuko hatarini kushambuliwa anatakiwa atoe taarifa Jeshi la Polisi, lakini hata pale anaposhindwa kufanya hivyo na akatamka hadharani, jeshi hilo lina wajibu wa kuchukua hatua zilezile ambazo linaweza kuchukua kwa mtu aliyetoa taarifa.

Tayari suala la usalama wa wananchi limeshakuwa mjadala mkubwa ndani na nje ya Bunge, ambalo sasa limeagiza kamati yake ya ulinzi na usalama ikutane kuzungumzia suala hilo.

Maana yake ni kwamba suala la usalama wa wananchi si lelemama tena na linahitaji umakini mkubwa.

-->