UCHAMBUZI: Inakera mabasi kugeuka kuwa nyumba za ibada njiani

Ni jambo la kawaida kuwa abiria anapoingia kwenye chombo cha usafiri, hategemei bughudha katika safari yake; anatarajia kufika salama ndio maana anakuwa na uhuru wa kuchagua usafiri anaoutaka.

Mathalan kwenye usafiri wa mabasi ya umma ya kwenda mkoa mmoja hadi mwingine, mikoani au nchi jirani, abiria anachagua basi kutokana na kuridhishwa na huduma zinazotolewa.

Zipo huduma ambazo zimebainishwa kulingana na madaraja ya mabasi, lakini zipo ambazo hazijaandikwa kwenye utaratibu ambazo hutolewa kwenye safari.

Hata hivyo, kwa muda mrefu sasa kumeibuka wimbi la watu wanaoendesha ibada katika vyombo vya usafiri. Nitatolea mfano usafiri katika mikoa ya Nyanda za Juu Kusini.

Kwa waliobahatika kusafiri mikoa hiyo hususan kati ya Mbeya na Songwe hasa kati ya barabara ya Mbeya na Tunduma aghalabu wamekutana na ibada ndani ya basi na huenda si mara moja.

Katika safari hizo, wanaibuka watu wanaojitambulisha kama wachungaji, watumishi, manabii na kuanza kuendesha ibada.

Naziita ibada kwa sababu kwa wale wanaofahamu taratibu za ibada kanisani hazina tofauti na zinazoendeshwa kwenye magari maana kuna kipindi cha kufungua kwa sala, kusoma neno na kufuatiwa na mahubiri lakini mwishoni kuna kutoa sadaka.

Hatua hizo zinatokea kwenye safari na kila hatua hufuatiwa na nyimbo ambapo mchungaji anaanzisha nyimbo huku baadhi ya abiria wakiitikia.

Hoja yangu hapa sio kupinga ibada au mahubiri ila hoja yangu ni kuangazia huu utaratibu wa huduma ya ibada ndani ya mabasi, ambayo kwa maeneo ya Mbeya unaonekana kuwa kitu cha kawaida.

Pengine sio wote wanaokubaliana na utaratibu huu kwa kuwa ndani ya basi lenye zaidi ya abiria wengi kuna watu wa hulka, jamii na imani tofauti.

Siingilii uhuru wa mtu kiimani kwa kuwa kila mmoja ana imani yake, lakini naona utaratibu huu ukikiuka haki za abiria kwa kuwabughudhi na pengine kuwalazimisha baadhi kuabudu au kushiriki ibada pasipo hiari yao.

Wakati mahubiri yakiendelea, abiria ambaye hataki kusikiliza hawezi kufunga masikio lakini pia wakati huo abiria ameshalipa nauli hivyo inakuwa vigumu kushuka kutafuta usafiri mwingine.

Ikumbukwe kuwa suala la ibada ni hiari ndio maana yamejengwa maeneo maalumu kama makanisa na misikiti ambapo huko kila mmoja anaenda kwa hiari kulingana na kile anachoamini.

Siwezi kujua kama hii ni mbinu mpya ya kutafuta waumini au pengine mwingine anaweza kuwaza kwamba imekuwa biashara kwa kuwa wengi wanapomaliza kuhubiri wanaomba sadaka.

Kiuhalisia lazima kutambua kuwa kwenye safari kuna mchanganyiko wa jamii mbalimbali, kabila, itikadi na imani mbalimbali.

Ndio maana nawiwa kusema utaratibu huu si mzuri katika safari yenye mchanganyiko wa watu wa jamii tofauti

Lakini kibaya zaidi ni pale baadhi ya hao wajiitao wachungaji au watumishi wa Mungu wanapotumia mafumbo na lugha za kejeli dhidi ya abiria ambao hawahitaji kuwasikiliza.

Kwa mtu mwenye busara unabaki kujiuliza, hivi kuna ulazima wa kusikiliza mahubiri hayo? Je, huo ni utaratibu rasmi ambao sasa umo kwenye mabasi ya abiria?

Kwa kuzingatia taratibu za kumlinda mteja, sidhani kama yanayofanyika kwenye mabasi hayo, yanalinda haki za mteja hata kama wapo baadhi wanaofurahia.

Rai yangu kwa mamlaka zinazohusika na usafiri wa barabarani, kuangalia namna ambayo haiwezi kuwakwaza baadhi ya abiria ikizingatiwa mahubiri yana sehemu maalum.

Kama inakuwa vigumu kupiga marufuku kwa kuwa imekuwa mazoea, basi kwenye mabasi hayo kuwe na maelekezo ya ziada yakibainisha kuwa kwenye basi hilo kuna huduma ya ibada ili abiria aweze kufanya uchaguzi mwenyewe.

Nimezngumzia mikoa ya Nyanda za Juu Kusini kama mfano tu ikiwakilisha maeneo ambayo abiria wanapata bughudha kwenye safari ikiwa ni pamoja na biashara zinazofanywa kwenye mabasi.

Ninachojaribu kuonyesha ni kuwa ni lazima wateja waheshimiwe na huduma zitolewe kulingana na taratibu, ili kuepuka kuwakwaza hasa ikikumbukwa kuwa kazi ya mabasi ni kusafirisha abiria na si kutoa huduma za ibada.

Wadau wa usafiri wakiwamo abiria msifumbie macho yale yanayowakera na kuwabughudhi katika safari kwa kuwa mna haki ya kupata huduma ya usafiri iliyo bora.

Emmanuel Mtengwa ni mwandishi wa kampuni ya Mwananchi

0753-590823