Inawezekana kuepuka majanga ya moto

Muktasari:

  • Janga hilo ambalo imedaiwa kusababishwa na hitilafu ya umeme, limetokea siku mbili tu tangu bweni la Sekondari ya Wasichana Korogwe nalo kuteketea kwa moto.

Alfajiri ya Jumanne iliyopita, moto uliteketeza soko lote la Mbagala Rangitatu lililokuwa na vibanda vya wafanyabiashara 673.

Janga hilo ambalo imedaiwa kusababishwa na hitilafu ya umeme, limetokea siku mbili tu tangu bweni la Sekondari ya Wasichana Korogwe nalo kuteketea kwa moto.

Jambo la kumshukuru Mungu ni kwamba hakuna madhara kwa watu yaliyotokana na maafa hayo, lakini mali na pengine fedha – vitu vilivyotafutwa kwa jasho jingi na muda mrefu – viliteketea kwa dakika chake.

Pamoja na msemo wa Waswahili kwamba ajali haina kinga, tunaamini kwamba majanga ya aina hii ambayo aghalabu husababisha uharibifu mkubwa wa mali au hata kugharimu maisha ya watu yanaweza kuzuilika kwa kiwango kikubwa ikiwa hatua za tahadhari zitachukuliwa.

Lakini tatizo tunaloliona ni elimu duni au uelewa mdogo juu ya namna ya kujikinga na majanga ya moto ambayo tunaamini kwamba Jeshi la Zimamoto na Uokoaji likijipanga na kuweka mikakati, balaa hili linaweza kudhibitiwa kwa kiwango kikubwa.

Katika matukio hayo mawili; ya Mbagala na Korogwe, imedaiwa kwamba chanzo chake ni hitilafu ya umeme na sababu hii huenda ikawa mojawapo kati ya zinazoongoza kwa kusababisha ajali za moto.

Tunatarajia kwamba kutokana na matukio ya aina hiyo kuwa mengi, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji na Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) wangekuja na mikakati ya mafunzo kwa wananchi hasa wale wanaofanya shughuli zao kwenye mikusanyiko mikubwa juu ya matumizi bora ya mfumo na salama wa umeme ili kuokoa maisha na mali zao pindi tatizo kama hilo linapojitokeza.

Watu hawa wanahitaji kuelimishwa kuhusu matumizi sahihi ya vifaa vya umeme kwenye nyumba na maeneo yao ya biashara. Majanga mengine yamekuwa yakisababishwa na ujuvi wa masuala ya umeme na kufikia hata kuhamisha nyaya bila kuzingatia weledi na vifaa stahiki.

Matumizi sahihi pia ya umeme ni tatizo kwa baadhi yetu hasa katika maeneo ya biashara, si ajabu kukuta soketi moja au mbili zikiwa na matumizi makubwa kushinda uwezo wake na kuzifanya kuzidiwa.

Pia wakati mwingine moto unatokana na hitilafu ya umeme husambaa na kusababisha madhara makubwa kutokana na kuhamaki au kutojua kwamba unapotilia shaka au inapotokea moto wa aina yoyote katika nyumba, jambo la kwanza ni kukimbia kwenye swichi kuu (main switch) na kuizima.

Tunaamini kabisa kwamba elimu ya majanga ikiyafikia makundi makubwa ya watu kama wafanyabiashara katika masoko, wanafunzi, viwandani na taasisi zenye mikusanyiko mikubwa ya watu, siyo tu itazuia majanga hayo katika maeneo hayo, bali itasambaa kwani watakaoelimishwa nao watafanya hivyo katika nyumba zao na watawaelimisha ndugu jamaa na marafiki.

Tumezungumzia majanga ya moto yanayosababishwa na hitilafu ya umeme na jinsi ya kuyaepuka kama mfano tu lakini yapo mengi.

Hivyo, ni jukumu la kila mmoja wetu kujisaili kama mahali anapofanyia kazi au anapoishi ni salama na amechukua kila aina ya tahadhari ya majanga hasa ya moto. Pamoja na hayo, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji wakiamua, wakawezeshwa, miaka ijayo tutashuhudia takwimu za mabalaa haya zikishuka.