Inawezekana vipi Umitashumta bila huduma ya kwanza?

Muktasari:

  • Lengo kubwa la kufanyika kwa michezo hiyo ni kuhakikisha Tanzania inakuwa na wanamichezo wake ambao wanapatikana katika misingi inayoeleweka. Kuwasaka wanamichezo wenye vipaji kutoka mitaani huwa na ugumu wake, lakini mfumo huu kupitia michezo ya Umitashumta na Umisseta, ni mzuri.

Michezo ya Shule za Msingi Tanzania (Umitashumta) inaendelea kwenye Chuo cha Ualimu, Butimba mkoani Mwanza ikiwa ni siku chache baada ya kumalizika kwa michezo ya sekondari ya Umisseta.

Lengo kubwa la kufanyika kwa michezo hiyo ni kuhakikisha Tanzania inakuwa na wanamichezo wake ambao wanapatikana katika misingi inayoeleweka. Kuwasaka wanamichezo wenye vipaji kutoka mitaani huwa na ugumu wake, lakini mfumo huu kupitia michezo ya Umitashumta na Umisseta, ni mzuri.

Wanamichezo huibuliwa na kuendelezwa, kung’ara na baadaye hupotea, na vipaji kila siku vinazaliwa, vinatengenezwa na kuendelezwa.

Tunapongeza mpango huu, lakini tumesikitishwa na waandaaji wa michezo hii, yaani tunaweza kusema Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Tamisemi kwa kushindwa kuwapatia magari ya huduma ya kwanza.

Tunajiuliza, inawezekana vipi Tamisemi kuandaa michezo tena inayoshirikisha wanafunzi na wasimamizi ao wapatao 2,500 katika eneo moja halafu kunakuwa hakuna gari la uhakika la huduma ya kwanza?

Ni ngumu kupata jibu lakini tunaweza kusema hii ni hatari. Kwa idadi hiyo ya wanamichezo mengi yanaweza kutokea. Si kusubiri wanaoumia michezoni pekee, bali wanaoweza kuumwa ghafla au matatizo mengine ya ghafla ya kiafya.

Ni kawaida kusikia mamlaka zinaunda kamati kuchunguza tukio fulani baya linaloweza kutokea kutokana na kutokuwa na huduma hiyo ya kwanza. Si vizuri kuanza kuunda kamati kuchunguza tukio linaloweza kuzuilika kwa kuhakikisha kunakuwa na huduma za uhakika za afya.

Kukosekana kwa magari ya uhakika ya kubebea wagonjwa kumesababisha kuanza kutumika magari ya kawaida kuwapeleka majeruhi hospitali, tofauti na ilivyokuwa kwenye Umisseta.

Mwenyekiti wa michezo hiyo, Jeshi Lupembe alikiri kuwepo kwa upungufu huo na kusema kuwa tatizo kubwa ni kukosa udhamini.

Alisema kuwa mashindano hayo yana gari moja la kubebea wagongwa, hivyo likiwa halipo huamua kutumia magari ya kawaida ili kuhakikisha majeruhi wanapata huduma. Tunachofahamu ni kwamba gari la huduma ya kwanza lina kila kitu, tofauti na magari ya mabosi hao wa elimu.

Hoja ya kukosa udhamini haina mashiko kwa sababu mashindano hayo ni ya kiserikali na kabla ya kufanyika kulikuwa na kamati ya maandalizi iliyopanga kila kitu.

Kamati hiyo ndiyo ilitakiwa ione kuwa huduma ya kwanza ni kipaumbele cha mashindano na hivyo vitu kama gari la wagonjwa vilitakiwa kuwa vya uhakika katika mkusanyiko kama huo.

Wito wetu ni kwa waandaaji na waendeshaji wa mashindano hayo kuacha majibu mepesi kuwa hakuna ufadhili wa kuwawezesha kuwa na gari la uhakika, badala yake watafute mbinu za kuhakikisha kunakuwepo na huduma ya uhakika ili kutoweka hatarini maisha ya wanafunzi wetu.

Kuendesha mashindano bila ya huduma za uhakika za afya ni kuweka rehani afya na maisha ya watoto wetu.

Pamoja na kuhakikisha gari linapatikana, waandaaji wahakikishe mashindano yajayo hayafanyiki bila ya huduma muhimu na za uhakika za afya kuwepo.