Itambue njaa iliyojificha na madhara yake kwa Watanzania

Muktasari:

  • Taarifa iliyotolewa na Taasisi ya Chakula na Lishe (TFNC) inaonyesha Serikali hupoteza Sh800 sawa na asilimia 2.7 ya pato la Taifa (GDP) kwa mwaka, kwa sababu ya madhara ya upungufu wa virutubisho vya chakula vya chuma, vitamin A na tindikali ya foliki.

Japo Tanzania inajitosheleza kwa chakula kutokana na mavuno ya kilimo kila mwaka, bado Watanzania wanakabiliwa na njaa iliyojificha ya mlo kamili.

Taarifa iliyotolewa na Taasisi ya Chakula na Lishe (TFNC) inaonyesha Serikali hupoteza Sh800 sawa na asilimia 2.7 ya pato la Taifa (GDP) kwa mwaka, kwa sababu ya madhara ya upungufu wa virutubisho vya chakula vya chuma, vitamin A na tindikali ya foliki.

Mtaalamu wa Chakula na Lishe wa TFNC, Celestin Mgoba anasema mbali na fedha hizo, madhara mengine ni kupungua kwa nguvu kazi, watoto kushindwa kuelewa masomo darasani na kuongeza mzigo kwa Wizara ya Afya. “Mtu anahesabiwa ameshiba kama atapata mlo kamili wenye mchanganyiko wa vyakula vya wanga, protini, mafuta, vitamin na madini kila siku,” anasema Magoba na kuongeza:

“Kupata mlo kamili kunapunguza uwezekano wa mtu kuingia katika hatari ya kupata maradhi ya moyo, kisukari, mifupa na aina fulani za saratani.”

Akieleza maana ya utapiamlo, Magoba anasema ni upungufu wa virutubisho au ongezeko lake (kitambi).

“Upungufu wa virutubisho vya msingi ni njaa iliyojificha ambayo ni ukosefu wa madini na vitamin kwenye chakula. Madhara yake ni watoto kushindwa kukua, kukosa kinga ya mwili na afya kwa ujumla kwa watoto na kina mama walio katika umri wa kuzaa,” anasema Mgoba.

“Upungufu wa madini ya chuma husababisha watoto zaidi ya bilioni mbili duniani kupata mtindio wa ubongo na asilimia 25 ya vifo vya watoto kwa nchi zinazoendelea. Ukosefu wa madini ya iodine pia husababisha madhara kwenye ubongo wa mtoto,” anaongeza.

Mbali na madini, anasema ukosefu wa vitamin A huathiri asilimia 33 ya watoto na asilimia 37 nchini ikiwa ni pamoja na kupata upofu na vifo.

“Ukosefu wa folate (tindikali ya foliki na vitamin B9), husababisha vifo kwa watoto walio chini ya umri wa miaka mitano. Ukosefu wa zinki hupunguza kinga ya mwili na kuongeza uwezekano wa maradhi ya kuhara hasa kwa watoto.

Anataja virutuibisho muhimu ni pamoja na zinc, folate, Niacin (B3), Cobalamin (B12), Thiamine (B1), Ribofalvin (B2), Pyrodoxine (B6) na Selenium akisema japo vinahitajika kwa kiwango kidogo (micro or milligrams) kwa siku, umuhimu wake ni mkubwa ikiwa ni pamoja na metabolizim, ukuaji na afya.

“Zinahitajika miligramu 18 za chuma, miligramu 11 za zinki na gramu 0.15 za iodine kwa siku. Kwa mujibu wa Shirika la Afya Ulimwenguni, upungufu wa damu mwilini (anaemia) unasababishwa na upungufu wa madini ya chuma, ni tatizo sugu ambalo asilimia 40 ya watu duniani wanalo na kwa watoto ni asilimia 58.”

Hata hivyo, anasema kwa madini ya iodine wenye madhara ni asilimia 5 kwa kuwa upatikanaji wa chumvi yenye madini hayo ni kwa asilimia 90.

“Kwa Tanzania, asilimia 7 ya watu wana ugonjwa wa goita na wanaotumia chumvi yenye iodine ni asilimia 61,” anasema Mgoba.

Sababu za kukosa virutubisho

Akielezea sababu ya watu kukosa virutubisho licha ya kula na kushiba, Magoba anasema watu wengi wanakula vyakula visivyo na lishe ya kutosha kwa mfano nafaka, mbegu (legumes), mizizi ambayo kimsingi haina vitamin A, zink, chuma wala iodine.

“Wengi hawali vyakula vyenye virutubisho vya kutosha kama nyama, samaki, kuku, mayai, maziwa, matunda na mbogamboga. Hata ulaji wa vyakula vya mafuta ni mdogo. Mafuta husaidia ufyonzaji wa virutubisho mwilini,” anasema.

Anasema kutokana na ukosefu wa virutubisho hivyo, asilimia 34 ya watoto wa Tanzania hudumaa na asilimia 14 huwa na uzito mdogo.

“Kukosekana kwa Vitamin na madini mwilini hakusababishi njaa inayoonekana, bali isiyoonekana na matokeo yake watoto hubakiwa wakiwa na uzito mdogo, upungufu wa kinga, vipofu, kushindwa kuelewa masomo na maradhi ya akili,” anasema na kuongeza:

“Asilimia 17 ya watu wazima hushindwa kufanya kazi za uzalishaji kutokana na lishe duni.”

Anataja madhara mengine ni pamoja na kuathirika kwa mfumo wa neva za fahamu, matatizo ya uzazi, mfumo wa akili na utendaji kazi, ukuaji hafifu na mwisho kuwa mbilikimo, goita, matatizo ya kusikia na kuwa bubu.

Akieleza mbinu za kupambana na upungufu wa virutubisho, Mgoba anasema ni pamoja na kuongeza virutubisho (supplementation) na uimarishaji wa virutubisho (food fortification) na kuongeza virutubisho kwa njia za kilimo (crop biofortification).

Pia kuwapo kwa elimu ya lishe kwa jamii na kuongeza uzalishaji wa kilimo.

Kwa upande wake, Mratibu mwandimizi wa mradi wa kuongeza virutubisho katika mfuko wa chakula (BNFB) Tanzania, Dk Richard Kasuga anasema tatizo la lishe ni sugu nchini, huku pia akitaja mikoa iliyoathirika zaidi.

“Mikoa yenye upungufu mkubwa kwa vitamin A ni Pemba Kaskazini asilimia 51, Kagera asilimia 47, Pwani asilimia 45, Manyara asilimia 44, Kigoma asilimia 39, Shinyanga asilimia 37 na Mtwara asilimia 36,” anasema Dk kasuga.

Anasema ili kuonyesha kuwa hiyo ni njaa iliyojificha, mikoa inayotajwa kwa uzalishaji mkubwa wa chakula nchini ndiyo inayoongoza kwa watoto wanaodumaa wakiwa chini ya miaka mitano.

Mikoa hiyo ni Rukwa asilimia 56, Ruvuma asilimia 44, Iringa asilimia 42, Kagera asilimia 42 na Geita asilimia 41.

Mikoa mingine ni Katavi, Mwanza na Tanga asilimia 39, Kigoma, Mbeya na Mtwara asilimia 38, Dodoma asilimia 37, Arusha na Manyara asilimia 36, Lindi asilimia 35 na Morogoro asilimia 33.

Mikoa yenye nafuu ni Pwani asilimia 30, Mara, Kilimanjaro na Singida asilimia 29, Tabora na Shinyanga asilimia 28 na Dar es Salaam asilimia 15.

“Lengo letu ni kuhakikisha tunapunguza njaa isiyoonekana kwa watoto, kuonyesha jinsi ya kuongeza virutubisho kwenye mazao na kuimarisha nguvu za wadau na uwekezaji katika chakula,” anasema Dk Kasuga.