Friday, November 4, 2016

JPM ameonyesha nia kutimiza ahadi

 

By AbdulrahmanKinana

Tangu aapishwe kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwaka mmoja  uliopita, Dk John Pombe Magufuli amefanikiwa kutekeleza ahadi kadhaa alizotoa wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu.

Moja ya hatua alizochukua tangu awe Rais ambazo zinasifika ni vita dhidi ya rushwa, ambayo imekuwa chukizo kote nchini.

Wakati akizindua Bunge la Kumi na Moja mjini Dodoma, siku chache baada ya kuapishwa kuwa Rais wa Tano wa Tanzania, Dk Magufuli alitangaza mikakati ya kupambana na rushwa, kupunguza matumizi yasiyo ya lazima na kuboresha huduma kwa jamii.

Ingawa ni mapema sana kupitisha hukumu kuhusu utekelezaji wa ahadi zake zote zilizomo kwenye ilani ya CCM, hakuna shaka kuwa amefanikiwa kutimiza  ahadi zake na kutimiza majukumu ya ofisi yake.

Hivi sasa ndio kwanza tumefikia robo ya mwaka wa bajeti ya utawala wa sasa, lakini Dk Magufuli ameonyesha utayari na nia ya kutekeleza ahadi zake kwenye kampeni na hivyo anastahili kuungwa mkono na Watanzania wenye nia njema.

Kitu kimoja kizuri kuhusu Rais ni kwamba ni mkweli wa dhati. Tofauti na wanasiasa wengi ambao hawamaanishi wanachokisema, Dk Magufuli amethibitisha kuwa ni mtu mkweli na anatekeleza anachokisema.

Ni kwa sababu hii amefanikiwa kurejesha uwajibikaji na nidhamu ya fedha serikalini. Mwaka mmoja katika kipindi chake cha miaka mitano, Rais Magufuli ameonyesha dhamira ya Serikali yake kuleta mabadiliko kwa wananchi wa Tanzania ambao wamekuwa wakiyataka ili kuijenga upya nchi iliyo na utajiri wa maliasili.

Kwa sasa, kazi inaendelea kujenga upya uchumi wa nchi, kurejesha huduma bora, kukarabati zaidi miundombinu na kuboresha mazingira na jamii.

Ikiwa ni matokeo ya nidhamu ya fedha ambayo imeonyeshwa na utawala wa Dk Magufuli katika kipindi cha mwaka mmoja, Shirika la Kimataifa la Fedha (IMF) limeiruhusu Serikali yake kukopa fedha bila ya masharti na yenye masharti nafuu.

Hii inamaanisha, IMF ina imani na usimamizi wa fedha na uchumi unaofanywa na Serikali.

Mkakati wa kuongeza ufanisi wa Rais pia umelenga katika makusanyo ya kodi ili kuongeza mapato ya ndani. Kuna ongezeko la wazi katika makusanyo ya mapato kutoka Sh1 trilioni wakati alipoingia madarakani hadi Sh1.5 trilioni kwa kipindi cha mwaka mmoja tu.

Rais amekuwa akitoa matamko makali dhidi ya wakwepaji kodi na mara kadhaa amesisitiza wateja kudai risiti baada ya kununua bidhaa, utamaduni ambao haukuwepo kabla.

Kutimiza ahadi yake katika nidhamu ya fedha, Rais ametangaza hatua kadhaa za kubana matumizi, ikiwa ni pamoja na safari zisizo na umuhimu nje ya nchi na semina. Pia alichukua hatua ya kufuta baadhi ya sherehe za kitaifa na kuagiza fedha zilizokuwa zimetengwa kwa shughuli hizo ziende kwenye miradi ya maendeleo.

Mkakati wa Dk Magufuli kupambana na rushwa na ubadhirifu umezima wapinzani ambao muda mfupi uliopita walikuwa wakinyanyua bango la kupinga rushwa, wakiituhumu CCM kukumbatia viashiria vya rushwa. Maoni ya wachambuzi wengi ni kwamba vita dhidi ya rushwa itakuwa ni kumbukumbu kubwa ya utawala wa Rais Magufuli.

Kuhusu ahadi ya kutoa elimu bora, wakati akiingia madarakani, Rais alitangaza utekelezaji wa sera ya elimu bure kwa watoto wanaoandikishwa elimu ya msingi na elimu ya sekondari.

Lengo la juhudi hizo za Serikali ni kuona watoto kutoka familia za watu wa kipato cha chini wanakwenda shule na kupata elimu. Ongezeko kubwa katika kuandikisha watoto shule katika mwaka wa kwanza wa utekelezaji wa sera ya elimu bure, linamaanisha kuwa awali wengi walikuwa hawawezi kwenda shule kutokana na matatizo ya kifedha ya wazazi wao.

Hali kadhalika katika upungufu wa madawati shuleni ambao ulikuwa ukionekana kuwa tatizo sugu. Rais mwenyewe aliongoza kampeni ya kuhakikisha madawati yanapatikana kote nchini. 

Rais Magufuli hapingani na wakosoaji wanaosema kuwa mwaka wake wa kwanza umeshuhudia fedha zikipotea kutoka kwenye mzunguko. Lakini amekuwa akisema kuwa hilo linaweza kuwa ni matokeo ya Serikali yake kuondoa mipango michafu ya kujipatia fedha na matumizi mabaya.

Sababu nyingine ni juhudi za Serikali kulipa madeni makubwa ya ndani na nje, ambayo muda wa kuyalipa umetimia, kwa lengo la kujenga imani ya kukopeshwa.

Wakati majukumu ya malipo ya madeni yakitekelezwa, utoaji fedha kwa ajili ya elimu bure na huduma nyingine muhimu unaendelea kikamilifu.

Pia kuna shutuma kuwa Serikali haiipi umuhimu sekta binafsi. Lakini ukweli ni kwamba sera ya CCM iko wazi katika hilo; kwamba sekta binafsi ni injini ya ukuaji uchumi, na hivyo haiwezi kuachwa katika mchakato kustawisha nchi.

Wote tunajua kuwa madini, mafuta na gesi, miundombinu na sekta ya huduma ni muhimu katika kuiendeleza nchi na kuifanya iwe ya uchumi wa kati. Rais mwenyewe alitangaza hilo vizuri wakati akizindua Bunge Novemba mwaka jana. Alielezea nia yake ya kusaidia sekta binafsi katika jukumu la Serikali la kuifanya nchi iwe ya viwanda.

Pia alisema ataondoa matatizo yaliyokuwepo ya kuwekeza nchini yalitokana na urasimu, mlololongo wa taratibu, ucheleweshaji usio wa lazima na rushwa. Ameitaka sekta binafsi kuchukua hatua za kuishirikisha Serikali. Wakati huohuo, mawaziri na maofisa waandamizi wa idara zote za Serikali wametakiwa kutafsiri kwa vitendo nia ya Serikali kwa sekta binafsi.

Sera ya CCM katika jukumu la sekta binafsi katika kujenga ustawi wa jamii na kutengeneza ajira si tu imefafanuliwa, bali pia imewekwa makusudi kuifanyia mageuzi nchi.

Katika ziara iliyomalizika hivi karibuni nchini Kenya, Rais Magufuli alisisitiza nia ya kuendeleza biashara na uwekezaji baina ya nchi hizi mbili ambazo ni wanachama wa EAC. Rais alisisitiza jambo hilo wakati wa ziara yake nchini Uganda na Rwanda.

Huu ni ushahidi mwingine wa wazi wa mkakati wa sera za nje za Rais Magufuli za kuendeleza ujirani mwema na utangamano wa kikanda.

Moja ya miradi mikubwa kwenye ilani ya CCM ni ujenzi wa reli ya kiwango cha kimataifa itakayounganisha Tanzania na nchi zisizopakana na bahari za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Uganda, Rwanda na  Burundi ili kufanikisha usafirishaji katika ukanda wa kati.

Reli hii itachangia kwa kiasi kikubwa maendeleo ya kiuchumi, si tu wa Tanzania bali pia nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na nchi jirani ya DRC. Matayarisho ya awali tayari yameanza na nia ya serikali kutekeleza na kuumaliza mradi huo ndani ya miaka mine, imewekwa bayana na Rais na kusisitizwa na mawaziri wake.

Katika mpango wa kufufua Kampuni ya Ndege ya Tanzania (ATCL), ambayo ni kioo cha taifa lakini iko kwenye hali mbaya, Serikali imeshanunua ndege mbili na mipango inaendelea kununua ndege mbili kubwa zaidi kwa ajili ya safari za nje.

Kuonyesha kuwa ni kiongozi shujaa, baada ya uamuzi wa kuhamishia makao makuu ya nchi mjini Dodoma miaka 40 iliyopita, Dk Magufuli ameshaanza kutekeleza uamuzi huo katika mwaka mmoja pekee.

Ameshaweka bayana kuwa anataka kuiona Serikali na taasisi zake zinahamia Dodoma katika kipindi cha miaka minne ijayo na kuifanya Dar es Salaam kuwa jiji kamili la kimataifa la biashara.

Kwa sababu ya nia yake ya kuwatumikia Watanzania, haikuwa ajabu wakati Serikali iliposifiwa kutokana na nia yake ya kupambana na masuala ya rushwa, utendaji mbovu na ufanisi katika utafiti uliofanywa na Twaweza mwezi mmoja uliopita.

Asilimia 80 ya watu waliotakiwa kutoa maoni yao kuhusu shughuli za upinzani, walisema kuwa Watanzania wa mirengo tofauti ya kisiasa waisaidie Serikali  kuleta maendeleo nchini kwa kuwa uchaguzi umeshapita.

Mwandishi wa makala hii ni Katibu Mkuu wa CCM.

-->