Jinsi ya kudhibiti mlipuko wa homa ya bonde la ufa

Homa ya Bonde la Ufa (RVF) ni moja ya maradhi yenye asili ya wanyama ambayo pia huweza kuenezwa kwa binadamu. Maradhi haya kitaalamu yanaitwa ‘Zuonosia’.

Ugonjwa huu husababishwa na virusi ambavyo huanza kushambulia mifugo na baadaye huweza kuenezwa kwa wanadamu pia. Maambukizi ya virusi vya ugonjwa huu yanaweza kusababisha dalili ndogo na ugonjwa hatari kwa wanyama hususan ng’ombe, mbuzi, kondoo, ngamia na binadamu, ambao husababishwa na virusi jamii ya Bunyaviridae.

Wanyama huambukizwa kwa kuumwa na mbu aina ya ‘Aedes’. Binadamu hupata ugonjwa kwa kushika au kula nyama ya mnyama aliyeambukizwa na virusi vya ugonjwa huo.

Katika siku za hivi Mamlaka ya Hali ya Hewa Kenya, Shirika la Afya ya Wanyama Duniani (OIE) na Shirika la Afya Duniani (WHO) wametoa taarifa za matukio ya ugonjwa wa Homa ya Bonde la Ufa (RVF) Kaskazini mwa Kenya na Mashariki mwa nchi ya Rwanda.

Hata hivyo Wizara ya Mifugo na Uvuvi inasema hakuna eneo lolote nchini lililoripotiwa kuwapo kwa ugonjwa huo hadi sasa.

Katibu Mkuu anayeshughulikia mifugo, wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dk Mary Mashingo akizungumzia ugonjwa huo anasema kutokana na kuwapo kwa ugonjwa huu katika nchi jirani, wizara imeshatoa maelekezo kwa Halmashauri na idara zote za mifugo, afya na elimu nchini, kuchukua tahadhari zote zinazotakiwa ili ugonjwa huo usiweze kuingia nchini.

“Nimeshaagiza halmashauri zianze kutoa taarifa na elimu kwa umma, hasa kwa wadau wote wanaofanya shughuli za mifugo, utoaji wa huduma za afya kuhusu njia sahihi za kudhibiti maambukizi au mlipuko wa ugonjwa huu,” anasema Dk Mashingo.

Anasema halmashauri zinatakiwa kuwahimiza wafugaji kuogesha mifugo yao mara kwa mara kwa kutumia viuatilifu vyenye kiini cha pareto au pyrethroids ili kudhibiti kupe, mbu, mbung’o na visumbufu wengine waenezao maradhi.

Wananchi nao wanapaswa kutoa taarifa haraka kwa wataalamu wa mifugo, vituo vya huduma za afya au vituo vya uchunguzi wa maradhi ya mifugo mara wanapoona vifo vingi vya ghafla kwa wanyama, kutupa au kuharibu mimba na wengine kuzubaa kwa homa kali.

Katibu mkuu huyo anasema hatua nyingine ni ile ya halmashauri kuanza kutoa elimu kwa umma na kuhahakisha wanyama wote wanachinjiwa machinjioni na wapimwe na nyama yao pia ipimwe na mtaalamu wa mifugo kabla na baada ya kuchinjwa. Aidha, nyama zinunuliwe kwenye maduka ya nyama yaliyoidhinishwa.

Wakizungumzia ugonjwa huo, wataalamu wa mifugo wanasema ugonjwa huo uliripotiwa mara ya kwanza katika maeneo ya Bonde la Ufa la Kenya miaka ya mwanzoni mwa 1900, na virusi vyake vilitambuliwa kwa mara ya kwanza mwaka wa 1931 wakati wa uchunguzi wa kitaalamu wa kondoo katika shamba moja huko Bonde la Ufa la Kenya.

Tangu wakati huo, mlipuko wa ugonjwa huu imekuwa ikiripotiwa kusini mwa Jangwa la Sahara na Kaskazini mwa Afrika.

Mara nyingi mlipuko wa ugonjwa huu hutokea katika misimu ya mvua nyingi inayosababisha ongezeko la idadi ya mbu. Mwaka 1997-1998 mlipuko mkubwa ulitokea Kenya, Somalia na Tanzania. Septemba, 2000 kesi kadhaa za ugonjwa huo zilithibitika Saudi Arabia na Yemen, zikifanya kesi za kwanza kuwahi kuripitiwa nje ya Bara la Afrika, hali hii iliongeza wasiwasi zaidi kwa mataifa mengine.

Baadhi ya watu hujiuliza ugonjwa huo unaenea namna gani.

Daktari wa Mifugo, Julius Matheru anasema wanyama wafugwao kama ng’ombe, kondoo, mbuzi na ngamia, wanaweza kuathiriwa. Ugonjwa huu mara nyingi husambazwa na mifugo hao kupitia mbu aliyebeba kirusi cha ugonjwa.

Dk Matheru anasema kirusi cha RVF kinaweza kumpata mtu pindi anaposhika damu au nyama yenye maambukizi wakati wa kuchinja, kupumua hewa ya eneo la machinjio ya wanyama lenye maambukizi, kukata nyama iliyo na maambukizi buchani au nyumbani, kunywa maziwa mabichi (yasiyochemshwa) ya mnyama aliyeambukizwa virusi. “Pia, wakati wa kumsaidia kuzaa mnyama aliyeambukizwa, wakati wa kutoa huduma kwa mifugo iliyo na maambukizi au taka za vitoto vilivyozaliwa kwenye maambukizi au kuumwa na mbu walioambukizwa hasa aina ya ‘Aedes’,” anasema daktari huyo wa mifugo.

Anasema kirusi cha RVF kinaweza kusambazwa na nzi wanaokula damu. Hata hivyo, anasema hakuna ripoti inayodai kuna maambukizi kutoka kwa binadamu mmoja hadi kwa mwingine pia hakuna maambukizi yaliyoripotiwa kwa mtumishi wa afya waliochukua tahadhari za kujikinga na maradhi wakati wakitoa huduma kwa wagonjwa wa RVF.

Dalili za ugonjwa

Ugonjwa wa Homa ya Bonde la Ufa (RVF) huchukua siku mbili hadi sita tangu kuambukizwa na dalili kuanza kutokea.

Dk matheru anasema walioambukizwa wanaweza wasiwe na dalili zozote mwanzoni, baadhi wanaweza kupata dalili ndogo ndogo kama mafua na homa, kuumwa misuli na viungo na kuumwa kichwa.

Wapo ambao pia hupatwa na ugumu katika shingo, kukerwa na mwanga, kukosa hamu ya kula, kichefuchefu na kutapika. Katika hatua za mwanzo, wagonjwa wa RVF wanaweza kufananishwa na wagonjwa wa Homa ya Uti wa Mgongo (Meninjitisi).

Anasema dalili za RVF hudumu kwa siku nne hadi saba na baada ya hapo, mfumo wa kinga huitikia na kufanya virusi vionekane kwenye antibodi na huanza kupotea muda hadi muda. Hivyo utambuzi hufanywa kwa kutafuta antibodi za kukabiliana na virusi au uwapo wa virusi vyenyewe katika damu.

Bainisho la ugonjwa huu linaweza kufanyika kwa vipimo vya damu ili kuangalia antibodi. Kirusi chenyewe kinaweza kugundulika kwenye damu kipindi cha mwanzo cha ugonjwa kwa vipimo vya antijeni na RT-PCR.

Ingawa wengi walioambukizwa huwa na dalili ndogo, Dk Matheru anasema asilimia chache hupata dalili kali zaidi. Anasema hizo hufanya hali ya mgonjwa kuwa mbaya. Dalili hizo ni pamoja na ugonjwa wa macho ambao humsababishia mgonjwa kupoteza uwezo wa kuona wiki ya tatu baada ya kuambukizwa.

Muathirika naweza kupatwa na maumivu makali ya kichwa na unaweza kumsababishia kuchanganyikiwa na nyingine ni kwa mgonjwa kutokwa na damu hali inayoweza kumsababishia kifo.

Nini matibabu na chanjo yake?

Dk Matheru anasema kwa kuwa wengi walioambukizwa huwa na dalili ndogo na za muda mfupi, hakuna tiba au dawa maalumu ya ugonjwa huo, ingawa wagonjwa wenye dalili kali hupewa matibabu ya kuwasaidia kupunguza ukali wa ugonjwa.

Jinsi gani ujikinge?

Katibu Mkuu Dk Mashingo anasema ili kujikinga na ugonjwa huo, ni kwa wananchi kutoa taarifa mapema mara wanapobaini dalili zinazoainishwa na wataalamu.

Anasema ni muhimu kwa watu kutoa taarifa kwa madaktari wa mifugo, ili waweze kuzuia mlipuko wa ugonjwa huo. “Kinga ya ugonjwa huu kwa binadamu ni kwa kuchanja wanyama dhidi ya ugonjwa wenyewe, chanjo lazima ifanywe kabla ya mzuko kwa sababu ikifanywa wakati wa mzuko inaweza kuzorotesha hali hii,” anasema Dk Mashingo.

Kuzuia mifugo kuhama kutoka sehemu ya maambukizi kwenda sehemu nyingine wakati wa mlipuko. Ikiwa kuna mlipuko, wananchi wanashauriwa kuendelea kujikinga na hali hatarishi kama damu ya wanyama, kujikinga na mbu na nzi wanaokula damu, kupika nyama na kuchemsha maziwa vizuri kabla ya kutumia.