Jukumu la malezi ya watoto ni letu sote

Muktasari:

  • Hali hii inatokana na kuongezeka kwa vitendo vya kihalifu na vya kufedhehesha katika jamii ya Watanzania.
  • Kukithiri kwa matukio ya wizi, ujambazi, mauaji hata kwa wasio na hatia, uvaaji wa nguo zinazoonyesha maungo ya mwili, matumizi ya dawa za kulevya na vileo ni baadhi ya tabia zilizoota mizizi katika jamii zetu nchini.

Kwa sasa kila mahali ni kilio cha kuporomoka kwa maadili kuanzia ngazi ya familia hadi Taifa.

Hali hii inatokana na kuongezeka kwa vitendo vya kihalifu na vya kufedhehesha katika jamii ya Watanzania.

Kukithiri kwa matukio ya wizi, ujambazi, mauaji hata kwa wasio na hatia, uvaaji wa nguo zinazoonyesha maungo ya mwili, matumizi ya dawa za kulevya na vileo ni baadhi ya tabia zilizoota mizizi katika jamii zetu nchini.

Kuna tatizo kubwa katika mifumo ya malezi kuanzia ngazi ya familia na hata kwenye mifumo ya elimu.

Huko kote watoto wanaishi kwa namna ambayo inafedhehesha na hakuna anayechukua hatua madhubuti wakati watoto wanapokengeuka.

Msingi wa malezi ya watoto yanaanzia kwenye ngazi ya familia na mtu wa kwanza kuwa na maadili ni mzazi mwenyewe.

Kwa mfano, tutarajie vipi mtoto kuwa na hofu ya Mungu kama wazazi hawaendi msikitini au kanisani kwa kukosa imani ya dini? Hivi mtoto anaanzaje kujenga hofu ya kutenda dhambi kama hajui kwamba kuna Mungu?

Kuna suala la mfumo wa maisha ya kila siku; kwamba wazazi au walezi wanatakiwa kutengeneza msingi wa kimaadili kwa mtoto kuanzia chini kujua nini kizuri cha kuiga na nini kibaya cha kukiepuka.

Tusipokuwa makini watoto wetu hawawezi kubaki salama hasa wakati huu wa zama za utandawazi na maendeleo makubwa ya teknolojia.

Teknolojia na utandawazi, lazima vitumike kuleta tija na maendeleo na si madhara ya kuharibu watoto wetu na jamii kwa jumla.

Kwa mfano, huwa napata shida ninapowaona baadhi ya wazazi wakiwapa uhuru mkubwa watoto wao kuangalia kila kipindi cha televisheni hata vile vyenye ukakasi wa kimaadili.

Wazazi tunapenda watoto waangalie katuni, lakini tunashindwa kukagua vipindi hivyo kuona kama vinawajenga watoto kimaadili au vinawabomoa, hasa wakati huu ambao baadhi ya katuni zinatumika kuchochea vitendo vichafu vya ushoga.

Kimsingi, wazazi hawawajibiki na ndio maana gazeti hili liliwahi kuripoti siku za nyuma kuwa wapo baadhi ya wazazi wanaoshindwa hata kugundua vitendo vya unyanyasaji wanavyofanyiwa watoto wao nyumbani.

Huu ni ushahidi kuwa wazazi hawana muda wa kufuatilia mienendo ya watoto wao.

Kinachosikitisha katika uporomokaji huu wa maadili ni kuona kuwa jamii haina habari na watoto. Kila mtu haoni kama ana jukumu la kuhimiza malezi kwa watoto hata wasiokuwa wake.

Ubinafsi huu umesababisha watoto kuwaogopa wazazi wao tu na si mtu mwingine, na hili limekuzwa na utetezi wa kijinga wa wazazi wenyewe hasa wale wanaokuja juu watoto wao wanapoadhibiwa na watu baki.

Ubaguzi wa huyu mtoto wangu na huyu si wangu kwa hiyo hata akikengeuka suala lake halinihusu, ndio uliotufikisha hapa tulipo.

Sote tuna jukumu la kusaidiana kukemea pale ambapo mtoto ametenda kosa na hivi ndivyo ilivyokua huko zamani kwamba mtoto akitenda kosa anaadhibiwa na mzazi yeyote.

Baadhi ya wazazi wa pili ambao ni walimu, nao wamepoteza sifa na uadilifu wa kuwa walimu. Wapo walimu na tafiti zinaonyesha ndio vinara wa kuharibu watoto ambao kimsingi wanapaswa kuwalea katika maadili mema.

Kuna kazi kubwa inatakiwa kufanyika hasa kwenye mchujo wa walimu. Kuna watu wameivamia fani hii adhimu lakini hawana kabisa sifa ya kuitumikia.

Hivi sasa mitaani iwe mijini au vijijini, mabanda ya kuonyesha filamu yametamalaki. Mengi huonyesha filamu zisizo na maadili, huku wateja wao wakubwa wakiwa ni watoto.

Iko haja kwa vyombo husika serikalini kufanya operesheni maalumu ya kufungia mabanda haya kwa sababu yanachangia watoto kuharibika kimaadili. Ni bora tukose kodi kama wanalipa, kuliko kuwaacha wahusika wakiendelea kuwaathiri watoto wetu.

Katika makala haya, nimewalenga watoto zaidi kwa sababu utoto ndiko hasa tunapoanza kujenga msingi wa maadili. Tunapokosea huko, ni wazi kwamba tunatengeneza taifa ambalo litagubikwa na kila aina ya maovu.

Ni muhimu tukafahamu kuwa jukumu la ulezi wa watoto wetu ni letu sote kuanzia nyumbani, mtaani, shuleni na taifa kwa jumla.

Kila mmoja akemee na kuuondoa uchafu anapouona kwa mkono wake. Tukumbuke msemo; mtoto wa jirani yako ni wa kwako pia.

Aziz Msuya ni mwandishi wa Mwananchi mkoani Morogoro, unaweza kuwasiliana naye kwa namba ya simu: 0716069926