KAKAKUONA : Rais Magufuli, wafanye wapinzani jicho lako la pili

Muktasari:

  • Mikutano hii, hakika na ninaamini ingemsaidia kujua wapi alipotoka, alipo sasa na kule anakoelekea kwa sababu hiyo ni fursa muhimu kwao kumkosoa pale alipoteleza na kumshauri aendeje.
  • Katika makosa makubwa aliyoyafanya Rais, ni kuzuia mikutano hiyo. Hapati mawazo mbadala kwa sababu waliomzunguka (kwa mtazamo wangu) wanamweleza kile anachopenda kukisikia.

Kama ningeteuliwa kuwa mshauri wa Rais katika masuala ya siasa, ushauri wangu wa kwanza kwa Rais John Magufuli, ungekuwa kuruhusu mikutano ya ‘kitaifa’ ya vyama vya siasa.

Mikutano hii, hakika na ninaamini ingemsaidia kujua wapi alipotoka, alipo sasa na kule anakoelekea kwa sababu hiyo ni fursa muhimu kwao kumkosoa pale alipoteleza na kumshauri aendeje.

Katika makosa makubwa aliyoyafanya Rais, ni kuzuia mikutano hiyo. Hapati mawazo mbadala kwa sababu waliomzunguka (kwa mtazamo wangu) wanamweleza kile anachopenda kukisikia.

Labda niwakumbushe tu, zuio la mikutano ya kisiasa ya hadhara kwa viongozi wa kitaifa (siyo wabunge na madiwani), lilitolewa Ikulu jijini Dar es Salaam na Rais Magufuli Juni 24 mwaka huu.

Rais alisema asingependa watu wamcheleweshe katika kutekeleza ahadi alizowaahidi Watanzania wakati akiomba ridhaa ya kuiongoza nchi, hivyo mikutano ya aina hiyo haitakuwapo hadi mwaka 2020.

Alitoa kauli hiyo Ikulu Dar es Salaam baada ya kukabidhiwa ripoti ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 na Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji mstaafu Damian Lubuva.

“Niwaombe wanasiasa wenzangu wafanye siasa za ushindani kwa nguvu zote baada ya miaka mitano ili wananchi watuhoji tuliyoyaahidi kama tumeyatekeleza au hatujayetekeleza,” alisema Rais.

“Yapo tuliyoyaahidi kuyatekeleza kwa wananchi katika kipindi cha miaka mitano, nisingependa kuona mtu yeyote ananichelewesha kutekeleza hayo niliyoahidi kwa kipindi cha miaka mitano,” alisema Rais.

Tumesikia kauli za wasomi na wanasiasa wakikosoa vikali uamuzi huu wa Rais kuwa unakiuka kifungu cha 11(1) A cha sheria ya vyama vya siasa ya mwaka 1992 na Katiba yetu ya mwaka 1977.

Bahati mbaya, wakati akitoa tamko hilo, washauri wake hawakuwa wamemweleza kuwa mwaka 2019 tunapaswa kuwa na kampeni kwa ajili ya uchaguzi wa viongozi wa vijiji, vitongoji na mitaa.

Katika kipindi cha mwaka mmoja wa utawala wake, pasipo kuwa mnafiki, kumejengeka hofu miongoni mwa viongozi ndani ya CCM yenyewe, serikalini na wananchi katika kumkosoa Rais na utawala wake.

Ni kwa msingi huo huo, hata wabunge wengi wa CCM wanashindwa kuisimamia vizuri Serikali ndani ya Bunge na hata wale wachache wanapojitokeza kuikosoa, hutazamwa kwa jicho baya.

Katika mazingira ya aina hii, ni dhahiri vyama vya upinzani imara ndivyo vingeweza kumsaidia Rais kuwa jicho la pili, kumweleza bila hofu kama amesimama au ameanguka, amevaa nguo au yuko uchi.

Mifano iko mingi ambayo kama siyo upinzani, tusingeweza kufahamu kashfa ya Sh133 bilioni ya Akaunti ya Madeni ya Nje (Epa), mwaka 2008 na mlolongo wa kashfa nyingine zilizofuatia.

Kama mtakumbuka, Waziri wa Fedha wakati huo, Zakhia Meghji na Serikali ya CCM kwa ujumla wake ilikana kabisa kuwapo kwa kashfa hii licha ya upinzani kufichua ufisadi huo na vielelezo.

Baada ya upinzani kusimama kidete ndipo baadaye tukaona baadhi ya wafanyabiashara waliokwapua fedha hizo wakiwamo makada wa CCM wakizirejesha na wengine kuburuzwa mahakamani.

Ni kupitia mikutano hiyo ya hadhara kwa viongozi wa kitaifa, tungepata jicho la pili kama tuko katika mstari sahihi katika masuala ya uchumi na kama tutaifikia ndoto ya Tanzania ya viwanda mwaka 2020.

Mikutano hii ingetusaidia kupata mawazo mbadala kama kupungua kwa mzunguko wa fedha mitaani kumesababishwa na watu kuficha fedha au ni kwamba uchumi wetu unaelekea kuchungulia kaburi.

Haya na mengine mengi, tungeweza kuyapata kupitia mikutano hiyo ya kisiasa hasa vyama vya upinzani, na mifano iko mingi lakini tukienda kibububu hivi hatujui tumesimama au tumekaa. Rais asione soni kurejea uamuzi wake huo na kurejesha demokrasia kwa vile manufaa yake ni makubwa na pale wanapotema nyongo, ndipo humsaidia kujua yuko njia sahihi ama la.

Hakuna utafiti wowote unaounga mkono hoja ya Rais kuwa kufanyika kwa mikutano hiyo kungemzuia kutekeleza ahadi zake. Tujiulize, mikutano hiyo inamzuia vipi kushughulikia mafisadi au ujenzi wa viwanda?

Asiwachukulie viongozi wa upinzani kama maadui, hapana. Katiba yetu inatambua uwepo wa vyama vingi vya siasa. Asimame kwenye utawala wa sheria ili wanapokiuka sheria washughulikiwe kisheria.

Kuzuia mikutano ya kisiasa hakuna afya yoyote kwa nchi yetu zaidi ya kujenga chuki zisizo za lazima kati ya watawala na watawaliwa na Rais na viongozi wa kitaifa wa vyama vya upinzani.

0769600900