KUELEKEA DODOMA: Wizara nne zaazimwa majengo ya Udom

‘Tumezingatia umuhimu wa taasisi za Serikali kuunga mkono agizo la Rais la kuhamia Dodoma. Majengo haya watayatumia kwa muda wakati wakijenga ya kwao ya kudumu.’
Makamu Mkuu wa Chuo, Profesa Idris Kikula

Muktasari:

  • Makamu Mkuu wa chuo hicho, Profesa Idris Kikula alizitaja wizara hizo kuwa ni Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Wizara ya Katiba na Sheria na Ofisi ya Rais Mejimenti ya Utumishi wa Umma.

Dodoma. Baada ya majadiliano ya kina  Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom) sasa kimekubali majengo yake kutumiwa na wizara nne kama ofisi za muda wakati wakiendelea na ujenzi wa ofisi za kudumu mkoani hapa.

Akizungumza jana Makamu Mkuu wa chuo hicho, Profesa Idris Kikula alizitaja wizara hizo kuwa ni Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Wizara ya Katiba na Sheria na Ofisi ya Rais Mejimenti ya Utumishi wa Umma.

“Baada ya majadiliano tumekubali majengo yetu mapya ambayo yalijengwa kwa ajili ya ofisi lakini hayatumiki, sasa yanaweza kutumiwa kwa muda wakati wakijenga ya kwao ya kudumu mjini hapa,” alisema.

Profesa Kikula alisema majengo hayo yako mbali na hayawezi kuleta athari ya kukosekana utulivu kwa wanafunzi wanaosoma kwenye chuo hicho.

“Tumezingatia pia umuhimu wa taasisi za Serikali kuunga mkono agizo la Rais (Dk John Magufuli) la kuhamia mkoani hapa. Majengo haya watayatumia kwa muda wakati wakijenga majengo ya kwao ya kudumu,” alisema.

Aidha alisema katika uamuzi huo walizingatia uwezekano wa majengo hayo kuharibika kutokana na kutotumiwa kwa shughuli za chuo.

Aliyataja majengo hayo ni Kituo cha Utafiti cha Asha-Rose Migiro na mengine kwenye Chuo cha Sayansi ya Jamii (College of Humanities and Social Sciences).

Julai 23 Rais Magufuli akihutubia Mkutano Mkuu wa CCM  mara baada ya kuchaguliwa kuwa mwenyekiti wa Taifa wa chama hicho alitangaza kuwa katika kipindi cha miaka minne iliyosalia ya uongozi wake, Serikali itakuwa imehamia mkoani hapa.

Julai 25 mwaka huu katika sherehe za siku ya mashujaa mkoani hapa, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alitangaza kuhamia mjini hapa ifikapo Septemba.

Majaliwa aliunda kikosi kazi kichoratibiwa na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Jordan Rugimbana ambacho kilibaini kuwa majengo ya ofisi yanaweza kupatikana kwa asilimia 70 huku  nyumba za kuishi kupatikana kwa asilimia 75.