KULEKEA DODOMA: Cowtu yabisha hodi Dodoma

TUNASIKILIZA: Wajumbe wa Baraza Kuu la Chama cha Wafanyakazi Sekta ya Mawasiliano na Uchukuzi Tanzania (Cotwu) wakiwa kwenye mkutano wa chama hicho uliofanyika mjini Dodoma jana. Picha na Anthony Siame

Dodoma. Chama cha Wafanyakazi wa Sekta ya Mawasiliano na Uchukuzi Tanzania (Cowtu), kimebisha hodi Dodoma kikitaka kuwa wa kwanza kuhamia mjini hapa kuliko vyama vingine vyote.

Kaimu Mwenyekiti wa Cowtu, Idrisa Washington alisema jana kuwa tayari wameshawasilisha barua ya maombi ya kupatiwa kiwanja na kabla ya hivyo watapanga jengo la muda.

Washington alisema mamlaka zinazohusika na viwanja akiwamo Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu Dodoma (CDA) ambaye ni Waziri wa nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Jenista Mhagama wameshapewa taarifa na leo Mhagama anatarajia kuwa mgeni rasmi kwenye mkutano wao mkuu wa uchaguzi hivyo atakwenda na majibu. “Leo tunatarajia kupewa majibu ya nini kinaendelea, lengo ni kuhamia kabla ya vyama vyote maana sisi tumetoka katika mgogoro mkubwa hivyo lazima kuanza kazi kwa kasi kubwa,” alisema Washington.

Awali, Kaimu Mwenyekiti huyo alifungua kikoa cha baraza kuu la chama hicho katika Ukumbi wa Morena huku akisisitiza suala la mshikamano na utulivu ndani ya chama.

Aliwata viongozi waliochaguliwa na watakaochaguliwa leo katika uchaguzi kwenye mkutano mkuu, kufanya kazi inayoendana na kuwasaidia wanachama lakini wakienda kinyume na hapo hakutakuwa na kubebana.

Mwenyekiti huyo aliwakumbusha wajumbe wake kuchagua viongozi wenye weledi na wenye kuzingatia masilahi mapana kwa wanachama wao lakini wakikosea na kuchagua viongozi wasioweka maslahi ya chama na wanachama mbele, hiyo itawagharimu kwa muda wa miaka mingine mitano.

Kaimu Katibu Mkuu wa Cowtu, Juliana Mpanduji aliwataka wajumbe kufanya kazi kwa kujitolea zaidi kuliko kutegemea masilahi ya fedha kwani hayo yatakuja baadaye.

Mpanduji alisisitiza suala la uvumilivu na kusaidiana kwa namna yoyote ikiwamo kutoa ushirikiano kwa viongozi ili kujiepusha na migogoro.