Kamera za CCTV ziimarishe usalama wa Watanzania

Muktasari:

  • Masauni alisema lengo la Serikali kununua kamera hizo ni kuimarisha ulinzi na usalama ili kukabiliana na matukio mbalimbali ya uhalifu yakiwemo ya kutekwa kwa watu.

Mwishoni mwa wiki iliyopita, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamad Yusuf Masauni alizungumzia mpango wa Serikali wa kununua kamera maalumu za CCTV na kuzifunga katika miji mikubwa na mikoa iliyopo karibu na mipaka ya nchi.

Masauni alisema lengo la Serikali kununua kamera hizo ni kuimarisha ulinzi na usalama ili kukabiliana na matukio mbalimbali ya uhalifu yakiwemo ya kutekwa kwa watu.

Hakika tunakaribisha kwa mikono miwili mpango huo wa Serikali hasa ikizingatiwa kwamba kwa dunia ya sasa matumizi ya teknolojia hayaepukiki kutokana na mazingira ya utendaji kazi wa polisi kuwa na changamoto nyingi ambazo baadhi yake zinakwaza utekelezaji wa majukumu yao.

Tunajua kamera hizo ni ghali, lakini Serikali haikuangalia gharama, bali thamani ya uhai wa raia, usalama na mali. Na katika kipindi hiki inapowekeza katika usalama wa raia wake ina maana inathamini nguvu kazi muhimu katika ujenzi wa uchumi wa viwanda.

Hadi sasa Serikali imesema watu 75 wametekwa na watu wasiojulikana katika kipindi cha miaka mitatu, lakini pia wapo wengine walioshambuliwa na kuuawa huku kazi ya kuwasaka wahalifu hao ikiwa ngumu. Baadhi ya waliopotea ni wafanyakazi na wafanyabiashara ambao ni muhimu katika maendeleo ya nchi.

Ndiyo maana tunapongeza hatua ya Serikali kununua na kusambaza nchini CCTV, yaani mfumo wa ufuatiliaji unaojumuisha kamera, rekodi na picha ni wa kupongezwa kwani utasaidia kubaini matukio mengi ambayo kwa sasa inakuwa vigumu kuyagundua.

Kuna matukio ya wizi, uporaji, madereva kugonga na kuharibu alama za barabarani au baadhi kutiririsha mafuta na kusababisha utelezi barabarani na watu kuharibu tu mali za umma kama vile kung’oa nondo za madaraja na vivuko. Tunaamini CCTV zitakomesha haya.

Hata hivyo, tuseme wazi kabisa kwamba kamera za CCTV si kitu kipya kwani majengo mengi kama vile hoteli, mashirika na taasisi mbalimbali zimefunga kamera hizo, lakini uhalifu unafanyika kwenye maeneo hayo na kuelezwa kwamba kamera zimeshindwa kunasa matukio husika. Kwa nini?

Tuna kumbukumbu ya tukio la Julai 2013, kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa ambako mabinti wawili wa Kitanzania walipitisha dawa za kulevya na kusafirisha hadi Afrika Kusini ambako walikamatwa. Hapa nyumbani hawakukamatwa licha ya kuwepo mbwa wa kunusa na kamera za CCTV.

Hata tukio linalogonga vichwa vya watu la kutekwa kwa mfanyabiashara bilionea Mohammed Dewji, kuna madai kwamba kamera za CCTV zilizopo kwenye hoteli zimeshindwa kunasa tukio hilo, ila zimenasa matukio upande mwingine. Tumeyataja maeneo hayo mawili kwa sababu yametokea matukio makubwa ya uhalifu licha ya kuwepo mifumo ya usalama ya CCTV.

Tujiulize ni nani wenye uwezo wa kuchezea kamera hizo? Je, ni mara ngapi kamera zimechezewa ili zishindwe kubaini mathalan wafanyakazi wanaoiba nyaraka za Serikali?

Tunafahamu namna kamera kama hizo zinavyosaidia kufuatilia na kuwakamata wahalifu kwingineko duniani. Kamera za CCTV ndizo Februari 13, 2017 zilitumika kubaini wasichana wawili kwenye Uwanja wa Kimataifa Kuala Lumpur, Malaysia waliotumia kemikali na punde kumuua Kim Jong-nam, ambaye ni ndugu wa kiongozi wa Korea Kaskazini, Kim Jong-un. Wahalifu wale wameshtakiwa.

CCTV pia ndizo zimewasaidia Waingereza kubaini wahalifu waliomdhuru kachero wa zamani wa Urusi, Sergei Skripal na binti yake, Yulia mjini Salisbury.

Tunapounga mkono kufungwa kamera za CCTV tunataka zifanye kazi kama katika mataifa hayo tuliyotaja, ziwezeshe maisha yetu kuwa salama.