MAONI: Kamisheni ya Ngumi, BMT ziratibu mabondia

Muktasari:

  • Baada ya ushindi katika pambano hilo Mwakinyo alipanda katika ngazi za ubora kimataifa, kutoka nafasi ya 175 hadi 16 duniani hatua iliyochangiwa kwa kiasi kikubwa na rekodi za mpinzani wake.

Wiki iliyopita, Tanzania ilisifika kimataifa baada ya bondia wake, Hassan Mwakinyo kumtandika kwa TKO, raundi ya pili mwanamasumbwi Sam Eggington wa Uingereza katika pambano lililofanyika huko Birmingham, England.

Baada ya ushindi katika pambano hilo Mwakinyo alipanda katika ngazi za ubora kimataifa, kutoka nafasi ya 175 hadi 16 duniani hatua iliyochangiwa kwa kiasi kikubwa na rekodi za mpinzani wake.

Tunampongeza Mwakinyo kwa ushindi huo mkubwa ambao tunaweza kusema ni wa kihistoria katika ngumi za kulipwa nchini.

Pamoja na ushindi huo, habari ya Mwakinyo kusema kuwa alikwenda Uingereza kwa kuungaunga au kama mwizi imetushtua. Bondia huyo alifichua hilo alipokuwa bungeni mjini Dodoma ambako pia alipata wasaa wa kukutana na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa.

Akizungumza na waandishi wa habari katika viwanja vya Bunge, Mwakinyo alisema alihangaika kupata viza ya kwenda Uingereza na kwamba hata nauli alilazimika kuomba kwa mwanafunzi ambaye ilikuwa akalipe ada lakini aliamua kumsaidia ili afike Uingereza kwa makubaliano ambayo wenyewe wanayafahamu.

Hivi karibuni, kulifanyika mabadiliko makubwa ya uendeshaji wa mchezo wa ngumi za kulipwa nchini ambao sasa utasimamiwa na chama kimoja ambacho ni Kamisheni ya Ngumi za Kulipwa (TPBRC).

Mabadiliko hayo yalifanywa na wadau wa ngumi katika mkutano wa kupitisha Katiba mpya ya kamisheni hiyo ambao Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe alishiriki.

Katika mkutano huo, Dk Mwakyembe alisema wadau wamefanya uamuzi wa kihistoria baada ya mchezo huo kusimamiwa na waliokuwa viongozi wa kampuni binafsi zilizolenga zaidi kujinufaisha badala ya kujali masilahi ya mabondia na mchezo huo kwa ujumla.

Kwa mabadiliko hayo, mchezo huo sasa utasimamiwa na TPBRC, tofauti na miaka ya nyuma ambako kulikuwa na migongano na mivutano ya kila kukicha kutoka kampuni zilizojiita vyama ili kujihalalishia kufanya shughuli za ngumi kama PST, TPBO, TPBF na TPBC kila upande ukidai kuwa na haki na mamlaka ya kusimamia mchezo wa ngumi ikiwamo kuandaa na kuratibu mapambano na kuwasafirisha mabondia kwenda kucheza nje ya nchi.

Dk Mwakyembe alisema baada ya Katiba kupitishwa na msajili, utafanyika uchaguzi mkuu kupata viongozi. Kwa sasa kamisheni hiyo inasimamiwa na Baraza la Michezo la Taifa (BMT) na katika kipindi hiki cha mpito, tunadhani ni muhimu kufanya uhakiki wa mabondia wote waliopo na kuwajua mawakala au vyama vinavyowasimamia ili kuratibu mipango yao ya mapambano kwa kila hatua.

Tunashauri wakati tukisubiri uchaguzi wa TPBRC, BMT ibebe dhamana kwa kuwatambua na kuwasajili mabondia wote wa ngumi za kulipwa nchini, kuitambua mikataba waliyonayo na kuratibu mapambano yao ya ndani na nje ya nchi.

Ikiwa itajulikana kila bondia yupo wapi au anakwenda wapi, itaisaidia BMT kujua kinachoendelea na hata bondia akipata matatizo huko ni rahisi kusaidiwa haraka ili tusisubiri kumsaka mchawi pindi tatizo litakapotokea.