Kauli ya Rais Magufuli iwazindue walimu usingizini

Muktasari:

Rais Magufuli aliwaeleza walimu kwamba wakati wanaidai Serikali, ni lazima pia waangalie fedha wanazokatwa katika mishahara yao zinatumikaje. Aliwaeleza kuwa wako walimu 286,000 na wanakatwa asilimia mbili kutoka kwenye mishahara yao kila mwezi. Je, wanajua fedha zinatumika vipi?

        Gazeti hili toleo la jana lilikuwa na habari iliyomnukuu Rais John Magufuli alipokuwa akifungua mkutano mkuu wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT), uliofanyika mjini Dodoma ambako ‘aliwauma sikio’ kwamba Benki ya Biashara ya Walimu (MCB) ni miongoni mwa benki ambazo ziko hatarini kufutwa kwa sababu inafanya vibaya.

Rais Magufuli aliwaeleza walimu kwamba wakati wanaidai Serikali, ni lazima pia waangalie fedha wanazokatwa katika mishahara yao zinatumikaje. Aliwaeleza kuwa wako walimu 286,000 na wanakatwa asilimia mbili kutoka kwenye mishahara yao kila mwezi. Je, wanajua fedha zinatumika vipi?

Alisema Benki ya Walimu haikopeshi walimu kama ilivyokusudiwa na badala yake inawakopesha wafanyabiashara ambao hata hawashiki chaki.

Alisisitiza kwamba Tanzania ina benki 58, lakini Benki ya Walimu ni miongoni mwa benki zenye mwelekeo wa kufutwa.

Maneno yaliyozungumzwa na Rais Magufuli yanapaswa kuwafikirisha walimu na kuchukua uamuzi ambao utakuwa na manufaa kwao, ikiwamo kurekebisha kasoro bila kuoneana aibu.

Tunajua benki hiyo ni miongoni mwa vitega uchumi vilivyoanzishwa na CWT kwa lengo la kumkomboa mwalimu anayeishi maisha duni kila kukicha. Pia, haitakuwa vema iwapo kauli ya Rais ya ‘kuwauma sikio’ wakaichukulia kisiasa.

Dhamira ya walimu kuanzisha vitega uchumi hivyo ni kujikwamua kimaisha kwa kupata huduma nafuu za kifedha kama vile mikopo. Lakini, kinachoshangaza licha ya kuenea kwa vitego uchumi hivyo bado hali ya maisha ya mwalimu ni duni sana.

Tunadhani kama walimu wanapenda kuendelea ushirika wao ambao ni jambo jema, wanapaswa kurekebisha kasoro zilizojitokeza kwa haraka na udharura wa pekee fedha walizochanga kwa kipindi kirefu sasa.

Ni imani yetu maisha ya mwalimu yangekuwa bora zaidi kama vitega uchumi hivyo vingetoa mikopo ya nyumba za gharama nafuu kwa walimu nchini. Tunaamini kwa kufanya hivyo kusingekuwa na mikakati ya kimkoa au wilaya kufanya harambee ya ujenzi wa nyumba za walimu.

Kinachoonekana hapa CWT na watetezi wengine wa haki za walimu wamejielekeza katika kudai madai yaliyopo Serikali na kusahau maeneo mengine ambayo wamewekeza fedha zao. Kwa kusema hivi si kwamba hatuna imani na CWT.

Hatua ya Rais Magufuli ‘kuwauma sikio’ walimu inawapasa wazinduke usingizini kama walikuwa wamelala, lakini pia wafanye juhudi za kuinusuru benki yao kwa lengo la kuokoa fedha walizowekeza huko. Pia, tunawashauri walimu kuwa wanapaswa kuyaangalia maeneo mengine ya uwekezaji uliofanywa na CWT kama vile Mwalimu House iliyopo Ilala jijini Dar es Salaam kujidhirisha kama kweli uwekezaji huo unafanyika kwa tija au kuna maeneo yanahitaji kuboreshwa.

Tunaamini bado walimu wana hoja ya kuendelea kufuatilia madai yao serikalini, lakini wanapaswa kupokea kwa namna ya pekee ushauri wa Rais Magufuli wa kuwataka kuangalia upande mwingine wa shilingi ili wasipoteze vyote.

Mazingira bora ya mwalimu ndiyo yanayomfanya aweze kutoa elimu bora, hivyo CWT inapaswa kujielekeza katika jukumu lake la msingi la kuboresha maisha ya mwalimu, ikiwa pamoja na kuwawezesha kuwa na makazi bora kwa kuwapa mikopo ya nyumba za gharama nafuu. CWT haitaeleweka kama zaidi ya nusu ya wanachama wake wataendelea kuishi maisha duni huku wakiendelea kuchukua fedha zao kila mwisho wa mwezi. Wito wetu kwa chama hiki kijielekeze kumkomboa mwalimu.