Kazi, cheo ni vifafanuzi vya kumtambulisha mtuhumiwa lakini havitendi kosa

Muktasari:

  • Alikuwa na malalamiko. Ni kuhusu kichwa cha habari katika gazeti hili, toleo la 8 Januari 2018. Kichwa hicho kinasomeka kama ifuatavyo: ‘Jinsi mhasibu alivyomuua mkewe, mtoto na shemeji yake.’

        Jumatatu wiki hii, saa 1.24 usiku, simu yangu ililia. Alikuwa Richard Mgendi. Huyu ni mhasibu. Alivyokuwa akizungumza, alionyesha kuwa mtu anayenifahamu. Sikukumbuka mara moja majina hayo; na yeye hakuonyesha nia ya kunikumbusha.

Alikuwa na malalamiko. Ni kuhusu kichwa cha habari katika gazeti hili, toleo la 8 Januari 2018. Kichwa hicho kinasomeka kama ifuatavyo: ‘Jinsi mhasibu alivyomuua mkewe, mtoto na shemeji yake.’

Malalamiko ya Mgendi ni juu ya matumizi ya neno “mhasibu” – jina au cheo cha mtu anayefanya kazi ya uhasibu.

Anasema “mhasibu hakuua.” Anasisitiza kuwa matumizi ya neno mhasibu, tena mwanzoni mwa kichwa cha habari na habari yenyewe, kunaelemea zaidi kwenye taaluma kuliko mtu anayedaiwa kufanya mauaji.

Mgendi anakubali kuwa hatimaye, katika kumtambulisha mtuhumiwa, bila shaka kazi yake, mahali anapoishi na uhusiano na wengine vingetajwa; lakini siyo kutaja jina la kazi katika nafasi ya mtuhumiwa.

Mlalamikaji ambaye baadaye alinieleza kwa maandishi kuwa anapenda kuitwa “Ndugu” na siyo “Bwana” kama nilivyokuwa nimemwashiria, anasema kutaja jina la kazi au taaluma ni kutanua wigo na kuonekana kuhusisha wahasibu au watu wengine.

Kulikuwa na mjadala kati ya Mhariri wa Jamii na mlalamikaji ulioendelea hadi saa 4.40 usiku ukihusisha kupelekeana taarifa na anwani. Kesho yake (Jumanne) nilimwandikia Mgendi kumshukuru kwa kuwasiliana na Meza ya Mhariri wa Jamii na kumwomba kuendelea kusoma vyombo vya habari vya MCL na kutoa maoni juu ya habari, uandishi na waandishi.

Anacholalamikia Mgendi si kipya. Uandishi wa taarifa, habari na, au vichwa vya habari kama anacholalamikia umekuwepo. Nimeshuhudia uandishi wa aina hiyo katika baadhi ya vyumba vya habari nilimopita nikitoa ushauri. Lakini mijadala imeibuka na kufa haraka.

Wakati wa kurejea mijadala hiyo ni sasa. Hebu tuangalie tena kichwa cha habari husika: Jinsi mhasibu alivyomuua mkewe, mtoto na shemeji yake.’

Je, hii yaweza kuwa na maana kwamba ndivyo wahasibu wanavyoua? Mwandishi wa kwanza niliyeuliza juu ya matumizi ya “mhasibu” alijibu haraka: “Wewe bwana ni mwandishi; tena wa miaka mingi. Huoni kuwa hiyo ni kufupisha; badala ya kutumia majina ya mtuhumiwa?”

Mhariri mmoja miongoni mwa wanne niliofanya mjadala nao juu ya hili, ndiye alisema, “Siyo sahihi. Kama huwezi kutumia jina au majina ya anayetuhumiwa, basi andika tu, ‘Atuhumiwa kuua mkewe, mtoto na shemeji yake.’

Hakuna ubishi kuhusu matumizi ya “njia ya mkato,” pale unapotumia jila la kazi. Ni mkato kweli. Mgogoro ni ile maana inayopatikana unapokuwa umetumia cheo badala ya jina la muhusika.

Kesho na keshokutwa tutakuwa na vichwa vya habari kama hivi: Daktari alivyoua shangazi yake. Injinia alivyonyonga mtoto wake. Mwalimu alivyozika binti yake. Kumbe na kwa uhakika, daktari hakuua; injinia hakunyonga na mwalimu hakuzika.

Kilichonifurahisha katika kutafuta maoni juu ya hili, ni pale mhariri mmoja aliposema “kama wanaotenda hawana majina makubwa; unaweka nafasi zao kijamii.” Ripota wa miezi mitatu amesema, kwa njia ya majibu, “kama hawafahamiki si ufanye tendo au mazingira ndiyo yawe kichwa cha habari?”

Mgogoro unapanuka pale kichwa cha habari kinapotumia neno “alivyoua” au “alivyonyonga,” ikiwa na maana ya kuonyesha ilivyotendeka, ilivyotokea au ilivyotendwa.

Kazi ya mtu, cheo chake, urefu wake, rangi yake na hata kabila lake, ni vifafanuzi vya nyongeza katika kumtambulisha mtuhumiwa lakini vyenyewe havitendi.

Angalia hili: Makengeza anusurika katika ajali; Kibogoyo abambwa na bangi. Matumizi ya maneno kwa njia hiyo huzaa ubaguzi; hata kama hauonekani haraka na moja kwa moja.

Unaweza kukuta mtu anaandika au anatamka, “Mkurya aadhibiwa; Mhaya anyongwa. Mhindi anyanyasa.” Ni akili na chembechembe za ubaguzi, hata kama tumezoea kuona yakitumika hivyo na sisi kunyamazia matumizi yake.

Lakini kuna kitu kingine katika habari inayojadiliwa ambacho mlalamikaji hakugusia. Turudi kwenye kichwa: ‘Jinsi mhasibu alivyomuua mkewe, mtoto na shemeji yake.’

Hakuna popote katika habari hiyo ambako kunaeleza au kunaonyesha “jinsi” yaliyotokea yalivyotokea. Jinsi hupatikana kwa utondoti – maelezo kamili, sahihi na timilifu.

Maelezo ya aina hiyo – ya kina na ya hatua kwa hatua – hayawezi kupatikana kwa kunukuu aliyechungulia dirishani wala polisi anayedai kuwa “chanzo cha mauaji ni “wivu wa mapenzi.” Tujadili.