Tuesday, October 10, 2017

Kazi iwe kuhamasisha kilimo, uvuvi, ufugaji wa kisasa

By Mwananchi

Mwishoni mwa wiki iliyopita, Rais John Magufuli alifanya uamuzi wa makusudi wa kuunda wizara mbili mpya ili kusaidia kuharakisha maendeleo kwa wananchi hasa katika awamu hii inayotilia mkazo uchumi wa viwanda.

Wizara mpya ni ya Madini baada ya kuigawa iliyokuwa inaitwa Wizara ya Nishati na Madini, na nyingine ni ya Ufugaji na Uvuvi baada ya kuigawa iliyokuwa inaitwa Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi.

Tunaungana na wadau wengine wa maendeleo kupongeza hatua hiyo, hasa ikizingatiwa mchango mkubwa wa wizara hizo katika maendeleo ya mwananchi mmojammoja na nchi kwa ujumla.

Hatua ya kuacha kilimo kuwa eneo linalojitegemea imefanywa kwa makusudi kutokana na mambo mawili. Kwanza sekta hiyo ndiyo inayoajiri watu wengi nchini kuliko ajira zote, na pili tunadhani Serikali inataka kuja na mkakati wa kuhakikisha kilimo, ufugaji na uvuvi katika awamu hii, vinatumia teknolojia ya kisasa kwa vitendo.

Baada ya uhuru, kutokana na umaskini wa kipato cha watu, mkazo ulikuwa kutumia majembe ya kukokotwa na wanyama (ng’ombe na punda) pamoja na mbolea. Baadaye mkazo ukawa kutumia matrekta, mbolea na dawa ya kuulia wadudu.

Katika awamu hii ya uhamasishaji na usimamizi wa uchumi wa viwanda, mbali ya Serikali kuendelea kuhamasisha matumizi ya matrekta makubwa na madogo yanayotumia injini yaani power tiller, tunashauri uangaliwe utaratibu wa kuwawezesha wakulima kutumia teknolojia nyingine rahisi ya mashine za mkono za kulimia, kupanda, kupalilia na kuvuna.

Mashine hizo, kama ambavyo watu huziona kwenye maonyesho ya biashara ndani na nje ya nchi na kwenye mitandao, zitaongeza wigo wa teknolojia hivyo kuwezesha wakulima kulima eneo kubwa kwa muda mfupi na pale wanapoambiwa na wataalamu kwamba mvua za kwanza ni za kupandia wafanye hivyo kwa vitendo.

Miaka mingi iliyopita tatizo la wakulima wengi lilikuwa kuachana na jembe la mkono lakini baadaye wengi wao waliliacha, lakini hata hao walioliacha wapo wasiotumia mbolea na dawa ya kuua wadudu.

Tena wapo baadhi ya wakulima, hata Serikali inajua, kwamba wanapewa mbolea ya ruzuku ili wapandie lakini wanauza na wao hupanda mazao katika ardhi iliyochoka na hatimaye hupata mazao kiduchu.

Wakati mwingine hali hiyo inatokana na usimamizi mdogo, wakulima kuridhika na hali yao au maofisa ugani kushindwa kuwafikia kwenye maeneo yao na kuwapa elimu ya kutosha kuhusu umuhimu wa mbolea iwe ya kisasa au samadi au manyua.

Tunatoa wito maofisa hawa watimize wajibu wao ili kilimo na ufugaji viwe na tija maana kadri kilimo kinavyokuwa cha kisasa, ndivyo vijana wengi zaidi watavutika kushiriki badala ya kukimbilia mijini kufanya kazi za kijungu jiko.

Wito wetu mwingine ni masoko ya mazao. Upo ushahidi kwamba katika baadhi ya maeneo wakulima hukumbana na tatizo la uhaba wa masoko ya mazao yao. Mfano katika miaka ya hivi karibuni kulikuwa na tatizo la soko la korosho na hivi sasa soko la mbaazi.

Ili kuondokana na tatizo la soko tunadhani hata viwanda vinavyojengwa nchini viwe ni vile vitakavyotumia malighafi inayopatikana nchini kama vile mazao ya wakulima au bidhaa za uvuvi na ufugaji. Tunatoa wito kwa mawaziri wa wizara hizo kwamba kazi iwe kuhamasisha kilimo, uvuvi, ufugaji wa kisasa

-->