Kazi ya Kijiji cha Uturo ni mfano wa kuigwa

Wananchi wa Kijiji cha Uturo wilayani Mbalali, Mbeya wakiwa wamepumzika baada ya kazi za kijamii. Picha na Syriacus Buguzi

Muktasari:

Katika makala hayo, viongozi wa kijiji hicho kilicho wilayani Mbarali wanazungumzia hatua mbalimbali zilizowafanya waweze kuzuia vifo vya wajawazito kwa miaka 18.

Katika toleo la jana la gazeti la Mwananchi, ukurasa wa 30 kulikuwa na makala maalumu inayozungumzia jinsi Kijiji cha Uturko kilichoko mkoani Mbeya kilivyodhibiti vifo vya wajawazito.

Katika makala hayo, viongozi wa kijiji hicho kilicho wilayani Mbarali wanazungumzia hatua mbalimbali zilizowafanya waweze kuzuia vifo vya wajawazito kwa miaka 18.

Miongoni mwa hatua hizo ni pamoja na kuunda kikundi maalumu cha kuratibu mpango huo kinachoundwa na watu wanaoitwa makomando. Kazi ya kikundi hicho ni kutafuta taarifa za kila mwanamke anayepata ujauzito na kujua kama anahuhudhuria kliniki.

Na kama mjamzito akigundulika ana kiashiria chochote cha hatari, zahanati hufanya uamuzi wa ama kutatua tatizo lake na kama ikishindikana basi apelekwe hospitali ya wilaya kwa matibabu zaidi.

Pia kikundi hicho hufanya kazi ya kuelimisha jamii ya kijijini hapo kuhusu umuhimu wa kupima na pia manesi wa zahanati ya kijijini hapo kufanya kazi kwa karibu na kamati za afya na hivyo kutokuwepo na msuguano wa kikazi.

Huduma nyingine hutakiwa kutolewa hospitali ya wilaya, lakini barabara ya kuelekea kwenye hospitali hiyo si nzuri. Wanakijiji hao wameona pia umuhimu wa kujitolea nguvu zao kutengeneza barabara hiyo, japo kwa vifaa walivyonavyo ili wagonjwa wao wapite bila ya matatizo.

Wanakijiji hao walijitolea matrekta madogo, majembe, chepeo, ndoo na vifaa vingine kwa ajili ya ukarabati wa eneo hilo la barabara ili kurahisisha kazi ya kusafirisha wagonjwa kutoka kijijini kwenda hospitali ya wilaya.

Juhudi hizo zilianzishwa na mganga mfawidhi wa zahanati ya kijijini hapo, ambaye wakati anafika kijijini hapo, alikuta vifo vya wajawazito vikiwa ni jambo la kawaida.

Hakukuwepo na takwimu sahihi za vifo hivyo lakini katika kuhesabu makaburi, walibaini kuwa kila kaburi la mjamzito ilimaanisha kifo cha mama na mtoto na walipohesabu walikuta vifo vitano vya wajawazito kwa mwaka na vifo 30 vya watoto.

Hapo ndipo walipoona haja ya kuanzisha mkakati wa kupunguza vifo hivyo hadi walipofanikiwa kudhibiti kwa miaka 18.

Bila shaka huu ni mfano wa juhudi binafsi za kijiji unaofaa kuigwa na sehemu nyingine. Ni dhahiri kwamba Serikali ina jukumu la kuhakikisha wananchi wanakuwa na huduma bora za afya, lakini pia wananchi nao wana wajibu wa kushirikiana na Serikali yao kupata huduma hizo.

Kwa nchi maskini kama Tanzania, uwezo wa Serikali kukifikia kila kijiji na kutoa huduma stahiki za afya bado ni mdogo, hivyo kunahitajika ubunifu wa viongozi na jitihada binafsi za wananchi kutumia kile wanachoweza kuhakikisha wanapata huduma muhimu wakati wakisubiri juhudi za Serikali.

Suala la kuhamasisha wajawazito kuhudhuria kliniki, halihitaji fedha bali wachache wenye elimu hiyo kutengenezewa mazingira ya kuwafikia wengi na pia kuwafanya wananchi waone umuhimu wa kile wanachoelezwa.

Na katika miundombinu, wananchi wa Uturo wameonyesha kuwa pale wanapoweza boresha miundombinu, wanafanya hivyo kwa kutuumia kila kifaa walichonacho.

Viongozi wengine wa vijiji hawana budi kuiga mfano huu ili kuinusuru jamii na vifo vinavyozuilika.