Thursday, June 15, 2017

Kigoda cha Mwalimu kiwe chachu ya maendeleo

By Mwananchi

Kongamano la Tisa la Kigoda cha Mwalimu Nyerere lililoanza juzi kwenye ukumbi wa Nkrumah Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, linamalizika leo na mada kuu ikiwa “Nafasi ya Wanasiasa Katika Kuinuka na Kuanguka kwa Maendeleo ya Bara la Afrika”.

Wakati akichangia mada katika siku ya kwanza ya kongamano hilo, mwanakigoda wa mwaka huu, Profesa Abdoulaye Bathily wa Senegal alisema bila kupepesa macho kwamba Afrika imekosa viongozi wenye mtazamo chanya kwa ajili ya maendeleo ya bara hili.

Tanzania ni mojawapo wa nchi ambazo, kama Profesa Bathily alivyosema, zimepata uhuru zaidi ya miaka 50 iliyopita lakini hadi sasa bado ni masikini licha ya kuwa na maliasili nyingi kama madini.

Katika maelezo yake, Profesa Bathily anawalaumu zaidi viongozi waliopokea vijiti kutoka kwa waasisi ambao walijitoa kwa hali na mali kupigania uhuru wa wananchi zao.

Tunakubaliana na Profesa Bathily kwamba wabia kutoka nje hawawezi kuwaletea maendeleo Waafrika, ndiyo maana Afrika inaendelea kuwa bara la kuzalisha malighafi na soko la bidhaa zinazozalishwa kwingine.

Kwa Tanzania, tatizo mojawapo ni kutokamilika kwa mchakato wa kuandika Katiba mpya ambayo ni mwongozo kwa viongozi wetu katika masuala ya kiuchumi, kisiasa na kijamii ili iendane na dunia ya sasa.

Wanasiasa wa Tanzania, hasa kutoka upinzani, wamekuwa na malalamiko mengi kama ya Rais kupewa mamlaka makubwa na Katiba, kama ilivyo kwa mawaziri katika kusaini mikataba ambayo hivi sasa inapigiwa kelele.

Pia, kumekuwa na malalamiko ya madaraka makubwa ya wakuu wa mikoa na wilaya kiasi cha mambo mengi katika maeneo yao ya kiutawala kupelekwa kisiasa zaidi.

Tunadhani mada kuu kwenye kongamano la Kigoda cha Mwalimu Nyerere inapaswa kutukumbusha kuepuka hayo na mengine mengi yanayosumbua nchi. Taifa linahitaji Katiba mpya itakayotoa mwongozo chanya kwa viongozi wetu na hata kuwabana wale wenye tamaa.

Kinachofanywa na Rais John Magufuli sasa ni juhudi binafsi, lakini kama kungekuwa na Katiba imara inayodhibiti na kuwajibisha viongozi, nchi isingefika hapa ilipo na hivyo Rais asingekuwa na kazi hiyo ngumu.

Tunaamini kwa Katiba imara, wasaidizi wa Rais wangewajibika kwa wananchi kuwa kuwa wangepitia mchujo unaofanywa na Bunge kwa njia ya uwazi na hivyo mfumo kuwalazimisha kufanya kazi kwa maadili na weledi.

Hivyo, kongamano kama hilo la kigoda cha Mwalimu Nyerere, halitakiwi kuwa jukwaa la kisiasa la watu kueleza fikra zao na kuondoka, bali kuchukulia kwa uzito yanayojadiliwa na wahusika kuyafanyia kazi.

Uendeshaji nchi na maendeleo ya kiuchumi unatakiwa uakisi mijadala inayotawala kongamano hilo na hivyo washiriki kutoka nje waone kuwa Tanzania inaishi falsafa za Mwalimu Nyerere ambaye alibadilika kulingana na mazingira yalivyotaka.

Tunawapongeza waandaaji wa Kigoda cha Mwalimu Nyerere kwa kufanya jitihada za kuendeleza fikra za muasisi huyo wa Taifa la Tanzania kwa kuandaa mijadala ambayo inawapa nafasi wale waliopewa dhamana ya kuongoza nchi, kutathmini mwenendo wao katika utendaji kulinganisha na msimamo na falsafa hizo.

-->