Kilichojiri katika Bunge la Bajeti tafakuri kubwa

Muktasari:

  • Ulikuwa ni mkutano ulioshuhudia wabunge wa CCM kutoka mikoa ya kusini wakiungana na wale wa upinzani kuibana Serikali juu ya fedha za mauzo ya korosho ghafi nje ya nchi.

Unaweza kusema yaliyopita si ndwele tugange yajayo. Tayari utekelezaji wa Bajeti ya mwaka 2018/19 umeanza Julai Mosi baada ya mjadala mzito na vuta vikute katika mkutano wa Bunge la Bajeti.

Ulikuwa ni mkutano ulioshuhudia wabunge wa CCM kutoka mikoa ya kusini wakiungana na wale wa upinzani kuibana Serikali juu ya fedha za mauzo ya korosho ghafi nje ya nchi.

Muungano huo uliwaweka katika wakati mgumu mawaziri na Serikali kwa ujumla baada ya wabunge kuwabana vilivyo mawaziri, ingawa vilevile baadaye haikushangaza pale bajeti hiyo ilipopita kwa kishindo.

Ndio kisa baadaye zikaibuka kauli zinazofikirisha. Mfano, ile kauli ya Rais John Magufuli baada ya Bunge na ile ya Mbunge wa Mtera (CCM), Livingstone Lusinde ‘Kibajaji’ wakati wa mjadala, unaweza kujiuliza iwapo ule muungano wa wabunge katika mkutano huo utajitokeza tena siku zijazo.

Kauli hizo mbili kwa nyakati tofauti zilionekana kama kuwabana wabunge wa CCM kukikisoa chama hicho ndani ya Bunge.

Kibajaji akitumia nafasi yake ya mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM (NEC) akitamka waziwazi kuwa anawapiga marufuku wabunge wenzake kukikosoa chama ndani ya Bunge.

“Humu ndani (bungeni) tunapochangia tujiepushe na kazi za wengine. Eti tukifanya hivi tutashindwa sisi si wasemaji wa chama,” alisema Lusinde na kuongeza:

“Sisi wabunge wa CCM kazi yetu ni kuisimamia Serikali, kuikosoa na kuitetea. Nasema kama bosi wenu humu ndani, natoa marufuku kwa mbunge wa CCM kukizungumzia chama humu.”

Lusinde alisema, “hiki ni chama chenye Serikali, kuisimamia si kukikosoa chama.”

Anaongeza, “Kuweza sisi kushinda au kutokushinda si sehemu yake. Kama wabunge wangu hamna lugha ya kumsifia Rais au kuikosa Serikali, tulieni.”

Kauli ya Lusinde inaongezwa nguvu na ile ya Rais Magufuli ambaye aligusia kuwachukulia hatua wabunge wa mikoa ya kusini anakotoka pia Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, waliopinga mapendekezo ya Serikali kuhusu suala la korosho. Kauli hiyo ya Lusinde inaibua maswali hasa ikilinganishwa na ile ya Katibu Mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally, kuwa wabunge wa CCM ni ruksa kuikosoa Serikali.

Julai 2, baada ya kuwaapisha mawaziri na naibu katibu wakuu aliowateua Julai 1, Rais Magufuli alimweleza Majaliwa na Katibu Mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally kuwa alipanga kuwatimua wabunge hao kama wangegomea mapendekezo hayo.

Hata hivyo, mkazi wa Tabata jijini Dar es Salaam, Frank Samson anasema kwamba kauli hizo za Lusinde na Rais Magufuli zinakwenda kuwafanya wabunge wa chama tawala kuwa wakimya.

“Ujue hata kama ni wewe, bosi wako anapozungumza kuwa kitu ulichofanya kingeweza kukugharimu sidhani kama unaweza kurudia tena kukifanya. Kwa hiyo, sina hakika kama lilivyokuwa Bunge la Bajeti litakuja kujitokeza tena. Wabunge wa CCM watakuwa waoga zaidi,” anasema Samson.

Hali hiyo pia inazungumziwa na Mbunge wa Konde (CUF), Khatib Said Haji kuwa, “muungano ulioonyeshwa na wabunge wa mikoa ya kusini na wengine wanaotoka nje ya mikoa hiyo ni afya kwa Bunge kwani inaonyesha jinsi masilahi ya wananchi yalivyopiganiwa.”

“Kunapokuwa na jambo linalowahusu wananchi, tunapaswa kuungana na kuweka kando tofauti za vyama vyetu, hili la korosho lilionyesha mfano jinsi tulivyoungana kuhakikisha kilio cha wananchi kinasikika.”

Hata hivyo, Khatib anatofautiana na Mbunge wa Mbinga (CCM), Sixtus Mapunda anayesema, “Bunge liliungana kwa agenda za wananchi ni jambo zuri lakini ukiona wabunge wa upinzani wanaungana na wale wa CCM ujue wana ajenda yao binafsi.”

Mapunda aliyepata kuwa katibu mkuu wa Umoja wa Vijana wa CCM, anasema muungano wa aina hiyo mara nyingi huwa haudumu, kwa hiyo kilichojitokeza ilikuwa ni kwa sababu ya korosho. Lakini kwa upande wake, Mbunge wa Momba (Chadema), David Silinde anasema, “kauli ya Rais ni kitisho dhidi ya demokrasia ya wananchi wa kusini na sasa ni kwamba wabunge hawana haki ya kutetea wananchi wao bali wanapaswa kutetea maslahi ya Serikali.”

Silinde ambaye ni katibu wa wabunge wa Chadema, anasema moja ya majukumu ya wabunge ni kuisimamia Serikali na pindi maslahi ya wananchi yanapoonekana kutoweka wabunge ndiyo huwatetea.“Wabunge wengi ni wa CCM lakini hilo haliondoi dhana ya kuwatetea kama kuna jambo lina kikwazo kwa wananchi lazima kuisimamia Serikali lakini kwa sasa wabunge wa CCM hawana kauli yoyote dhidi ya serikali yao.”

Inawezekana CCM ina hoja muhimu juu ya namna ya kufanikiwa katika uongozi, lakini suala la uwakilishi ni pana, linahitaji pia kuwasikiliza zaidi wawakilishi wa wananchi. Kwa maana hii naamini mbele ya safari wataachwa wasimame kwa miguu miwili katika majukumu yao. 0716 386 168