Kiswahili kinazidi kukua tukithamini

Muktasari:

  • Kwa sasa Afrika Mashariki inaunganishwa na nchi wanachama ambao ni pamaoja na Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi na Sudan Kusini. Nchi hizi zina makabila mbalimbali kwa mfano Tanzania ina zaidi ya makabila 120, Kenya makabila zaidi ya 40 na hali kadhalika nchi nyingine wanachama zilizobakia zina makabila yao pia.

Lugha yoyote inakua na kuenea pale inapokuwa na watumiaji, nara nyingi inaweza kusambazwa kwa watu wengine kwa sababu ya mwingiliano unaotokana na shughuli za kijamii au kiuchumi. Leo katika safu hii nitaizungumzia lugha adhimu ya Kiswahili inayokua na kuenea zaidi duniani ikiwa na asili ya Pwani ya Afrika Mashariki.

Kwa sasa Afrika Mashariki inaunganishwa na nchi wanachama ambao ni pamaoja na Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi na Sudan Kusini. Nchi hizi zina makabila mbalimbali kwa mfano Tanzania ina zaidi ya makabila 120, Kenya makabila zaidi ya 40 na hali kadhalika nchi nyingine wanachama zilizobakia zina makabila yao pia.

Licha ya ukweli kwamba lugha hiyo ndiyo lugha pekee kwa Tanzania iliyofanikiwa kuunganisha makabila yote bila kuhitaji lugha nyingine, binafasi naitaza lugha hii na uimara wake umesababishwa na kutochangiwa na lugha nyingine yoyote ya asili iliyopo nchini.

Mbali na kuenezwa na shughuli za kijamii na kiuchumi, lugha hiyo ya Kiafrika yenye wazungumzaji wengi imetengenezewa taasisi kwa ajili ya kuikuza na kuieneza. Hapa Tanzania kuna vyombo vingi vinavyofanya kazi ya kukuza na kueneza lugha ya Kiswahili. Pamoja na majukumu mengine, vyombo hivyo vina jukumu la kuhakikisha lugha hiyo inapata wazungumzaji wengi.

Hivyo imefika wakati hata kwa upande wa taasisi za kiserikali na zile zisizo za kiserikali kukifanya Kiswahili kuwa lugha rasmi katika shughuli zao zote. Licha ya kuwa na vyombo vinavyosaidia kuikuza lugha hii ikiwamo Taasisi ya Taaluma za Kiswahili, Baraza la Kiswahili Tanzania, Usanifu wa Kiswahili na Ushairi Tanzania na Umoja wa Waandishi wa Vitabu Tanzania, lakini bado kuna baadhi ya watu wanakwamisha usanifu wao kwa kutaka lugha za nje ndizo zitumike kama lugha rasmi katika shughuli na maandiko mbalimbali wayachapishayo, jambo ambalo binafsi naona tunajirudisha nyuma. Nasema hivyo kwa sababu pamoja na kuanzishwa kwa vyombo hivyo miaka ya 1960, kazi zao zimekuwa zikikwamishwa na teknolojia duni ya habari na mawasiliano. Machapisho yao mengi yako kwenye vitabu, jambo linalochelewesha lugha hiyo kwenda mbali zaidi.

Lakini baada ya baadhi ya wadau kubaini mkwamo huo, hivi karibuni mitandao ya kijamii imejitosa na sasa imeanza kukitambua Kiswahili kama moja ya lugha ambazo zinaweza kutumika kwa mawasiliano. Kama inavyofahamika, mitandao ya kijamii inatumiwa na watu wengi, hivyo ikitumika ipasavyo itasaidia kuikuza lugha hii. Rekodi ya Kiswahili mitandaoni ilianza kuwekwa na mtandao wa Facebook baada ya kuamua kukitumia Kiswahili kwenye orodha ya lugha zitakazotumika, hali inayotoa fursa kwa watumiaji wake kuitumia lugha hiyo ipasavyo.

Wataalamu wa lugha wanatuambia hivi sasa hakuna lugha iliyo bora kuliko nyingine kwa sababu zote zinafanya kazi moja kama chombo cha mawasiliano. Tofauti zinazojitokeza ni mawanda ya kuenea kwa lugha yenyewe na wingi wa misamiati yake. Utafiti unaonyesha tayari baadhi ya mitandao ya simu hapa nchini imeanza kuwawezesha wateja wao kutumia facebook kwa lugha ya Kiswahili na wiki chache zilizopita mtandao wa kijamii wa Twitter nao umekitambua rasmi Kiswahili kama lugha mojawapo itakayotumika kwenye mtandao huo, jambo ambalo binafsi naliona ni kubwa kwa watumiaji wa lugha hii inayozungumzwa zaidi kwenye ukanda wetu huu wa Afrika Mashariki.

Hivyo tuna kila sababu kama Watanzania kuisambaza kwa nguvu zote lugha hii ndani ya nchi na nje, lakini pia kuipeleka kwa nchi nyingine za Afrika na duniani kwa sababu kubwa moja, Afrika Mashariki ndiko nyumbani kwa lugha hii ya Kiswahili na wataalamu waliobobea kwenye lugha hiyo wanatoka nchi za Afrika Mashariki.

Mwandishi ni mhariri wa jarida la afya ndani ya Gazeti la Mwananchi. 0713-235309.

Lakini Pia, inafundishwa katika vyuo vikuu mbalimbali duniani ambavyo ni pamoja na vya Marekani, Ujerumani, Uingereza, Japan na Korea Kusini.

Sambamba na kufundishwa vyuo vikuu, lugha hiyo pia hutumika katika vyombo mbalimbali vya habari katika mataifa makubwa kama ya Ujerumani, Uingereza, Japan, Ufaransa na Urusi. Hivyo, hakuna ubishi kwamba Kiswahili ni fahari yetu ya Afrika.

Tuungane kwa pamoja kuikuza lugha yetu hii ya Kiswahili ndani na nje ya nchi huku tukilenga pia kupanua ajira kwa wananchi kupitia ufundishaji wa lugha hiyo adhimu ya Afrika katika nchi mbalimbali duniani. Tusiwe watazamaji katika ajira zinazotokana na lugha ya Kiswahili, bali tuwe hasa watendaji wa kutolewa mfano katika utekelezaji na usambazaji.