Kiwanda cha kokoto kinahitajika mikoa ya Nyanda za Juu Kusini

Muktasari:

Kiwanda cha kutengeneza kokoto cha Kongoro kilichopo eneo la Mswiswi wilayani Mbarali kinachomilikiwa na Mamlaka ya Reli ya Tanzania na Zambia (Tazara), ni tegemeo kubwa la uzalishaji wa kokoto maarufu kwa jina la CNR ambazo zinawekwa kabla na baada ya kumwaga lami.

Miradi ya ujenzi wa barabara za lami katika mikoa ya Nyanda za Juu Kusini iko shakani kukamilika ama kujengwa kwa ubora hususan mjini Mbeya, kutokana na kukosekana kwa kokoto zinazotumika kuchanganya na lami.

Kiwanda cha kutengeneza kokoto cha Kongoro kilichopo eneo la Mswiswi wilayani Mbarali kinachomilikiwa na Mamlaka ya Reli ya Tanzania na Zambia (Tazara), ni tegemeo kubwa la uzalishaji wa kokoto maarufu kwa jina la CNR ambazo zinawekwa kabla na baada ya kumwaga lami.

Lakini kiwanda hicho kwa sasa hakina uwezo wa kuzalisha kokoto hizo.

Miongoni mwa barabara ambazo zimekwama kwa zaidi ya miezi mitatu katika Jiji la Mbeya ni ile ya Isyenye inayoanzia Maduka saba hadi Kilimo yenye urefu wa kilomita 2.5 na nyingine ya karibu na ile ya Uwanja wa Sokoine yenye urefu wa nusu kilomita.

Kukwama kwa barabara hizo tangu mwezi Machi ni kero kubwa kwa wakazi wa eneo hilo, kutokana na kuwapo kwa vumbi jinsi huku mamlaka husika wakishindwa kumwagilia maji.

Hali kadhalika kukwama kwa barabara hizo kunasababisha hasara kwa Serikali ambapo italazimika kuongeza fedha ili kukamilisha miradi hiyo.

Taarifa kutoka mikoa ya Njombe, Iringa na Songwe zinasema kwamba uhaba wa kokoto aina ya CNR umekwamisha ujenzi wa miradi kadhaa na hivyo hatua za dharura zinahitajika ili kazi iweze kuendelea.

Mmiliki wa kampuni ya Global Link inayojenga barabara ya Uwanja wa Sokoine, Baltazar Malamsha anasema amelazimika kununua kokoto hizo kutoka Goba mkoani Pwani na kuzisafirisha hadi Mbeya.

Naye Meneja wa Tarura katika Jiji la Mbeya, Alberto Kindole anasema ukosefu wa kokoto umekwamisha ujenzi wa barabara za lami katika jiji hilo.

Lakini Kaimu Meneja wa kiwanda cha kutengeneza kokoto cha Kongoro Mswiswi wilayani Mbarali, Musa Kalala anasema kiwanda chake kipo kwa ajili ya kutengeneza kokoto za Tazara na siyo za ujenzi wa barabara.

Kalala anasema kokoto za kuweka kwenye reli zipo nyingi, ingawa anakiri kwamba mtambo unaotoa kokoto za CNR umeharibika.

Tayari kiwanda hicho kimeandika barua za kuarifu tatizo hilo wateja wanaonunua kokoto kutoka hapo.

Naye Kaimu Meneja uzalishaji wa kiwanda hicho, Athanas Malimi anasema uzalishaji umeporomoka kutoka tani 500 kwa wiki hadi chini ya tani 100.

Kwa hali hii, tatizo ni kubwa na ni fursa kwa wenye uwezo wa kuwekeza mitambo ya kutengeneza kokoto za aina hiyo katika mikoa ya Nyanda za Juu Kusini.

Mikoa ya Iringa, Ruvuma, Njombe, Mbeya, Songwe, Rukwa na hata Katavi ina miradi mingi ya ujenzi wa barabara ambayo inahitaji kokoto.

Kwa mfano, zipo taarifa kwamba barabara kuu ya Dar es Salaam kwenda Zambia inaweza kuanza kujengwa kuanzia Igawa mkoani Mbeya hadi Tunduma huko Songwe, jambo ambalo litahitaji kokoto nyingi.

Hali kadhalika barabara ya kutoka Chunya mjini hadi Makongorosi itahitaji kokoto na hata ujenzi wa barabara ya kutoka Tukuyu kupitia Mwakaleli hadi Lwangwa utahitaji kokoto.

Kwa hali hiyo, Watanzania wenye mitambo ya kutengeneza kokoto wanayo fursa kubwa ya kuwekeza katika mikoa hii.

Mpango wa uwekezaji katika uzalishaji wa kokoto utakuwa na manufaa makubwa kwa wananchi na miradi mbalimbali inayohitaji kokoto kwa ajili ya utekelezwaji wake.

Ni vyema wawekezaji wakashauriwa kuwekeza katika uzalishaji wa kokoto ili kuwezesha shughuli za kiuchumi kufanyika kwa wakati badala ya kuendelea kusuasua katika utekelezwaji wake.

Mwandishi ni mdau wa maendeleo mkoani Mbeya