Mliobahatika kupata mafunzo ya ujasiriamali chapeni kazi

Muktasari:

Elimu hii inamsaidia kijana kuwa mbunifu wa jambo gani alifanye la kiabiashara litakaloweza kumuingizia kipato.

Kati ya vitu vinavyowasumbua vijana katika kujikwamua kimaisha ni pamoja na kukosa elimu ya ujasiriamali.

Elimu hii inamsaidia kijana kuwa mbunifu wa jambo gani alifanye la kiabiashara litakaloweza kumuingizia kipato.

Jambo hilo linaweza kuwa katika sekta yoyote ikiwamo kilimo, uvuvi, teknolojia na sekta nyinginezo.

Kama mnavyojua Tanzania imejaliwa kuwa na rasilimali za kutosha ambazo kama vijana watachangamsha bongo zao ni wazi kwamba wataondokana na tabia ya kubaki kulalama vijiweni na kuchapa kazi zitakazomnufaisha yeye mwenyewe pamoja na familia yake kwa ujumla.

Hivi karibuni nilibahatika kutembelea mikoa mitano, katika ziara hiyo nilijionea namna mradi wa kuwawezesha vijana kiuchumi unaojulikana kwa jina la YEE, ulivyotekelezwa ambapo takribani vijana 10,280, wamefikiwa.

Mikoa iliyonufaika na mradi huo ni pamoja na Morogoro, Pwani, Mtwara, Lindi na Dar es Salaam, huku wilaya 10 katika mikoa hiyo zikishirikishwa.

Ili kushiriki katika mradi huu ilimpasa mhusika kujaza fomu maalumu katika ofisi ya mtendaji kata na hakika vijana wengi waliitikia wito.

Hata hivyo, kama unavyojua kwenye msafara wa mamba na kenge wapo, wako waliojitokeza kwa ajili ya kwenda kuuza sura na wapo waliojitokeza wakiwa na nia kweli ya kujikwamua kutoka hapo walipo na hao waliokuwa na nia ya dhati wameona matunda ya ujio wa mradi huo.

Katika mradi huo ambao uliwalenga zaidi vijana wanaotoka katika mazingira magumu, mbali ya mafunzo, wahitimu walisaidiwa kuunda vikundi vya watu wasiopungua watano na kukabidhiwa vifaa vya kuanza kufanyia kazi kulingana na fani waliyosomea.

Hiki ni moja ya kitu kilichovutia, kwani yapo mashirika mengi yanayotoa elimu kwa vijana lakini matunda yake hayaonekani kutokana na wengi wao kutokuwa na vitendea kazi vya kufanya yale waliofundishwa.

Mkurugenzi wa mafunzo mafupi kutoka Chuo cha Mafunzo ya Ufundi (Veta), mkoani Morogoro, Christopher Magwai anasema kitaalamu mtu anaposomea mafunzo ya ufundi na baada ya hapo akakaa muda mrefu bila kuyafanyia kazi, kuna uwezekano wa kusahau.

Ndiyo maana Veta, wanafunzi husoma darasani kidogo huku masomo ya vitendo yakiwa yanachukua muda mwingi zaidi.

Kwa mantiki hiyo, ilichofanya YEE ni cha kuigwa na wadau wengine kama kweli tumedhamiria kuwakomboa vijana.

Nimesikitika kuona baadhi ya vijana wa hususan mikoa ya Lindi na Mtwara, kufungia ndani vifaa walivyopewa na kuendelea na shughuli zao nyingine.

Baadhi ya vifaa ni vile vya umeme ambavyo kama havitatumiwa muda mrefu kuna hatari ya kuharibika na kushindwa kufanya kazi.

Ifike mahali vijana wanapopewa nafasi wazitumie na kuacha kubaki kulalama kuwa hakuna ajira wakati wanapata fursa na kuzichezea.

Katika mradi huu, Serikali kupitia halmashauri zake zimekuwa zikitoa mikopo kwa wale ambao hawana pa kuanzia. Je, vijana wa Mtwara na Lindi hapo mnataka mbebwe na mbeleko gani.

Ni vyema vijana hao wakajitathmini na kama wamepata kazi nyingine zinazowaingizia fedha, basi warushe vifaa walivyopewa ili wengine wakavifanyie kazi.

Ni vyema wale wenye nia wakapewa usaidizi na kuwezeshwa kutumiza ndoto zao. Mathalan, wapo walioanza kwenye kikundi cha vijana 12 lakini wakajikuta baadaye wanabaki wawili na bado hawakukata tamaa.

Naishauri Serikali na wadau kwamba ni vyema wakaendelea kuwafuatilia vijana wenye moyo huo na ikiwezekana wawaongezee vitendea kazi na fedha ili kampeni Tanzania ya viwanda itekelezeke kwa kushirikisha kundi hilo ambalo kwa idadi ni wengi na kama watawezeshwa vizuri wataiinua nchi kiuchumi.

Kwenu Maofisa Vijana ni muda sasa wa kuacha tabia ya kukaa ofisini na kuwafuata vijana hawa huko walipo kujua changamoto zinazowakabili na nini muwasaidie, kwani ajira zenu zimetokana na nyie.

Msiwasubiri kila wakati wawafute nyie, kwani kuna baadhi wanafanya vizuri lakini hawajui wafanye nini ili wakue katika biashara na kazi zao, msaada wenu unahitajika hata wa ushauri.

Shirika la Plan International ambalo ndilo lilikuwa msimamizi Mkuu wa mradi huu likishirikiana na wadau wengine, msisite kuendelea kutoa huduma kama hizo kwa vijana, kwani kwa hali niliyojionea bado vijana wengi wanahitaji mafunzo ambayo mmekuwa mkitoa na pia ni wakati wa kufika na mikoa minginekwa kuwa mliyofika tayri wana uwezo wa kusambaza ujuzi huo kwa wengine.