NEC itoe elimu kwa wagombea, matatizo ya fomu yasijirudie

Muktasari:

NEC ndiyo yenye mamlaka ya kusimamia uchaguzi ikiwamo kutoa elimu kwa wapigakura, wagombea wa nafasi mbalimbali za uongozi na kusimamia kwa haki mchakato wa kuhesabu kura za wagombea hadi matokeo.

Watanzania kwa mara nyingine ndani ya kipindi cha zaidi ya miaka miwili wanaingia kwenye uchaguzi mdogo wa nne. Uchaguzi huo unafanyika baada ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kutangaza kata 77 na jimbo moja la ubunge ziko wazi kutokana na sababu mbalimbali.

NEC ndiyo yenye mamlaka ya kusimamia uchaguzi ikiwamo kutoa elimu kwa wapigakura, wagombea wa nafasi mbalimbali za uongozi na kusimamia kwa haki mchakato wa kuhesabu kura za wagombea hadi matokeo.

Lakini, kwa takriban miaka 26 tangu Tanzania iliporejea kwenye mfumo wa vyama vingi vya siasa, uzoefu unaonyesha kuwa kwenye chaguzi nyingi baadhi ya wagombea hasa wa upinzani wamekuwa wakishindwa kukidhi vigezo na masharti hivyo kuenguliwa kwenye nafasi za kugombea.

Mfano, baadhi ya kasoro ambazo zimekuwa zikiwatupa nje ya ulingo wagombea wengi kutoka vyama vya upinzani ni kushindwa kujaza vyema fomu. Mathalani, kukosekana kwa mhuri au mhuri kugongwa na mtu asiyehusika, kukosekana kwa saini ya mmoja wa wadhamini na jina kukosewa.

Kinachoshangaza tatizo hili linawakumba zaidi wagombea wa upinzani kuliko wenzao wanaotoka CCM, kila unapoitishwa uchaguzi mdogo au hata Uchaguzi Mkuu mara nyingi fomu za kuomba uteuzi kutoka kwa wagombea wa upinzani huwa na kasoro na mara kadhaa na mwishowe kutolewa kwenye nafasi wanazogombea.

Sheria ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Sura ya 292 na Maelekezo ya Tume, vimeweka wazi kwamba ili mtu aweze kuteuliwa kuwa mgombea hana budi awe ametimiza masharti ya kudhaminiwa na wapigakura wasiopungua 10 walioandikishwa kupiga kura katika kata anayogombea, awe ametoa tamko la kisheria mbele ya Hakimu kuthibitisha kuwa anazo sifa za kugombea.

Sifa nyingine ni ile inayomtaka kuweka dhamana ya Sh5,000 kwa msimamizi wa uchaguzi, awe hajatenda vitendo vilivyokatazwa kwa mujibu wa Sheria ya Gharama za Uchaguzi ya 2010, awe amejaza fomu zinazohitajika za uteuzi ambazo ni Fomu Na. 8C na Fomu Na. 10 ya kukubali kutekeleza Maadili ya Uchaguzi na awe amewasilisha picha nne za rangi zenye ukubwa wa pasipoti.

Tunajiuliza kwa nini kwa miaka 26 ya mfumo wa vyama vingi vya siasa, wapinzani bado hawajaelewa namna ya kujaza fomu za kuomba uteuzi kutoka NEC? Je, lugha inayotumika kwenye fomu hizo ni ngumu kueleweka kwa wagombea hawa.

Maswali haya yanatokana na namna kasoro hizi zinavyoonekana kujirudia kila mchakato wa uchaguzi unapotangazwa na kuwafanya wagombea wa CCM kupita bila kupingwa.

Kwa kuwa moja ya jukumu la NEC ni kutoa elimu ya uchaguzi, tunaishauri kuangalia kipengele hiki cha ujazaji na urudishaji wa fomu ili kasoro hizi zisiwanyime wananchi fursa ya kuchagua viongozi wao baada ya kusikiliza mikakati na ahadi zao kwao na kisha kuwapima na kuwachagua kwa kura.

Hilo likifanikiwa, wagombea wote wakajaza vyema na kurejesha fomu zao na kushindana majukwaani, huko ndiko kukua kwa demokrasia ya mfumo wa vyama vingi vya siasa. Hatuwezi kujinadi kwamba tuna demokrasia ya mfumo wa vyama vingi vya siasa kama elimu ya namna ya kujaza fomu za kuiomba uteuzi haitasambaa na kueleweka kwa wote.

Rai yetu kwa wasimamizi wa uchaguzi ikiwamo NEC wafanyie kazi kasoro hizi kwa kutoa elimu kwa wagombea ili kuhakikisha wote wanapita hivyo kuwapa wananchi uhuru wa kuchagua viongozi wanaowataka na huko ndiko kukuza demokrasia ya vyama vingi vya siasa.