UCHAMBUZI: Namba ya simu yaweza kuwa akaunti ya benki ujue

Muktasari:

  • Enzi hizo laini pekee ilikuwa inauzwa mpaka Sh50,000 lakini kwa sasa hivi hali ni tofauti. Bei imeshuka sana na unaweza ukapata laini hata bure wakati simu za mkononi zikiuzwa kwa bei ya chini kiasi cha wengi kumudu.

Wakati simu za mkononi zinaingia nchini mwanzoni mwa miaka ya 1990 ilikuwa fahari kumiliki moja. Hata kuwa na laini peke yake ilitosha kukuweka kwenye daraja la juu.

Enzi hizo laini pekee ilikuwa inauzwa mpaka Sh50,000 lakini kwa sasa hivi hali ni tofauti. Bei imeshuka sana na unaweza ukapata laini hata bure wakati simu za mkononi zikiuzwa kwa bei ya chini kiasi cha wengi kumudu.

Si ajabu kwa sasa kukuta mtu anamiliki zaidi ya simu moja hasa maeneo ya mjini. Simu ni sehemu ya maisha. Wapo baadhi ya watu hawawezi kukaa nusu saa bila kushika simu.

Kutokana na wingi wa simu wapo wanaopenda kuwa na laini zinazofanana namba iwe kutoka mitandao tofauti hata ukiwa mmoja.

Wapo wanaopenda namba zao zifanane na za baadhi ya wapendwa wao. Teknolojia inaruhusu na hayo yote yanawezekana.

Kutokana na urahisi wa kutumia simu, huduma za fedha nazo zinatolewa kupitia huko. Kampuni saba za mawasiliano hivi sasa zinatoa huduma za fedha kupitia simu za mkononi.

Benki nyingi za biashara kama si zote zinaruhusu baadhi ya miamala kufanyika kupitia simu za mkononi. Watu wanaweza kuweka au kutoa fedha kwenye akaunti zao za benki bila haja ya kwenda kupanga foleni benki ili kufanya hivyo.

Kutokana na ubunifu unaoendelea, kuna jipya. Eti sasa hivi namba yako ya simu inaweza kuwa akaunti ya benki. Unaweza usiamini lakini Benki ya NMB inatoa huduma hiyo.

Baada ya kuzinduliwa mapema mwezi huu, benki hiyo inamruhusu mtu yeyote mwenye simu ya mkononi kufungua akaunti kwa kutumia kitambulisho alichonacho kufanikisha nia ya kuwa na akaunti.

Kwa mtu mwenye pasi ya kusafiria, kitambulisho cha Taifa au cha mpigakura anaweza kufungua akaunti hii kwa kufuata maelekezo maalumu baada ya kupiga namba zinazomruhusu kufanya hivyo.

Maelekezo hayo yanapatikana kwenye App ya benki hiyo pia. Kwa namna yoyote ambayo mteja ataamua kuitumia ataweza kufungua akaunti itakayolingana na namba yake ya simu ya mkononi.

Hili linawezekana muda wowote; usiku na mchana. Na jambo la kuvutia ni kwamba mteja anaweza kufanya hivyo akiwa mahali popote hivyo kuondokana na usumbufu wa kuwasilisha nyaraka kadhaa kwa ajili ya kufungua akaunti kwenye tawi lolote lililo jirani naye.

Kutokana na urahisi wa kutumia simu ya mkononi, hii ni fursa kwa wafanyabiashara wadogo kama mamalishe na wamachinga kumiliki akaunti ya benki.

Hili linawahusu wafanyakazi wa nyumbani na mashambani pia. Kwa mabosi wenye wasaidizi wa kazi mfano za ndani au bustani, hawana haja ya kuwalipa fedha taslimu mkononi.

Wanayo fursa ya kufungua akaunti wakawa wanawalipa kupitia huko jambo litakalosaidia kuondoa malalamiko yanayoibuka pindi mktaba unapovunjika na mfanyakazi akalalamika kuwa hajalipwa mshahara wake kwa miezi au miaka kadhaa.

Benki nyingine pamoja na taasisi za fedha zikirahisisha utaratibu wa kungua akaunti bila shaka wananchi wengi zaidi watakuwa nazo. Takwimu zilizopo zinaonyesha ni watu 17 tu katika kila 100 wana akaunti ya benki.

Hali hii pamoja na mambo mengine inachangiwa na utaratibumgumu unaohitaji uvumilivu kuukamilisha kabla mteja hajafanikiwa kufungua akaunti. Matumizi ya lugha pia ni suala jingine ambalo benki zinapaswa kulizingatia. Kiingereza kingi kinawakimbiza wateja.

Mwandishi anapatikana kwa namba 0759 354 122