Tuendelee kuisaidia Serikali kupunguza matumizi ya fedha za kigeni

Muktasari:

  • Hivi karibuni, Serikali kupitia Wizara ya Fedha ilikuja na mpango wa kudhibiti matumizi ya fedha za kigeni kwa lengo la kulinda thamani ya shilingi ya Tanzania.

Tangu Serikali ya Awamu ya Tano iingie madarakani mwishoni mwa 2015, imeendelea kuonyesha nia ya dhati ya kutaka kuinua uchumi wa nchi katika nyanja mbalimbali.

Hivi karibuni, Serikali kupitia Wizara ya Fedha ilikuja na mpango wa kudhibiti matumizi ya fedha za kigeni kwa lengo la kulinda thamani ya shilingi ya Tanzania.

Binafsi naona ni jambo jema na la muhimu litakalosaidia kuinua uchumi wa nchi na kuinua maisha yetu.

Desemba mwaka jana, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango alitoa maagizo yaliyohusu kupunguza matumizi ya fedha za kigeni.

Katika maagizo hayo ambayo alitaka utekelezaji wake uanze Januari Mosi, mwaka huu, aliagiza bei za bidhaa zote nchini ziuzwe kwa fedha ya Kitanzania badala ya zile za nje hususan dola ya Marekani.

Pia, alitaka uwazi katika viwango vya ubadilishaji wa fedha na kuondoa ulazima wa mtu kulazimishwa kulipa fedha za kigeni akiwa hapa nchini isipokuwa kwa huduma za kitalii ambazo aliziainisha.

Hatua hii inapaswa kuungwa mkono na Watanzania kwani nchi nyingi duniani ambazo zimepiga hatua kiuchumi na kuongeza thamani ya sarafu zao, katu haziruhusu matumizi ya fedha nyingine ila za kwao.

Hata maduka ya kubadilishia fedha yapo zaidi katika viwanja vya ndege, mipakani na kwenye benki zao.

Ningependa kuwakumbusha Watanzania wenzangu kuwa nchi hii si ya kwanza kuchukua hatua hiyo ya udhibiti wa matumizi ya fedha za kigeni, bali hata nchi za China, Afrika Kusini, Rwanda na nyinginezo nyingi matumizi ya fedha za kigeni ndani ya nchi zao hayakubaliki.

Na ili upate huduma mbalimbali za ununuzi ukiwa kwenye nchi hizo, ni sharti kwanza ubadilishe fedha ulizo nazo kuwa katika sarafu zao.

Tayari Serikali imetuonyesha njia, kazi yetu sisi wananchi ni kushirikiana nayo hasa katika masuala kama haya yenye masilahi mapana kwa Taifa letu la leo na kesho.

Nilitarajia kuona Watanzania hawamfumbii macho mtu ambaye anakiuka utaratibu huu kama ilivyozoeleka na badala yake ataripoti kwa vyombo vya dola ili vichuke hatua kama alivyoelekeza Waziri Mpango.

Lakini bado kuna baadhi ya maeneo dola zinaendelea kutumika kwa ajili ya manunuzi na huduma mbalimbali.

Kiuchumi, matumizi ya fedha za kigeni kwa shughuli za ndani mbali ya kudidimiza thamani ya shilingi, pia fedha nyingi hupotea katika biashara au ubadilishaji kwa sababu sarafu ya ndani hununua fedha za nje kwa kiwango kikubwa, lakini fedha hiyo hununua sarafu ya ndani kwa kiwango kidogo. Ikumbukwe kuwa thamani ya sarafu ya nchi ni miongoni mwa masuala muhimu yanayopaswa kutazamwa kwa umakini, kwa kuwa ni muhimu kwa mustakabali wa biashara, deni na pato la Taifa pamoja na wananchi.

Thamani ya shilingi ya Tanzania iko chini sana ikilinganishwa na fedha ambayo inatumika zaidi nchini yaani dola ya Marekani.

Shilingi yetu inaonekana kuporomoka na hata tofauti ya ubadilishaji wa sarafu hiyo na fedha nyingine za kigeni imekuwa ikiongezeka siku hadi siku.

Mfano 2006, dola moja ya Marekani ilikuwa inanunuliwa kwa Sh789, mwaka 2012 ilikuwa inanunuliwa kwa Sh1,600 na mwaka huu inanunuliwa kwa zaidi ya Sh2,240.

Kiwango cha kubadilisha fedha kinaposhuka maana yake sarafu yetu imeimarika na kinapoongezeka ni kinyume chake.

Lakini wataalamu wa uchumi wanatuambia thamani ya sarafu yetu itaongezeka zaidi kwa kuongeza mauzo ya bidhaa zetu nje ya nchi na kupunguza uagizaji wa bidhaa kutoka nje hususani zile zinazoweza kupatikana nchini.

Ni muhimu kama nchi kujitahidi kupunguza ununuzi wa bidhaa na huduma kutoka nje ambazo zinapatikana nchini.

Hii itasaidia kuepuka kushuka kwa thamani ya sarafu yetu.

Tunapaswa kuongeza uzalishaji na usafirishaji wa bidhaa za madini, pamba, korosho na kuendelea kuutangaza utalii na huduma zake zaidi ya tufanyavyo sasa.

Ununuzi wa bidhaa nyingi nje ya nchi hupunguza akiba ya fedha za kigeni, huathiri soko la fedha kama ilivyo kwa bidhaa na huduma nyingine zo.

Hivyo thamani ya shilingi hushuka kwa sababu kunahitajika shilingi nyingi ili ipatikane dola moja ya Marekani.

Hebu tubadilike, tuache kutukuza fedha za wenzetu na kudharu ya kwetu.

0713235309