Umefika wakati sasa sheria hii itazamwe upya

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Selemani Jafo.

Muktasari:

  • Jafo alikuwa akizungumzia matumizi ya Sheria ya Tawala za Mikoa Sura ya 97 inayozungumzia mamlaka ya wakuu wa mikoa na wilaya ya kuwaweka mahabusu watu wanaoonekana wanaweza kuhatarisha amani na utulivu iwapo watakuwa huru kwa kipindi fulani.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Selemani Jafo amekemea tabia ya baadhi ya wakuu wa wilaya kutumia vibaya mamlaka waliyonayo ya kuwaweka watu mahabusu.

Jafo alikuwa akizungumzia matumizi ya Sheria ya Tawala za Mikoa Sura ya 97 inayozungumzia mamlaka ya wakuu wa mikoa na wilaya ya kuwaweka mahabusu watu wanaoonekana wanaweza kuhatarisha amani na utulivu iwapo watakuwa huru kwa kipindi fulani.

Siyo mara ya kwanza kwa Jafo kulalamikia matumizi yasiyostahiki ya sheria hiyo, Septemba 16 mwaka jana wakati akiwa naibu waziri wa Tamisemi, aliwataka wakuu wa mikoa na wilaya kuitumia vizuri sheria inayowapa mamlaka ya kuwaweka ndani watu katika maeneo yao.

Aidha, aliyekuwa waziri wa Tamisemi, George Simbachawene naye alizungumza mara kadhaa kuonya matumizi mabaya ya sheria hiyo na mara ya mwisho ilikuwa Juni, mwaka jana alipojibu bungeni swali la mbunge wa viti maalumu (Chadema), Cecilia Pareso aliyeuliza kama Serikali ina mpango wa kuibadili sheria hiyo.

Jibu la Simbachawene kwa Pareso, lilikuwa na msisitizo wa kuwataka wateuliwa hao kuacha kuitumia sheria hiyo kama kielelezo cha kuonyesha mamlaka waliyonayo katika jamii.

Lakini juzi, Jafo akiwa sasa waziri kamili wa Tamisemi aliwataka tena wateule hao kuacha kuitumia vibaya sheria hiyo. Wakati akisema hayo, siku chache zilizopita mkuu wa wilaya ya Ilala, Sophia Mjema alimuweka mahabusu kwa saa 48 diwani wa Kitunda, Nice Gisunte.

Tunachoona hapa ni kwamba hoja ya mbunge Pareso inazidi kupata nguvu kwa kuona umuhimu wa kuibadili sheria hiyo, inayoonekana kutumika vibaya.

Hatuoni kama ni afya kwa ujenzi wa umoja na mshikamano wa Taifa, ikiwa viongozi hao wataendelea kutumia sheria hiyo kama adhabu au hukumu, badala ya malengo yaliyowekwa ya kulinda usalama na watu wengine. Imani yetu ni kwamba sheria hii kama itaachwa iendelee kutumika, itajenga tabia sugu kwa wateule hayo ‘kujiona miungu watu’ kwa kuwashikisha adabu wabaya wao.

Tunalaani tabia ya kuitumia hii sheria vibaya kwa kuwa inasababisha wananchi kuichukia Serikali kwa sababu ambazo hazina msingi wowote.

Hivyo, dhamira njema ya kutungwa kwa sheria hii inashindwa kuonekana kwa kuwa baadhi ya wateule wameamua kuitumia kuonyesha nguvu ya mamlaka zao badala ya kuitumia kuwasaidia wananchi.

Imefika wakati sasa kuufanyia kazi ushauri wa Jaji Mkuu mstaafu, Barnabas Samatta alioutoa mbele ya Rais John Magufuli akielezea umuhimu wa utawala wa sheria unaoambatana na haki.

Jaji Samatta akizungumza kwenye mkutano wa Rais Magufuli na viongozi wastaafu, alionyesha kushangazwa na amri hasa za wakuu wa wilaya kwamba nyingi zinakiuka misingi ya haki. Alisisitiza umakini wa miswada inayopelekwa bungeni kwamba lazima iangaliwe sheria itakayotungwa haitakuwa chanzo cha kunyang’anya haki ya mtu.

Kwa msingi huo, tunaona kuna umuhimu wa kuitazama upya sheria inayowapa mamlaka wakuu wa mikoa na wilaya kuwaweka watu mahabusu kwa kuwa wakati mwingine inatumika kudhulumu zao.

Tunamshauri Waziri Jafo kwa kuwa naye ameonyesha kukerwa na matumizi mabaya ya sheria hiyo, afanye utaratibu wa kuwasilisha bungeni muswada marekebisho ili hoja hiyo ifike tamati.