Vyama vya ushirika viimarike

Muktasari:

  • Ni kutokana sheria hii pia kuna Shirikisho la Vyama vya Akiba na Mikopo Tanzania (SCCULT). SCCULT ndio msingi wa kuongoza mabadiliko na maendeleo kwenye sekta ya ushirika nchini kwani ndio vyama vyenye kuwakilisha na kuwa sauti za vyama vya ushirika wa aina zote Kwa pamoja Shirikisho na chama kikuu cha ushirika wa akiba na mikopo vinasimamia ustawi wa vyama vyote vya ushirika Tanzania, na kwa maana hiyo vinapokuwa kwenye nafasi nzuri na imara basi kwa nafasi yake vinaweza kutekeleza majukumu vizuri na kuleta tija kwa wanachama na sekta nzima ya ushirika.

Sheria namba 6 ya ushirika ya mwaka 2013 katika sehemu ya nne (4) kuanzia kifungu cha 19 inatoa nafasi ya vyama vya ushirika kuungana na kutengeneza umoja wanaoona unafaa mpaka ngazi ya juu kabisa katika ushirika ambayo ni shirikisho.

Ni kutokana sheria hii pia kuna Shirikisho la Vyama vya Akiba na Mikopo Tanzania (SCCULT). SCCULT ndio msingi wa kuongoza mabadiliko na maendeleo kwenye sekta ya ushirika nchini kwani ndio vyama vyenye kuwakilisha na kuwa sauti za vyama vya ushirika wa aina zote Kwa pamoja Shirikisho na chama kikuu cha ushirika wa akiba na mikopo vinasimamia ustawi wa vyama vyote vya ushirika Tanzania, na kwa maana hiyo vinapokuwa kwenye nafasi nzuri na imara basi kwa nafasi yake vinaweza kutekeleza majukumu vizuri na kuleta tija kwa wanachama na sekta nzima ya ushirika.

Yalifanyika makosa miaka ya nyuma hasa kwenye uongozi ambayo yaliyosababisha taasisi hizi mihimili ya ushirika Tanzania kuyumba na kupoteza mwelekeo na mvuto kwa wanachama wake na wana ushirika wengi.

Hata hivyo, pamoja na changamoto hizi wanaushirika wanatakiwa kutambua umuhimu mkubwa wa taasisi hizi mbili na wasiziache katika kipindi hiki kigumu, bali wajitahidi kuwa nazo karibu ili kusaidia kwenye maeneo tofauti kuzijengea uwezo mpya zirudi kwa nguvu kusimamia vizuri masilahi ya vyama wanachama

Pamoja na kuwa vyama vya ushirika ni mali ya wanachama, ni muhimu kutambua mchango na kuingilia kati kwa Serikali kwa kupitia Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania chini ya Wizara ya Kilimo, kwa kazi nzuri ya kuwachukulia hatua watu wote waliochangia kudidimiza sekta ya ushirika nchini kwa kutumia ofisi zao vibaya na kukosa uwajibikaji.

Tunategemea mambo yaliyofanyika kwenye vyama vikuu yatakuja kwenye taasisi hizi mbili kusaidia uchunguzi na kutoa majibu ya kitaalamu ili kusaidia uhuishaji wenye tija.

Huduma za vyama hivi vikubwa zilififia na ili zirudi kwa nguvu, vyama vinatakiwa kutumia huduma tofauti zinazotolewa na taasisi hizi kama vile mafunzo, ushauri wa kitaalamu, uandaaji wa nyaraka mbalimbali za kihasibu, sera, tafiti ndogo na mambo mengine ya kitaalamu.

Ili kuyafanikisha haya ni lazima shirikisho pamoja na SCCULT kujitengenezea uwezo wa ndani kwa kuwa na mifumo thabiti ya utunzaji kumbukumbu na uendeshaji, sera na miongozo yote muhimu.

Pia kuwa na rasilimali watu kwa kuajiri vijana wenye maono mapya, wenye weledi na ubunifu kwenye sekta ya ushirika watakaosaidia kuongoza mabadiliko ya sekta hii inayokumbwa na ushindani mkubwa kwa ugumu wa kutopokea mabadiliko ya haraka kwenye dunia hii ya sayansi ya ubunifu na teknolojia

Ni muhimu wana ushirika kukumbuka uzuri wa sekta hii miaka iliyopita na namna ambavyo ilifanikiwa kipekee kabisa kusaidia maisha ya Watanzania wengi wa kipato cha chini kwa kutoa fursa mbalimbali za kiuchumi na kijamii.

Tanzania tumejaliwa kuwa na muungano tofauti wa vyama, jambo ambalo ni tofauti na nchi nyingine ambazo zinakosa shirikisho na zinakuwa na mhimili mmoja.

Wana ushirika wasisusie vyama vyao, wanatakiwa kuwa washauri na walezi wa vyama hivi vikubwa kwa kukumbuka tunu moja kati ya zile tunu sita za ushirika inayotaka ambayo ni uzalendo kwa chama chako na kuhakikisha unawajibika kwa nafasi yako na hukati tamaa kwa chama chako, badala yake wewe mwenyewe kuwa chachu ya mabadiliko.

+255 657 157 122 au [email protected]