Wenye madeni ya kodi wachangamkie fursa ya msamaha

Muktasari:

Msamaha huu umetokana na malalamiko ya wafanyabiashara waliyoyatoa kwa Rais John Magufuli kuhusu malimbikizo makubwa ya madeni ya kodi za nyuma ikiwamo riba na adhabu yanayowakabili.

Hivi karibuni Serikali imetangaza msamaha wa riba na adhabu kwenye malimbikizo ya madeni ya kodi kwa asilimia 100 tofauti na asilimia 50 ilivyokuwa hapo awali.

Msamaha huu umetokana na malalamiko ya wafanyabiashara waliyoyatoa kwa Rais John Magufuli kuhusu malimbikizo makubwa ya madeni ya kodi za nyuma ikiwamo riba na adhabu yanayowakabili.

Walitoa malalamiko hayo kwenye mkutano wa Baraza la Taifa la Biashara (TNBC) uliofanyika Machi. Rais aliwaambia wafanyabiashara hao wazungumze na Wizara ya Fedha na Mipango kupata suluhu la kudumu.

Baada ya mkutano huo, Bunge la bajeti lilipitisha marekebisho ya Sheria ya Usimamizi wa Kodi na kumpa mamlaka waziri mwenye dhamana kutoa msamaha wa riba na adhabu kwenye malimbikizo ya madeni ya kodi ya nyuma.

Baada ya marekebisho hayo, waziri amemuagiza mamishna mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kutoa msamaha maalum wa riba na adhabu kwenye malimbikizo ya madeni ya kodi kwa asilimia 100.

Kutokana na mamlaka hayo, Julai 11, kamishna wa TRA, Charles Kichere alitangaza msamaha huo kwa walipakodi wenye malimbikizo ya madeni ya riba na adhabu na kuwapa fursa ya kulipa kodi ya msingi mara moja au kwa awamu.

Msamaha huo unahusu kodi zote zinazosimamiwa na TRA ikiwamo ya mapato, maendeleo ya ufundi stadi, ongezeko la thamani (VAT), ushuru wa stempu na bidhaa, ada ya huduma za bandari pamoja na ada ya huduma ya viwanja vya ndege.

Hivyo basi, mapato yasiyo husika kwenye utaratibu huu ni yasiyo ya kodi ambayo TRA ina jukumu la kuyakusanya kama vile kodi ya michezo ya kubahatisha na majengo, tozo ya kuendeleza utalii au reli na ada za matangazo.

Aidha, Kichere aliwataja walengwa wa msamaha huu kuwa ni kampuni, taasisi na watu binafsi ambao wamewasilisha ritani ya kodi lakini bado wanadaiwa ama kodi yote au sehemu ya kodi zitokanazo na ritani hizo au ambao hawajawasilisha ritani.

Wengine ni wale ambao hawajasajiliwa na kupewa namba ya TIN au VAT na waliowasilisha pingamizi au rufaa za kodi ambazo bado zinashughulikiwa na TRA, Bodi ya Rufaa na Mahakama ya Rufani za kodi.

Vilevile aliwataja ambao hawahusiki na msamaha huu kuwa ni wale wanaostahili msamaha lakini wameshalipa madeni yao, wanaokaguliwa, wenye madeni yanayotokana na kesi za jinai za kodi, utakatishaji fedha, usafirishaji wa binadamu au shughuli nyingine haramu yaliyothibitika kisheria.

Wapo pia wenye madeni yanayotokana na adhabu zilizoamuliwa tayari au adhabu za makosa yatokanayo na uzembe wa kukusudia uliobainika kisheria pamoja na wenye riba au faini zilizotokana na kutoa au kutumia risiti za kielektroniki za kughushi.

Mwisho wa kuwasilisha maombi hayo Novemba 30 na baada ya hapo kamishna atakuwa anajibu maombi husika ndani ya siku 30 tangu alipoyapokea.

Msamaha huu umetolewa kwa kwa miezi sita kuanzia Julai Mosi mpaka Desemba 31 na madeni yanayohusika ni yaliyolimbikizwa hadi Juni 30 mwaka huu isipokuwa madeni ya wafanyabiashara wapya ambao hawajasajiliwa kama walipakodi.

Ikumbukwe, mnufaika wa msamaha huu anapaswa kuwasilisha ritani zote, kuingia mkataba wa makubaliano na kamishna wa TRA utakaoanisha deni lote, riba na adhabu inayosamehewa.

Hata hivyo, msamaha utatolewa kwa maombi yatakayokidhi vigezo vya masharti na kukubaliwa na TRA ambapo kamishna na mlipakodi husika watakuwa na makubaliano yatakayoainisha kiwango cha deni, riba na adhabu inayosamehewa. Kodi isiyo na riba wala adhabu itapaswa kulipwa kabla ya Juni 30, 2019.

Kutokana na umuhimu wa msamaha huu, ni vyema wafanyabiashara, washauri wa kodi na wadau wakawasilisha maombi kwa wakati ili kunufaika nao.

Kaimu kamishna wa walipakodi wakubwa, Alfred Mregi kwenye semina iliyofanyika katikati ya mwezi huu jijini Dar es Salaam alisema TRA ina hakikisha wafanyabiashara wengi wanajitokeza ili wanufaike kuondoa malalamiko yao ya muda mrefu.

Milango ya TRA ipo wazi kutoa elimu kuhusu msamaha huu na masuala mengine ya kodi kwa ujumla. Ni vyema walipakodio wakaitumia fursa hii kuondokana na malimbikizo ya madeni ili waweze kuimarisha biashara zao kwa manufaa yao na Taifa kwa ujumla.

Hii ni nafasi ya wafanyabiashara ambao hawajasajiliwa kukamilisha utaratibu wa kisheria utakaowaruhusu kujitanua.

Ni jambo jema kuliko kuchelewa na kusubiri kukimbizana dakika za mwisho.

Mwandishi ni ofisa habari wa TRA. Anapatikana kwa namba 0713 986 541.