Serikali iangalie upya gharama za mbegu za pamba kwa wakulima

Muktasari:

  • Ni dhahiri kwamba mwitikio huo wa kampeni hiyo iliyofanywa karibu katika mikoa yote inayolima zao la pamba, wakulima wengi waliitikia kulima kwa wingi na kila kiongozi wakiwemo wakuu wa wilaya na mikoa walizunguka kwenye maeneo yao kuhamasisha kilimo hicho.

Katika msimu wa kilimo wa mwaka 2017/2018 Serikali ilitumia nguvu kubwa kuwahamasisha wakulima walime zao la pamba ikiwa ni njia mojawapo ya kulifufua zao hilo, juhudi ambazo kwa mwaka huu zinaonyesha hazikuzaa matunda kama ilivyotegemewa.

Ni dhahiri kwamba mwitikio huo wa kampeni hiyo iliyofanywa karibu katika mikoa yote inayolima zao la pamba, wakulima wengi waliitikia kulima kwa wingi na kila kiongozi wakiwemo wakuu wa wilaya na mikoa walizunguka kwenye maeneo yao kuhamasisha kilimo hicho.

Lakini sasa pamoja na juhudi hizo kubwa ambazo pamoja na wakulima kulima pamba kwa wingi, wamepata hasara kubwa kutokana na wengi wao kutumia mbegu za kisasa ambazo zilitolewa kwa lengo la kuleta ufanisi zaidi kwa wakulima ikiwemo kupata mavuno mengi.

Kinyume na matarajio ya wengi, pamba hiyo ilistawi vizuri na kurefuka mithili ya kimo cha mtu, lakini ajabu baada ya kupata matunda yalisinyaa hayakuweza kukua tena, pengine kutokana na mvua kubwa zilizonyesha ama wakulima kutokuwa na utaalamu wa kutunza mimea hiyo ya mbegu za kisasa.

Pia wapo wengine waliosingizia dawa za kuua wadudu kwamba zilikuwa hazifai, wapo wengine waliodai kwamba mbegu hizo zilibuniwa na wataalamu kwa ajili ya kuvumilia ukame ilimradi kila mmoja alisindikiza maumivu hayo kadri alivyofikiria.

Kutokana na hali hiyo wakulima walikuwa wamekopeshwa mbegu na kampuni mbalimbali, huku pembejeo zikiwemo dawa walizokopeshwa na Serikali ambayo baada ya kuona tathimini ya uzalishaji wake uko chini kwa msimu huu iliwafutia madeni hayo.

Uamuzi huo wa kuwafutia deni wakulima hao Serikali inapaswa kupongezwa, kwani hali halisi ya wakulima wa pamba si nzuri kwa kuwa mkulima aliyelima eka 10 kwa lengo la kujipatia Sh5 milioni, aliambulia 300,000 wakati huohuo gharama za uendeshaji zikiwemo mbegu na dawa zaidi ya sh1 milioni.

Kwanza nipongeze Serikali kwa uamuzi wake wa kufuta madeni ya pembejeo zake, lakini kama kweli imedhamiria kulinyanyua zao hilo iangalie upya suala la mbegu ambazo wakulima hukopeshwa na kampuni binafsi.

Katika miaka ya 1970, pamba ilikuwa ikilimwa kwa wingi na iliingiza fedha nyingi katika uchumi wa Taifa, lakini hakukuwa na masharti ya upatikanaji wa mbegu kwani zilikuwa zikitolewa bure na vyama vya msingi.

Kwa sasa baada ya kuwepo mabadiliko hayo wanauziwa ingawa kwa mkopo.

Katika msimu wa mwaka huu, wakulima wengi wameshindwa kufanikiwa. Kwa mfano mkulima anayedaiwa laki mbili za mbegu amepata laki na ishirini baada ya kuuza pamba yake kutokana na hali niliyoielezea hapo juu.

Hivyo basi kama kweli imedhamiria kuinua kilimo cha pamba iangalie upya namna ya kulegeza masharti ya kodi kwenye kampuni za kununua ili mbegu hizo zigawiwe bure kwa wakulima kama ilivyokuwa miaka ya 1970.

Hali ya sasa ni mbaya kwa wakulima kutokana na misako inayofanywa na wakuu wa wilaya ya kukusanya fedha za mbegu kwa waliopata hasara.

Wapo wengine siku za msako wanakimbia familia zao kwa kukosa fedha za kulipa kutokana na hasara hiyo na hao wakuu wa wilaya ni lazima wafanye msako wa kusaka fedha hizo.

Nasema lazima misako ifanyike kutokana na kampuni kuingilia mikataba na halmashauri za wilaya kama wadhamini kwamba, wakulima wakishindwa kulipa kampuni hazitalipa ushuru kwa halmashauri husika.

Na ili ushuru huo ulipwe wakulima hao wanasakwa usiku na mchana kulipa fedha hizo ambazo hawana, lakini kama wangepewa bure mbegu hizo isingekuwepo hali hiyo ya kukimbia familia zao.

Mimi nasema kwamba hakuna mtu anayependa kukimbia familia yake kwa sababu anadaiwa.

Kwanza ni aibu mtu mzima kukimbia familia yake, lakini sasa analazimika kufanya hivyo kutokana na hali halisi.

Hata hao wasakaji wanatakiwa kuelewa kwamba hawakimbiwi kwa makusudi bali ni hali halisi ya maisha.

Sasa ikiwa mkulima hajavuna kitu unafikiria atakulipa nini na familia yake ile nini?

Ni bora ungewekwa utaratibu ambao utamsaidia mkulima kuhakikisha kwamba anaweza kulipa mkopo hata msimu mwingine kutokana na hali ya mavuno ilivyokuwa mbaya.

Wakulima wengi wanategemea kilimo ili waendeshe maisha, hivyo Serikali inatakiwa kuwapa nafasi kubwa wakulima hawa ili waweze kumudu hali ngumu ya maisha.

Mwandishi anafanya shughuli zake mkoani Shinyanga. Anapatikana kwa simu namba 0769 423 770