UCHAMBUZI: Kukiwa na utashi wa Serikali wakulima nchini watacheka

Muktasari:

  • Msukumo wake kwa mfano tunauona ulivyozaa matunda hasa kwa wakulima wa zao la korosho nchini.

Tangu ateuliwe kuwa Waziri mkuu, Kassim Majaaliwa, amejipambanua kama mtetezi wa wakulima.

Msukumo wake kwa mfano tunauona ulivyozaa matunda hasa kwa wakulima wa zao la korosho nchini.

Kwa wanaofuatilia zao hili wataungana nami kuwa baada ya miaka mingi ya vilio na mateso, hivi sasa wakulima wa korosho hasa mikoa ya Kusini inayoongoza kwa uzalishaji, wanafaidi matunda ya kazi ya mikono yao.

Unapoona bei ya korosho kilo moja ikifikia Sh4,000 ujue kuna nguvu kubwa nyuma ya bei hiyo.

Nguvu hiyo si nyingine, bali ni Serikali ya Awamu ya Tano chini ya ufuatiliaji wa karibu wa Waziri Mkuu Majaliwa.

Mara kadhaa amenukuliwa na vyombo vya habari akisema lazima zao hilo liwanufaishe wazalishaji wake na si watu wengine kama ilivyokuwa miaka ya nyuma.

Zamani hali ilikuwa mbaya. Kwa mfano, mfanyabiashara angeweza kutaja bei hata ya Sh300 kwa kilo na bado wakulima wakaridhia kutokana na kukosa kukosa mtetezi.

Leo wakulima wanacheka na hii ni ishara kuwa Serikali ikiamua kuwa na utashi, inaweza kuwasaidia wananchi wake na siyo tu wakulima wa korosho, bali hata kwa mazao mengine.

Kwa sababu ya utashi huo, tunashuhudia sasa zao hilo kwa mujibu wa Serikali likiongoza kuipatia pato kubwa miongoni mwa mazao yanayouzwa kwenye masoko ya nje.

Kwa mfano, taarifa ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ya Februari mwaka 2017 inaonyesha kuwa zao hilo liliingizia Serikali jumla ya Dola346.6 milioni za Marekani.

Kiasi hicho kinalifanya zao la korosho kuongoza katika kuiingizia Serikali mapato.

Nchi yetu imejaliwa kuwa na kilimo cha mazao mengi ya biashara na yenye soko zuri kimataifa, lakini wanachokikosa wakulima wetu ni utashi wa viongozi kuwaonyesha fursa na namna ya kuziendea.

Hiki kinachofanyika katika korosho kinaweza kufanywa kwa mazao mengine na wakulima wakanufaika kiuchumi na kuboresha ustawi wa maisha na hatimaye kukuza uchumi wa nchi yetu.

Nasisitiza kwamba kukiwa na utashi kama huu wa Waziri Mkuu kama tunavyoona sasa anavyoshupalia maendeleo ya korosho, pamba na kahawa na sioni sababu ya wakulima nchini kuendelea kuwa watu duni.

Kilimo kinalipa, wakulima wanahitaji watu wa kuwasemea kama alivyo Waziri Mkuu Majaliwa.

Zamani wapo waliofikia hatua ya kukisusa kilimo cha korosho kutokana na kutoridhishwa na soko hasa upunjaji wa bei na dhuluma mbalimbali walizokuwa wakifanyiwa na wafanyabiashara, lakini leo upepo umebadilika.

Raha ya zao hilo inasababisha watu kulichangamkia siyo tu kwa mikoa ya Kusini, bali hata kwenye mikoa mingine ambayo linaelezwa kuwa linaweza kustawi kama vile Ruvuma, Tanga, Singida na mingineyo.

Naamini hata suala lile la ‘hujuma’ ya korosho zetu kukutwa na vipande vya mawe, Waziri Mkuu kama kiongozi mkuu wa Serikali aliyejipambanua kuwa mtetezi wa wakulima, analijua na analiandalia mkakati mzito wa kuwashikisha adabu watu wanaotaka kuchafua jina la Tanzania katika biashara ya zao hilo.

Ukali wake uleule alionao kwa watu wanaowapunja wakulima wa korosho auhamishie kwa wote waliohusika katika tukio hili. Naamini hili analimudu.

0754990083