Thursday, December 7, 2017

Kulipa madeni ya walimu kwa wakati kutainua elimu

 

        Nianze kwa kumpongeza Rais John Magufulu kwa kauli ya kuwapa matumaini watumishi wa umma kuwa kuanzia Novemba 2017, watumishi wa umma 57,000 wangepandishwa vyeo na kungekuwa na nyongeza ya mwaka katika mishahara yao.

Kauli hiyo iliwatia moyo watumishi wa umma kwani awali walipomsikia Rais akiwaambia wajumbe wa Jumuiya ya Serikali za Mitaa (ALART) kuwa hakutakuwa na nyongeza ya mishahara, wengi hawakumwelewa.

Wafanyakazi hawakumwelewa kwa sababu Mei 1, 2016, Rais akishiriki sherehe za Mei Mosi ya kwanza Mjini Morogoro, aliwaambia wafanyakazi kuwa mwaka wa fedha wa 2016/17 hakungekuwa na nyongeza ya mishahara badala yake, angewaongeza mishahara mizuri mwaka 2017/18.

Kwa ahadi hiyo, wafanyakazi walijenga matumaini ya kuneemeka katika mwaka huu wa fedha.

Pamoja na kauli ya Rais kuwa na matumaini, bado haijaeleweka ni nini kiliahidiwa na Rais wetu. Kwanza, idadi ya watumishi watakaopandishwa madaraja katika mwaka wa fedha wa 2017/18 ni ndogo kuliko uhalisia wa mambo. Kwa wastani, walimu 35,000-40,000 hupandishwa madaraja kila mwaka. Kwa takwimu hizo, mwaka wa fedha wa 2016/17 walimu takribani 35,000- 40,000 walistahili kupandishwa madaraja na hawakupandishwa kwa maelekezo ya uhakiki wa wafanyakazi hewa.

Mwaka wa fedha wa 2017/18 idadi hiyohiyo ya walimu wanastahili kupandishwa madaraja na kufanya walimu peke yao kufikia walimu 70,000-80,000 wanaostahili kupandishwa madaraja kwa muda wa miaka miwili iliyopita.

Kwa Serikali kuwapandisha wafanyakazi 57,000 tu katika mwaka huu wa fedha, inatuma ujumbe kwamba walimu wengi hawatapandishwa madaraja. Kwa kuwa walimu ni takribani asilimia 60 ya watumishi wa umma, hivyo kati ya watumishi 57,000, walimu ni takriban 34,200 ambao wanaweza kuwa ni wale waliostahili kupanishwa madaraja katika mwaka wa fedha wa 2016/17 na wale wanaostahili kupanda madaraja kwa mwaka huu wa fedha wakasubiri mwaka ujao wa fedha.

Pili, kauli ya Rais haijaweka wazi kama kitakachoongezeka kwenye mishahara ya watumishi ni ongezeko la mishahara au nyongeza ya mwaka. Kuna tofauti kati ya ongezeko la mishahara na nyongeza ya mwaka. Ongezeko hutokana na majadiliano ya mishahara kati ya Serikali na vyama vya wafanyakazi kupitia mabaraza ya kujadili mishahara.

Kwa urahisi wa kueleweka, kuna Teachers’ Service Joint Staff Council (Baraza la Pamoja la Huduma za Walimu) ambalo hujadili mishahara ya walimu, lakini ni mwaka wa tatu halijakaa kujadili mishahara hiyo. Kinachojadiliwa kwenye baraza hilo hupelekwa kwenye Public Service Joint Staff Council (Baraza la Pamoja la Watumishi wa Umma) ambapo kunakuwa na makubaliano ya mishahara kwa mwaka husika.

Sina uhakika kama kumekuwa na makubaliano kati ya vyama vyenye uwakilishi katika ‘Public Service Joint Staff Council’ ambavyo ni TALGWU, TUGHE, RAAWU na CWT.

Vilevile, sina uhakika kama kuna makubaliano yoyote yaliyotangazwa kwenye Gazeti la Serikali kama tuzo kwa wafanyakazi baada ya majadiliano kufanyika.

Kutokuwepo kwa taarifa hizo kwa mujibu wa Sheria ya Majadiliano ya Pamoja kwenye Utumishi wa Umma ya mwaka 2003 kunaleta swali la msingi juu ya kile alichomaanisha Rais katika kuongeza mishahara Novemba.

Kwa upande mwingine, walimu sawa na watumishi wengine, wana mikataba yao ambayo wamesaini na waajiri wao ambayo inaeleza kwamba kila Julai kunakuwa na nyongeza ya mishahara (annual increment) ambayo imewekewa viwango kulingana na daraja la mtumishi. Hii iliongezwa kwa watumishi mara ya mwisho chini ya uongozi wa shemeji yetu, Jakaya Kikwete. Mwaka wa kwanza wa JPM hakukuwa na nyongeza ya mwaka kwa maelezo yaleyale ya uhakiki wa wafanyakazi hewa.

Walimu ambao ni takribani asilimia 60 ya watumishi wa umma hulipwa takribani asilimia 49 ya mishahara inayolipwa na Serikali kila mwezi kwa mujibu wa takwimu za mwaka 2009. Kwa hali hiyo, wingi wa walimu hauathiri malipo kutokana na kuwa na mishahara midogo ukilinganisha na watumishi wa kada zingine wenye elimu na viwango sawa ya elimu.

Walimu wanapolalamikia kutolipwa kwa madeni yao, akili zao hazitulii ili watoe elimu bora. Ninatoa wito kwa Serikali kufumba macho na kulipa madeni yote ya walimu ili kuwapa haueni ya kufanya kazi kwa bidii.

Walimu wasiopata motisha, hata wakisimamiwa kwa fimbo na wakuu wa mikoa, wilaya au waziri, hawawezi kutoa elimu bora kwa watoto.     

-->