Kuna zaidi ya mapokezi katika ujio wa Fifa

Muktasari:

Kati ya Februari 20 na 24, Tanzania itakuwa na ugeni wa juu katika soka duniani.

Kati ya Februari 20 na 24, Tanzania itakuwa na ugeni wa juu katika soka duniani.

Rais wa Shirikisho la Kimataifa la Soka (Fifa), Gianni Infantino na Rais wa Shirikisho la Soka Afrika (CAF), Ahmad Ahmad watakuwa nchini kwa kikao cha kawaida kujadili masuala mbalimbali ya maendeleo ya soka Afrika na dunia kwa jumla.

Mkutano huo utakaoshirikisha nchi wanachama 19 wa Fifa, utakaofanyika kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNICC), unajulikana kwa jina la “Fifa Executive Football Summit”. Mataifa hayo 19, yatawakilishwa na Rais na katibu wake mkuu wa kila shirikisho.

Tanzania ni nchi pekee katika Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati iliyopewa heshima ya kuandaa mkutano huo ambao pia utajadili masuala ya soka la wanawake, vijana na mfumo wa usajili wa kielektroniki wa TMS ambao kwa sasa utakuwa chini ya Fifa wenyewe na si wakala.

Hii ni mara ya kwanza kwa kiongozi mkubwa wa Fifa kutembelea Tanzania na kubwa zaidi ni kupewa nafasi ya mkutano huo wa siku moja ambao viongozi wa mashirikisho ya soka katika nchi mbalimbali watashiriki.

Pia madhumuni ya mkutano huo ni kuirejesha Fifa kwenye mpira wa miguu na mpira wa miguu kwa Fifa, kupanga mikakati ya maendeleo ya siku za usoni ikiwa ni pamoja na mataifa 12 duniani kupewa heshima ya kuandaa mikutano hiyo.

Pamoja na hatua hiyo, tunachukua fursa hii kuitaka Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Soka Tanzania, TFF, kujipanga kuiomba Fifa kusaidia maendeleo ya soka.

Tumesikia Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe akisisitiza kuwapa mapokezi makubwa, sasa pamoja na hayo mapokezi inatakiwa kuwa na ajenda muhimu za maendeleo.

Kuna maeneo mengi yanahitaji msaada wa Fifa, ujenzi wa viwanja vya kisasa kama si kuviboresha, ujenzi wa vituo vya kuendeleza soka, ukiacha hicho cha TSA kilichopo Karume.

Tutafanya kosa la mwaka kuwapa mapokezi makubwa ambayo si dhambi pia, lakini kikubwa ni maendeleo na ujenzi wa miundombinu ya soka.

Pamoja na Fifa, yapo mataifa yaliyoendelea katika mchezo huo na ni kati ya wenyeviti na makatibu 19 kutoka kona mbalimbali za dunia wanaoandamana na msafara wa Fifa kuja Tanzania.

Viongozi wa TFF wanaweza kutengeneza urafiki na zaidi kuangalia wapi pa kuweka nguvu kwa maendeleo ya mchezo huo nchini. Kuna maeneo mengi kama vile ubadilishanaji uzoefu, kuomba msaada wa wakufunzi wa makocha ngazi mbalimbali kwa maana soka ya vijana, wanawake na wakubwa.

Pia, madaktari wa michezo, waamuzi na makamishna wa mchezo, matumizi ya teknolojia katika soka na mambo mengine kwa maendeleo ya soka Tanzania.

Tuna imani TFF watachangamka katika hili badala ya kutaka kuwaonyesha mapokezi makubwa na ukarimu. Hayo yanaweza kufanyika, lakini msingi zaidi uwe kwa maendeleo ya mchezo huo.

Tunadhani, itapendeza kama TFF itaandaa taarifa zake na kuwapatia viongozi wa vyama vya soka na zaidi ziara za mafunzo hasa kwa timu za taifa ya Tanzania, Taifa Stars. Huu ndiyo wakati wa kuchangamkia neema ambayo hatudhani kama itarudi tena, japo ni uamuzi wa Rais wa Fifa na kamati yake ya utendaji kuamua kurudi Tanzania. Tunataka kuona baada ya muda mfupi, matunda ya ujio wa Fifa yanaanza kuonekana kwa misaada na mambo mengine kwa maendeleo ya soka la Tanzania.

Tunawatakia mkutano wa amani ili siku nyingine Fifa wakumbuke na warudi Tanzania kwa kuwapa heshima nyingine.