Kuongezeka ubakaji, ulawiti si habari njema

Muktasari:

Taarifa hizo zilitolewa na msamaji wa Jeshi la Polisi, Kamishna Msaidizi Barnabas Mwakalukwa wakati alipofanya ziara kwenye ofisi za kampuni ya Mwananchi Communications Limited inayozalisha magazeti ya Mwananchi, The Citizen na Mwanaspoti.

Wakati Taifa likifanya jitihada za kukabiliana na uhalifu, hasa wa kutumia silaha ambao umepoteza maisha ya watu wengi, Jeshi la Polisi limesema vitendo vya ubakaji na ulawiti vinazidi kukua.

Taarifa hizo zilitolewa na msemaji wa Jeshi la Polisi, Kamishna Msaidizi Barnabas Mwakalukwa wakati alipofanya ziara kwenye ofisi za kampuni ya Mwananchi Communications Limited inayozalisha magazeti ya Mwananchi, The Citizen na Mwanaspoti.

Mwakalukwa alisema kuwa kuongezeka kwa vitendo hivyo kumebainishwa na jamii kuanza kuelewa ubaya wa ubakaji na ulawiti na hivyo kutoa taarifa vituo vya polisi.

Alisema vitendo vingi vinahusisha watoto wadogo na ndugu wa familia ambao hukaribishwa majumbani na kuwekwa chumba kimoja na hivyo kupata fursa ya kufanya vitendo hivyo.

Mwakalukwa pia alisema wazazi wamesahau majukumu yao ya ulezi na hivyo kutoyatekeleza ipasavyo, jambo linalotoa mwanya kwa watoto kujifunza vitendo viovu.

Alisema matukio mengine yanaripotiwa baada ya wasichana wanaofanya kazi ya uchangudoa kutolipwa kwa kadri ya makubaliano na wateja wao.

Ongezeko la vitendo hivyo, kwa mujibu wa Mwakalukwa, linachangiwa na wazazi au ndugu kutokuwa tayari kutoa ushirikiano kwa Jeshi la Polisi pale mtoto anapobakwa au kulawitiwa na ndugu wa familia, wakihofia hatua kali dhidi ya mtenda kosa.

Pia wazazi kutotekeleza vyema wajibu wao wa malezi na jamii kutoshirikiana kulea watoto, ni jambo jingine linalofanya vitendo hivyo vizidi kuongezeka.

Kwa upande wa madada poa, vitendo hivyo vya ulawiti hufichwa pale wateja wanapokubali kufanya malipo kwa mujibu wa makubaliano, jambo ambalo linalea na kukuza vitendo hivyo viovu.

Pia alisema maendeleo ya kiteknolojia yanasababisha watoto kujifunza mambo yasiyofaa.

Taarifa hizi si nzuri hata kidogo kwa Taifa ambalo limeshafikisha zaidi ya miaka 50 ya uhuru, likiwa limejenga misingi yake ya kiutamaduni, kijamii na kisiasa ambayo inatokana na historia yake.

Kama wanasaikolojia wanavyosema, vitendo vya ubakaji na ulawiti huathiri sana wanaofanyiwa kiasi cha kupendelea kujitenga na wengine hata kujidhuru kwa kuona wameshushiwa hadi yao katika jamii.

Bahati nzuri, uwezo wa kudhibiti vitendo hivyo uko ndani ya mamlaka yetu na hauhitaji nguvu ya ziada au fedha za kigeni kukabiliana navyo, bali kudhamiria kwa dhati kuondoa uozo huo.

Kama Taifa lililojengwa katika misingi ya kijamaa, jukumu la malezi ya mtoto yoyote yule ni la jamii nzima. Kila mtu katika jamii anao wajibu wa kuhakikisha vitendo kama hivyo havitokei mbele ya macho yake akaviacha vikapita bila ya hatua kuchukuliwa.

Ni muhimu kwa kila mtu katika jamii kuhakikisha anatoa taarifa za mtu yeyote anayejaribu kumfanyia ukatili mtoto yoyote bila ya kujali kama ni wake, au wa jirani, anamjua au hamjui.

Pia wazazi hawana budi kuangalia kwa makini mahusiano yao na ndugu wa familia na jinsi kuishi nao. Ni kweli kwamba ndugu wengi wanapotembelea familia fulani, hulazwa kwenye vyumba vya watoto. Utamaduni huu hauna budi kuangaliwa upya ili kutowaweka ndugu wa familia katika mazingira yanayoweza kuwapa mwanya kufanya vitendo hivyo.

Pia kumekuwepo na malezi ya kudekeza watoto kwa kuwaachia kufanya watakayo. Watoto wanaruhusiwa kuangalia televisheni hadi usiku wa manane bila ya kujua wanaangalia nini. Wengine wamemilikishwa simu ambazo huwekewa fedha za kutosha kuwawezesha kufungua hata vitu visivyo na maadili ya Kitanzania.

Hii ni hatari. Jamii haina budi kupambana na tatizo hilo kwa kila hali kwa kuwa uwezo wa kulishinda uko mikononi mwetu.