Kupiga madaktari, wauguzi hakukubaliki

Muktasari:

  • Habari hiyo ilimnukuu mkurugenzi mkuu wa Bugando, Dk Abel Makubi akisema ndugu hao walifanya kitendo hicho baada ya kupewa taarifa kwamba mgonjwa wao waliyempeleka hospitalini hapo siku iliyopita alikuwa amefariki dunia usiku.

Gazeti hili toleo la jana kulikuwa na habari iliyosema ndugu wawatembezea kichapo muuguzi, walinzi Bugando. Habari hiyo iliyotoka mkoani Mwanza ilieleza kuwa walinzi watatu na muuguzi mmoja wa Hospitali ya Rufaa ya Bugando, wamejeruhiwa baada ya kutembezewa kichapo na ndugu wa mgonjwa aliyefariki dunia wakiwatuhumu wafanyakazi wa hospitali hiyo kwa uzembe.

Habari hiyo ilimnukuu mkurugenzi mkuu wa Bugando, Dk Abel Makubi akisema ndugu hao walifanya kitendo hicho baada ya kupewa taarifa kwamba mgonjwa wao waliyempeleka hospitalini hapo siku iliyopita alikuwa amefariki dunia usiku.

Dk Makubi alisema ndugu baada ya kupewa taarifa ya kifo cha mgonjwa wao walivamia hospitalini hapo na kuwapiga walinzi na muuguzi waliokuwa zamu usiku. Tunalaani kitendo kilichofanywa na ndugu hao kwani mgonjwa kupoteza uhai wakati akipatiwa matibabu siyo jambo geni.

Mgonjwa anayepoteza uhai akiwa hospitali kunaweza kuwa na sababu nyingi za kitabibu, hata uzembe wa watendaji wa hospitali unaweza ukachangia, lakini kama mgonjwa ama ndugu wana malalamiko kuna utaratibu wa kufuata ili hatua zichukuliwe.

Kinachoshangaza ni kitendo cha ndugu hao kuvamia hospitali usiku, kumpiga muuguzi ambaye hawana uhakika kama ndiye aliyekuwa akimtibu mgonjwa wao, lakini baya zaidi ni kuwapiga walinzi ambao hawahusiki kabisa na kutibu wagonjwa.

Tunachoona hapa vitendo hivi kama wahusika hawatachukuliwa hatua kali za kisheria vitaendelea kutokea na kuna hatari baadhi ya watu wakageuza uhuni huo kuwa ndiyo njia sahihi ya kuwaadhibu watendaji wa hospitali.

Ni wazi vitendo hivi vya kuwapiga, kuwadhalilisha na kuwatukana madaktari na wauguzi wa hospitali vinaendelea siku hata siku. Mfano, Machi 2016 madaktari na wauguzi wa Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Mtwara, Ligula, waligoma kutoa huduma baada ya mwenzao kudaiwa kupigwa na ndugu wa mgonjwa hadi kuvuliwa nguo.

Daktari aliyepigwa na kudhalilishwa, Saini Dickson aliliambia gazeti hili kwamba tukio hilo lilitokea baada ya kuwaeleza ndugu wa mgonjwa aliyekuwa amepelekwa hapo baada ya kupata ajali ya pikipiki kwamba amempa rufaa ya kwenda Hospitali ya Taifa Muhimbili.

Ndugu hawakuridhika mgonjwa wao kupewa rufaa Muhimbili, wakamtaka daktari huyo awape rufaa ya hospitali ya Nyangao au Ndanda, hata hivyo Dk Dickson akawaeleza hawezi kumtoa mgonjwa hospitali ya rufaa ampeleke hospitali ya chini na hilo ndio likawa kosa lake, wakaamua kumpiga na kumvua nguo.

Cha kushangaza hadi sasa hakuna taarifa za kukamatwa kwa watuhumiwa wa vurugu za Hospitali ya Rufaa Mtwara zaidi ya kuelezwa walitoroka. Lakini, kuna taarifa waliofanya vurugu Bugando wamekamatwa. Ni vema watuhumiwa wa kuwapiga madaktari na wauguzi wakafikishwa kwenye vyombo vya sheria ili kukomesha matukio ya namna hiyo.

Pia, tunawaomba madaktari na wauguzi nao wajiepushe na lugha za kuudhi kwa ndugu wenye wagonjwa wao hospitali au kwa wagonjwa wenyewe. Yapo malalamiko ya uzembe wa madaktari na wauguzi katika kuhudumiwa wagonjwa, ni vema watendaji hawa wakaishi viapo vyao na watekeleze majukumu yao kwa weledi.

Lakini, hata ndugu na jamaa wenye wagonjwa wao hospitali na wagonjwa wenyewe wazingatie utaratibu wa kufikisha malalamiko yao, kuna masanduku ya kutoa maoni na pia kuna ofisi za kufikisha malalamiko. Wazitumie njia hizo kuendeleza uhusiano mzuri kwa kuwa muuguzaji naye kuna siku ataugua.