Kuwatelekeza wagonjwa wa akili kunaigharimu jamii yetu

Muktasari:

  • Kuna mtu ameweka makazi kwa zaidi ya mwaka sasa. Iwe mvua au jua, mavazi yake ni yaleyale tangu alipoonekana eneo hili kwa mra ya kwanza. Anakaa kando ya barabara na kuomba chochote kwa wapita njia.

Tupa jicho kando ya barabara fupi ya lami inayotenganisha kituo kikuu cha polisi Bukoba na jengo la Wakala wa Huduma ya Ununuzi Serikalini(GPSA).

Kuna mtu ameweka makazi kwa zaidi ya mwaka sasa. Iwe mvua au jua, mavazi yake ni yaleyale tangu alipoonekana eneo hili kwa mra ya kwanza. Anakaa kando ya barabara na kuomba chochote kwa wapita njia.

Ukipita karibu yake, utasikia manung’uniko. Anataja kesi mahakamani na muda wote macho anayaelekeza kwa watu wanaoingia na kutoka.

Hakuna anayejua sababu za manung’ung’uniko na za kuchagua kuweka makazi eneo hili. Hakuna anayejua akiwazacho kichwani. Hatujui ni lini akili itamtuma kulipa kisasi dhidi ya binadamu waliomtenga.

Ugonjwa wa akili ni tatizo kubwa katika jamii na ni sehemu ya magojwa yasiyopewa kipaumbele.

Ungekuwa unatiliwa maanani, pengine mganga wa jadi, Jilumba Mabula wa kijiji cha Ididi, Wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga, asingeuawa wakati akimpatia mgonjwa wake dawa kwa nguvu.

Katika tukio hilo la Februari, 2016 mganga huyo aliuawa baada ya kupigwa kwa jembe kichwani na mgonjwa aliyepelekwa kwa matibabu, kwa kile kilichoaminiwa alikuwa mgonjwa wa akili.

Mgonjwa huyo alipelekwa kwa mganga wa jadi, badala ya hospitali maalumu walipo wagonjwa wa aina hiyo.

Yapo matukio mengi ya kutisha yanayohusishwa na watu wenye matatizo ya afya ya akili. Mwaka 2010 mwanamke katika kijiji cha Kaiwa mkoani Kilimanjaro aliwaua watoto wake watatu kwa shoka.

Aliyekuwa Kamanda wa Polisi wakati huo, Lucas Ng’hoboko alisema uchunguzi ulionyesha mtuhumiwa alikuwa na matatizo ya akili na alipelekwa hospitali ya Mawenzi kwa matibabu.

Ugonjwa wa akili huathiri uwezo wa kufikiri na mhusika kushindwa kudhibiti hisia zake na tabia; mara nyingi hali hiyo huambatana na madhara makubwa.

Ni bahati mbaya kuwa watu wanaojikuta katika hali hii wanabaguliwa, kunyanyaswa kwa njia mbalimbali ikiwa ni pamoja na kutengwa.

Mara nyingi hukumu inayotolewa dhidi yao, inajengwa juu ya msingi wa ushirikina na uchawi bila kurejea sababu za kihistoria, kijamii na kisaikolojia.

Huyo anayeonekana kwa zaidi ya mwaka mmoja akinyeshewa mvua na jua kando ya barabara ya polisi mjini Bukoba, ni miongoni mwa maelfu ya wagonjwa wa akili wanaokosa haki zao kama binadamu.

Ana haki ya kupata uangalizi maalumu na matunzo kama inavyotaka Sera ya Afya ya mwaka 2007 na huduma bila malipo kwa wagonjwa wa kundi hilo.

Taarifa iliyotolewa na Serikali wakati wa maadhimisho ya Siku ya Afya ya Akili Duniani mwaka 2015,ilionyesha mwaka 2014/2015 Watanzania 817,532 walikuwa wakiugua magonjwa mbalimbali ya akili.

Mkoa wa Dar es salaam ulitajwa kuongoza kwa idadi kubwa ya wagonjwa ukifuatiwa na Dodoma, huku Mkoa wa Lindi ukiwa na idadi ndogo zaidi.

Kwa mujibu wa Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii,Wazee,na Watoto, Ummy Mwalimu wakati wa hotuba ya Makadirio ya mapato na matumizi ya wizara yake kwa mwaka 2017/2018, bado kuna changamoto ya tatizo la magonjwa ya akili.

Alisema hospitali ya Mirembe iliyopo mkoani Dodoma, imeendelea kutoa tiba kwa wagonjwa wa akili na kawaida ikiwa ni pamoja na wagonjwa wa akili ambao ni wahalifu.

Kundi la wagonjwa wa akili wenye historia ya uhalifu, wanaweza kusababisha madhara makubwa zaidi ikiwa wataachwa bila uangalizi maalumu na kupatiwa matibabu.

Hospitali ya Mirembe kwa miaka minne iliyopita kuanzia mwaka 2012 hadi 2016, imetoa huduma za afya kwa wagonjwa wa akili zaidi ya 60,000 miongoni mwao ni waathirika wa dawa za kulevya.

Mwananchi huyu pamoja na kutia huruma, pia anaturejesha katika tukio la mgonjwa wa aina hiyo aliyevamia gari la aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Kagera John Mongella na kulivunja vioo kwa mawe.

Ni shambulio la Disemba 12, 2014 nje ya ofisi za Chama Cha Mapinduzi (CCM)mjini Bukoba. Mongela na wenzake walikuwa wakijiandaa kukagua ujenzi wa maabara.Tiba aliyopewa ni kufungiwa mahabusu mpaka ziara ilipomalizika.

Aidha, tayari tumesahau tukio la Novemba moja,2011 pale mtu aliyetajwa kuwa na tatizo la afya ya akili alipovamia shule ya msingi Kabutaigi wilayani Muleba na kumuua kwa panga Anisia Goodluck aliyekuwa mwanafunzi wa darasa la nne.

Mtuhumiwa huyu aliyeishi na jamii bila matunzo na matibabu sahihi, akahukumiwa kifo kwa kupigwa mawe na wanafunzi wenye hasira.

Phinias Bashaya ni mwandishi wa Mwananchi Kagera.0767489094